Profesa Ngowi: Wananchi washirikishwe katika miradi ya maendeleo

0
699

Leonard Mang’oha-Dar es Salaam

Wakati leo Serikali ikisoma bajeti kuu ya mwaka wa fedha 2019/2020, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Profesa Honest Ngowi, ameshauri wananchi kujengewa mazingira ya kushiriki katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo ili kuweza kunufaika na kasi ya ukuaji uchumi.

Ametoa kauli hiyo leo Juni 13, jijini Dar es Salaam katika mjadala wa bajeti unaofahamika kama Kijiwe cha Kahawa, ulioandaliwa na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP).

Profesa Ngowi amesema kushirikishwa kwa wananchi katika utekelezaji  wa miradi hiyo kutapunguza villio vya wananchi wanaodai kuwa licha ya uchumi kudaiwa kukua hali ya maisha imeendelea kuwa ngumu.

Amesema hapa nchini sekta zinazoonekana kukua zaidi ni zile zinazotumia mitambo katika utekelezaji wake ikilinganishwa na sekta kama vile kilimo ambazo ukuaji wake ni mdogo.

“Kama inakuwa sekta inayotumia mitambo, kinacholipwa ni ile mitambo, kwa hiyo uchumi unaweza kukua lakini fedha haziingii mfukoni.

“Ni lazima kuwe na mgawanyo mzuri wa kisekta kwa sababu uchumi unaweza kukua kwa kujenga SGR na Stigler’s lakini kama kina dada na kina kaka wa Tanzania hawatashiriki hawawezi kuona uchumi unakua,” amesema Profesa Ngowi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here