24.4 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Profesa Mwandosya amshika pabaya Dk. Slaa

MwandosyaNa Debora Sanja, Dodoma
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi Maalumu), Profesa Mark Mwandosya ‘amemvaa’ Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willibrod Slaa na kusema kwamba kiongozi huyo amekosa uzalendo kwa hatua yake ya kuizungumza vibaya Tanzania akiwa nje ya nchi.
Profesa Mwandosya alitoa kauli hiyo bungeni jana wakati akichangia mjadala wa Bajeti ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Utawala Bora, Uhusiano na Uratibu kwa mwaka wa fedha 2015/16.
Ingawa hakumtaja kwa jina, Profesa Mwandosya alisema anamshangaa kiongozi anayeenda nje ya nchi na kuisema vibaya nchi yake.
Hivi karibuni, Dk. Slaa alikwenda Marekani kutembelea vyuo mbalimbali ambako taarifa za mitandao zilimnukuu akisema vyombo vya dola katika Tanzania vimekuwa vikifanya ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu na kutesa raia wasio na hatia.
“Anaweza kutoka kiongozi, mwananchi akaenda nje ya nchi akaisema nchi yake vibaya, hiki ni kitu cha ajabu sana, watakushangilia huku wanakushangaa.
“Hakuna Mmarekani, Mjerumani anayeizungumzia nchi yake vibaya nje ya nchi yake, lakini yeye anakwenda nje ya nchi anasema oh… tunateswa, oh sheria ziko hivi, hakuna haki za binadamu watakupigia makofi lakini moyoni wanakushangaa wanasema wewe mtu wa ajabu,” alisema Profesa Mwandosya.
Alisema nchi za nje siasa zao zipo ndani ya nchi na kwamba hata katika familia mambo ya ndani hayawezi kuzungumziwa nje ya familia.
“Sasa kiongozi mmoja alikwenda Marekani huko akatusema, akasema haki za binadamu, atatupeleka The Hague, wale walimshangilia lakini walimshangaa.
“Na wanavyotudharau sasa wakasema tutawaletea pia wanasheria wawasaidie. Jamani, yaani sisi hatujasoma hata sheria, hata upande huo, hili jambo liliniuma sana,” alisema Profesa Mwandosya.
Alisema mambo ya ndani ya nchi yazungumzwe ndani ya nchi na mtu anapotoka nje ya nchi atambue kwamba yeye ni Mtanzania.
Aaga rasmi ubunge
Wakati huo huo, Profesa Mwandosya alitumia nafasi hiyo kuwashukuru wananchi wa Rungwe Mashariki na kuliambia Bunge kuwa hatawania tena nafasi hiyo badala yake anatarajia kuwatumikia Watanzania katika nafasi nyingine.
“Miaka 15 ya kupita bila kupingwa jimboni ni mingi sana, ni wakati wa kuwaachia wengine wapokee kijiti, lakini huo ndiyo mwanzo wa kulitumikia taifa katika ngazi nyingine.
Akijibu baadhi ya hoja za wabunge katika mjadala huo, alitaka wabunge kumheshimu Rais kama taasisi na siyo kumzungumzia kwa dhihaka.
“Huwezi kumzungumzia Rais kama mbunge wa kawaida, heshima ya Rais ipo duniani kote, tulinde heshima ya Rais ili kujenga utamaduni ambao hata watoto na wajukuu wataheshimu,” alisema.
Mwandosya pia alisisitiza staha ndani ya Bunge kwa kuwa heshima ya mtu hujengwa kutokana na jinsi anavyozungumza.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles