30.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Profesa Muhongo mtegoni

profmuhongo*Apata kigugumizi kuzungumzia ushiriki wake sakata la mita za kupimia mafuta

*Aponzwa na meseji aliyomtumia Mkurugenzi aliyetumbuliwa jipu Bandari, mwenyewe azungumza

NA AZIZA MASOUD, DAR ES SALAAM

UJUMBE mfupi wa  maneno alioutuma Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo kwa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Vipimo nchini (WMA),  Magdalena Chuwa,  akimtaka awashe  mita ya kupimia mafuta kwa sababu tu Waziri Mkuu Kassim Majaliwa anafanya ziara bandarini umezua maswali na kuacha wingu la shaka.

Mashine hiyo (flow meter) ambayo haijawahi kuwashwa kwa takribani miaka mitano  tangu inunuliwe kwa gharama inayozidi Sh bilioni 12, imesababisha jana Waziri Mkuu, Majaliwa awasimamishe kazi watendaji wawili wa WMA, akiwemo Chuwa na Meneja Vipimo Kitengo cha Mafuta, Bernadina Mwijarubi, ili kupisha uchunguzi wa upotevu wa mafuta bandarini kutokana na zuio la kutotumia mita hiyo kupima nishati hiyo.

Tayari ujumbe huo wa Muhongo umezua mjadala mkubwa katika maeneo mbalimbali, ikiwemo mitandao ya kijamii, wengine wakidai kuna namna na huenda Waziri huyo alikuwa anajua kinachoendelea Bandarini kuhusu wizi wa mafuta.

Wengine wamekwenda mbali na hata kujenga hisia kwamba huenda ujumbe huo usingetumwa Waziri Mkuu Majaliwa angekuta hali mbaya zaidi, huku wengine wakitaka achukuliwe hatua kama ilivyochukuliwa kwa wengine.

Juzi Chuwa alimwambia Waziri Mkuu kuwa sababu ya  kuwasha mita hiyo imetokana na kutumiwa ujumbe mfupi na Profesa Muhongo kuwa ahakikishe anawasha kifaa hicho  ndani ya saa 24.

“Mita imeanza kufanya kazi jana (Jumatano) kutokana na maagizo yaliyotolewa ngazi za juu, nilitumiwa meseji (ujumbe mfupi) kutoka kwa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Muhongo aliagiza ianze kazi ndani ya saa 24,” alisema Chuwa.

Baada ya  kutoa maelezo hayo, Waziri Majaliwa alimtaka Chuwa aseme kama serikalini wanafanya kazi kwa utaratibu wa ujumbe mfupi, lakini alishindwa kujibu.

Kutokana na ujumbe huo kuzua maswali, gazeti hili lilimtafuta Profesa Muhongo kwa njia ya simu ili kuweza kutolea ufafanuzi suala hilo, japo hakupokea simu lakini alipotumiwa maswali kwa njia ya ujumbe mfupi alijibu.

Maswali na majibu kati ya gazeti hili na Profesa Muhongo yalikuwa ni kama ifuatavyo;

Mwandishi: Habari Profesa Muhongo. Mimi naitwa Aziza Masoud, mwandishi wa gazeti la Mtanzania, nilikuwa naomba kujua kwa nini kitengo cha upimaji mafuta kilikuwa hakifanyi kazi, na ilikuwaje ukaandika ujumbe juzi kuwa kifanye kazi. Je, tunaweza  kupata ufafanuzi kwako kama waziri mwenye dhamana.

Profesa Muhongo: Flow meters hizo zinamilikiwa  na kusimamiwa na wakala wa vipimo (Weight & Measures) ambayo iko chini ya Wizara ya Biashara na Viwanda, waulize wakusaidie.

Swali: Asante, nimeelewa maelezo yako, lakini tulikuwa tunataka kujua kwa nini uliamuru ziwashwe, maana Mtendaji Mkuu wa WMA katika maelezo yake kwa Waziri Mkuu anadai ulimtumia ujumbe mfupi kumueleza aziwashe, tukaona kama unaweza ukawa unajua chanzo.

Profesa Muhongo: Waulize, hazipo chini yangu, mbona hutaki kwenda Wizara ya Viwanda na Biashara???????

Mwandishi: Ok, jioni njema, asante Profesa.

Profesa Muhongo: Nashukuru kwa kuelewa.

Profesa Muhongo ameingia katikati ya sakata hilo wakati ambako uteuzi wake katika Serikali ya Magufuli ukizua mjadala mkubwa kutokana na kuhusishwa na kashfa ya Escrow, wakati akiwa Waziri wa Nishati na Madini katika serikali iliyopita.

Ingawa katika serikali iliyopita  katika uchunguzi wake ilimsafisha Profesa Muhongo, hata hivyo, alivyoteuliwa katika serikali ya awamu ya tano, hatua hiyo ilipigiwa kelele na baadhi ya wanasiasa, akiwemo Mbunge wa  Singida Mashariki, Tundu Lissu pamoja na Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe, wakiapa suala hilo kulirejesha bungeni.

Wakati Profesa Muhongo akikwepa kuzungumzia ujumbe aliomtumia  Chuwa, taarifa iliyotolewa jana na Ofisi ya Waziri Mkuu ilieleza kuwa uamuzi wa kumsimamisha Mtendaji huyo Mkuu wa WMA na Meneja wa  Vipimo Kitengo cha Mafuta, Mwijarubi ulifikiwa kwenye kikao cha Makatibu Wakuu kilichofanyika jana ofisini kwake, jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo,  Waziri Mkuu Majaliwa amemwagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Dk. Adelhelm Meru, awaandikie barua za kuwasimamisha kazi watendaji hao kuanzia muda huo ili kupisha uchunguzi.

“Katibu Mkuu Viwanda, waandikie barua za kuwasimamisha kazi ili kupisha uchunguzi, katika kipindi hiki hawatatakiwa kusafiri kwenda popote hadi uchunguzi utakapokamilika, pia utafute mtu wa kukaimu nafasi hiyo ili kazi ziendelee,” alisema.

Alisema mbali na masharti hayo, ofisi yake pia itawaandikia barua ofisi ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na Jeshi la Polisi wafuatilie suala hilo mara moja.

Alisema baada ya uchunguzi endapo itathibitika kuwa watendaji hao walihusika  na hujuma hizo, hatua rasmi zitachukuliwa na ikithibitika hawakuhusika watarudishwa kazini.

Katika taarifa hiyo pia Waziri Mkuu Majaliwa ameagiza mfumo wa upimaji mafuta kwa kutumia flow meters uendelee kutumika na ule upimaji wa kukadiria uache kutumiwa mara moja.

Katika ziara ya juzi pia alikagua flow meters za zamani zilizopo Kurasini (Kurasini Oil Jetty), kisha kutembelea na kukagua flow meters mpya ambazo zinajengwa Kigamboni.

Alisema mita hizo zimegharimu dola za Marekani milioni 6 (sawa na Sh bilioni 12.96 za sasa).

Pia Waziri Mkuu alitembelea sehemu ya kuchukulia mafuta yanayotoka bandarini (TPA Manfold) iliyoko Kigamboni na kukagua mitambo ya kusambazia mafuta kwenye matenki ya mafuta ya kampuni ya TIPER yaliyoko Kigamboni, yanayomilikiwa kwa ubia baina ya Serikali na Kampuni ya Oryx Energies.

Katika ziara hiyo ilibainika kuwa Kampuni ya TIPER imejiunganishia bomba la moja kwa moja kutoka kwenye bomba kubwa la mafuta linalotoka Bandarini, hali iliyomlazimu Waziri Mkuu kuagiza kwamba bomba hilo litolewe kwenye maungio hayo ndani ya mwezi mmoja.

“Jana (juzi) niliagiza kuwa bomba hilo ling’olewe, nimetoa mwezi mmoja ili kurekebisha mfumo huo, simamieni vizuri na kuhakikisha kuwa na wao pia wanarudi kwenye manfold kama ilivyo kwa wengine,” alisema Waziri Mkuu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles