27.9 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Profesa Maghembe alia hujuma miradi ya maji

Profesa Jumanne Maghembe
Waziri wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe

Na Fadhili Athumani, Mwanga

WAZIRI wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe, amesema kuna baadhi ya watu wamejipanga kukwamisha miradi ya maji ili aonekane mzembe.

Amesema katu hatokubali kuona hali hiyo na ameahidi kuhakikisha miradi yote ya maji nchini inatekelezwa na kukamilika kwa wakati.

Kauli hiyo aliitoa katika mkutano wa hadhara wilayani Mwanga jana, uliofanyika katika Ofisi ya CCM Kata ya Lembeni.

Aliwataka wakandarasi waliopewa kazi ya kujenga visiwa virefu vya maji kuhakikisha wanakamilisha kazi hiyo kwa wakati.

Profesa Maghembe ambaye pia ni mbunge wa Mwanga kwa tikei ya CCM, alisema atapambana kwa nguvu zake ili kushirikiana na Kijiji cha Kisangara, kuhakikisha mradi huo wa kisima kirefu unakamilika kwa wakati.

“Nikiwa ndiye waziri mwenye dhamana ya wilaya hii ya Mwanga, nitahakikisha miradi yote inakamilika kwa wakati kwa nchi nzima. Ninajua kuna watu wamejipanga kukwamisha miradi hii ili Maghembe aonekane mzembe.

“Ninatoa agizo kwa viongozi wa mamlaka ya maji, wakandarasi na halmashauri mhakikishe miradi yote ya maji inakamilika kwa wakati uliopangwa,” alisema.

Alisema wapo watu wachache wasiopenda maendeleo ambao wamekuwa wakihujumu miradi ya maji kwa kutumbukiza taka ngumu katika mabomba na visima vilivyopo.

Kuhusu mradi wa maji Kisangara, aliiagiza Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga kuhakikisha inachimba kisima kingine.

Alisema wizara yake imekwisha kuagiza pampu mpya pamoja na mabomba yatakayoongezwa katika mradi huo .

“Tumeshaagiza pampu na mabomba mapya yaletwe…pampu hizi na mabomba yakifika nataka nipate taarifa kuwa yamefungwa na ikiwezekana mwaka huu huu kazi hii likamilike,” alisema Profesa Maghembe.

Naye mkandarasi aliyepewa kazi ya kujenga mradi huo wa maji, Mwakilishi wa Kampuni ya Howard Humphrey Tanzania Ltd, Felis Fidelism, alisema utekelezaji umekwisha kuanza kwa kuchimba mitaro kwa ajili ya kupitisha mabomba ya maji.

Alisema mradi huo unatarajia kukamilika mapema kama walivyoagizwa na Waziri Maghembe na unatarajiwa kuwahudumia wananchi wapatao 800.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles