31.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Prof. Ndalichako: Elimu ya msingi itaendelea kuwa miaka saba

Na OSCAR ASSENGA-PANGANI

WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako, amesema wanafunzi wanaosoma kupitia mtaala mpya watasoma kwa miaka saba kwa elimu ya msingi kama ilivyokuwa awali.

Aliyasema hayo juzi mjini hapa wakati wa kongamano la elimu lililoenda sambamba na harambee ya kuchangia ujenzi wa mabweni ya wanafunzi wa Shule ya Sekondari Mwera.

Profesa Ndalichako alisema suala la muda wa elimu ya msingi lipo kwa mujibu wa sheria ya elimu ya mwaka 1982.

“Sheria hiyo imeweka bayana kwamba muda wa elimu ya msingi ni miaka saba na bado haijafanyiwa marekebisho,” alisema Profesa Ndalichako.

Alisema kukiwa na ulazima wa kuongeza miaka ya wanafunzi kusoma shule ya msingi, kitakachotanguliwa ni kufanya marekebisho ya sheria kwa sababu jambo linalokuwa ndani ya sheria huwezi kulifanyia mabadiliko bila kuanza kufanya marekebisho ya sheria husika.

“Niwatoe hofu Watanzania kwamba suala la kisheria huwezi kubadilisha kwa tamko wala waraka wa kamishna wa elimu au kubadilika kwa maelekezo mengine yoyote, linaweza kubadilika pale Sheria ya Elimu 1982 kwenye kipengele kinachoeleza muda wa elimu ya msingi miaka saba kitakapofanyiwa marekebisho,” alisema Profesa Ndalichako.

Alisema baada ya kufanyiwa marekebisho ndiyo inaweza kubadilika na haitakuwa kinyumenyume na itawekwa bayana kwa sababu badiliko kama hilo ni kubwa la sera na kisheria, hivyo watu watafahamu mapema.

“Kumekuwa na mchanganyiko kwa sababu sera ya elimu ya mwaka 2014 imeonyesha Serikali itakuja kuweka utaratibu, lakini haikusema itaweka lini kwamba elimu ya msingi iwe lazima mpaka sekondari.

“Bado hatujawa tayari kuwa na elimu ya msingi na sekondari kwa wanafunzi wote, hivyo tunaendelea kuboresha elimu ya msingi na sekondari kuhakikisha mazingira mazuri ya kufundisha na walimu wa kutosha,” alisema Profesa Ndalichako.

Alisema watakapoona wamefika mahali na kuona haja ya kufanya mabadiliko, Serikali itawashirikisha wadau wote.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Pangani, Zainabu Issa, alimweleza Profesa Ndalichako namna walivyohamasisha elimu wilayani humo ili kuwapa uelewa wananchi juu ya umuhimu wake.

“Kutokana na awali kuwa na hali ambayo si nzuri kwa elimu wilayani hapa, mimi na Mbunge wa Jimbo la Pangani, Jumaa Aweso, tulikwenda studio kurekodi nyimbo za kuhamasisha elimu, tunashukuru Mungu hali imebadilika na elimu imekuwa ikipewa kipaumbele,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles