25.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

PROF. MWANDOSYA ATEMA NYONGO

  • Ashangaa watu kufanyiwa uadui katika masuala ya kitaifa

Na EVANS MAGEGE

WAKATI Taifa likiadhimisha miaka 18 leo ya kumbukumbu ya kifo cha mwasisi wake, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, mwanasiasa Profesa Mark Mwandosya amekumbushia kile kilichopata kusimamiwa na Mwalimu, juu ya umuhimu wa uhuru wa mawazo.

Mwandosya, ambaye tangu ajikite kwenye mbio za urais mwaka 2015 na kushindwa kwa mara ya pili na zaidi amekuwa akikosoa  mwenendo wa mambo mbalimbali, alisisitiza kuwa, watu hawawezi kupingana au kugeuka maadui kwa jambo lenye manufaa kwa Taifa.

Profesa Mwandosya, ambaye ni Mwenyekiti mpya wa Bodi ya Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, aliyasema hayo jana, katika mahojiano na MTANZANIA Jumamosi, mara baada ya kumaliza kikao chake cha kwanza cha ndani na viongozi wa chuo hicho, kilichoko Kigamboni, jijini Dar es Salaam.

Akijibu swali kuhusu malengo ya Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere juu ya umuhimu wa kuwapo kwa vyama vingi hapa nchini, Profesa Mwandosya alisema katika jambo lenye manufaa kwa Taifa watu hawawezi kupingana, ingawa wanaweza kupishana mikakati ya kufikia lengo.

Akifafanua hoja hiyo, alisema hata mikakati haiwezi kuwafanya watu wakagombana, kuraruana au kuwa maadui, kwa sababu ni kitu kizuri kinachotoa mwanya au mawazo mbadala ya kufikia lengo.

Alisema hata kabla ya kuwapo kwa vyama vya siasa, viongozi au watawala waliamini katika uongozi wa pamoja, ambao unawashirikisha watu nini cha kufanya.

Alisema ukiachilia mbali ubinafsi wa watu, hasa viongozi wa vyama vya siasa, kikiwamo CCM, malengo ya utaifa hayapishani.

“Mfumo wa vyama vingi lazima ujikite katika misingi ya kitaifa ya Kiafrika, hata kabla ya vyama bado jamii ya Kiafrika ilikuwa na mfumo wa viongozi au watawala,” alisema Profesa Mwandosya.

Akikumbushia nyakati za Mwalimu Nyerere, alisema walikuwa wana kitu kinaitwa uongozi wa pamoja au maamuzi ya pamoja, ambayo watu wanakaa na kukubaliana nini chenye manufaa kwa taifa.

“Kitu chenye manufaa kwa taifa kinacholeta maendeleo, hicho unaweza kusema tu kwamba tunachopishana ni mikakati ya kufikia lengo, lakini mikakati haiwezi kufanya mkagombana, kuraruana au kuwa maadui, kwa hiyo ni kitu kizuri ambacho kinatoa mwanya au mawazo mbadala. Ingawa mawazo mbadala yanakuwa na lengo lile lile la kumfanya mwananchi aweze kuwa na maendeleo zaidi,” alisema.

Akizungumzia miaka 18 ya kifo cha Nyerere, Profesa Mwandosya alisema, Hayati Baba wa Taifa aliishi kabla ya wakati wake.

Alisema hali hiyo inatokana na kila alichokizungumza kwamba  kinaonekana kama utabiri kwa sasa.

“Mwalimu Nyerere alikuwa mbele yetu kwamba yale ambayo tunazungumza au kutaka kuyafanya sasa yeye alikuwa ameisha yasemea na kuyatekeleza,” alisema.

Aliongeza kwamba, Nyerere alikuwa na upeo wa juu zaidi kuliko wale aliokuwa anawaongoza.

“ Kwa kweli ni kama vile tulimsikitisha kwa sababu hatukwenda naye na hatukuwa watu wa wakati wake, yeye alikuwa mbele yetu na mbele ya wakati, alisimama katika utu wa Mwafrika, uhuru wa Mwafrika, uhuru wa binadamu na kumheshimu binadamu,” alisema.

Profesa Mwandosya, ambaye amepata kutumikia kwa miaka 10 katika serikali ya Rais Jakaya Kikwete, alisema jambo ambalo Mwalimu Nyerere hakufanikiwa, ingawa lengo lake lilikuwa zuri, ni kuanzisha Umoja wa Afrika, ambao matokeo yake yamekuwa hasi kuliko alivyokuwa anategemea.

Akizungumzia suala la ufisadi, mfano wizi wa rasilimali za nchi, hususan madini, Profesa Mwandosya alisema hawezi kuwalaumu watu waliojihusisha kwa namna moja au nyingine kufisidi nchi, kwa sababu watu hao hawakutoka kwenye sayari nyingine.

“Watu hawa ni sehemu ya jamii, ni watoto wetu, ni ndugu zetu, cha msingi kwa sasa ni kujiangalia sisi wenyewe ndani ya jamii kwamba tunawezaje kutoa sasa vijana ambao wanalipenda Taifa lao, lakini katika utaifa ni wadadisi na katika udadisi vilevile wana maadili au watakwenda kuwa watumishi katika mazingira ya kulisaidia Taifa,” alisema Prof. Mwandosya.

Akizungumzia uteuzi wake wa kuongoza Bodi ya Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, Profesa Mwandosya, ambaye pia amepata kuwa mbunge wa Rungwe Mashariki kwa miaka 15, alisema anajisikia fahari na heshima kubwa kupewa nafasi ya kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo hicho, chenye jina kubwa la heshima.

“Mbali na fahari, lakini vilevile nabeba uzito mkubwa kwa matarajio ya aliyeniteua, pia matarajio ya Taifa juu ya chuo hiki,” alisema.

Alisema matarajio ya chuo hicho  yalipoanzishwa yalikuwa ni kutoa zao la wahitimu ambao watakwenda kuongoza Taifa katika maeneo mbalimbali kwa kujikita katika maadili na misingi ya utu, uadilifu na utawala bora.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles