31.2 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Prof. Muhongo abaini chanzo cha jipu Tanesco

Profesa Sospeter MuhongoNA ELIYA MBONEA, ARUSHA

WAZIRI wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, ameliagiza Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), kuacha kununua transfoma kutoka Kampuni ya Quality Group na Inter Trade.

Profesa Muhongo alitoa agizo hilo mjini hapa jana alipotembelea kiwanda cha kutengeneza transfoma cha Tanelec.

Akiwa kiwandani hapo, Profesa Muhongo alishangaa Tanesco kuacha kununua bidhaa inazozalisha na kununua mali kutoka nje ya nchi kwa kisingizo cha sheria ya manunuzi ya umma.

Kampuni zinaoiuzia Tanesco transfoma hizo kwa mujibu wa sheria ya manunuzi ni Inter Trade iliyoshinda zabuni kwa dola za Marekani milioni 5 na Quality Group inayomilikiwa na mfanyabiashara wa jijini Dar es Salaam, Yussuf Manji iliyoshinda kwa dola za Marekani milioni 3.

“Ununuzi wa transfoma hizo kutoka nje, kwa ujumla wake umeendelea kugubikwa na vitendo vya rushwa kutokana na ukweli kwamba kampuni zilizoshinda tenda hizo hazizalishi transfoma.

“Hawa hawazalishi transfoma, badala yake nao wananunua huko India na kuja kuiuzia Tanesco.

“Cha ajabu ni kwamba pamoja na kutokuwa na viwanda vya transfoma, walishinda tenda na kumwacha Tanelec anayezalisha transfoma, hii ni rushwa ya wazi,” alisema Prof. Muhongo na kuongeza.

“Kuanzia sasa, nimepiga marufuku kuagiza transfoma kutoka nje ya nchi, badala yake mnunue zinazozalishwa na Tanelec. Hii ni sawa na mtu umesaga unga wa matumizi ya nyumbani halafu anajitokeza mtu na kukukataza kuutumia akitaka ununue unga wa dukani, huo ni uhuni.

“Mahitaji ya Tanesco kwa mwaka ni takribani transfoma 1,500 hadi 2,000, hivyo upo uwezekano mkubwa wa transfoma hizo kupatikana hapa nchini pasipo sababu ya kutangatanga.

“Ni jambo la kushangaza kwa Tanesco kukimbilia kununua transfoma nje ya nchi wakati wanajua kabisa wao wanamiliki hisa asilimia 20 na Shirika la Maendelea la Taifa (NDC) nalo likimikili hisa asilimia 10 kwenye Kiwanda cha Tanelec,” alisema Profesa Muhongo.

Kwa upande wake, Meneja Kiwanda cha Tanelec, Zahir Saleh, alisema kwa sasa wanazalisha transfoma 7,000 ingawa lengo ni kuzalisha 10,000.

Salehe alimuomba Waziri Muhongo kuangalia namna Serikali itakavyoweza kuwabana au kuweka sheria itakayowabana Watanzania kununua bidhaa zao kwa asilimia 40 kama ilivyo nchini Kenya.

“Sheria ya manunuzi imewanyima Tanesco uhuru wa kununua bidhaa zetu na hii imetusababishia kupunguza wafanyakazi 60 kutokana na kupungua kwa uzalishaji,” alisema Salehe.

Katika hatua nyingine, Salehe alisema kiwanda hicho kwa sasa kinazalisha transfoma zenye uwezo wa kupambana na radi wakati wa mvua.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles