30.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Prof. Lipumba achambuliwa kila kona

Profesa Ibrahim Lipumba
Profesa Ibrahim Lipumba

CHRISTINA GAULUHANGA NA JAMILA SHEMNI, DAR ES SALAAM

SIKU moja baada ya aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba kutangaza nia ya kurejea ndani ya chama hicho, wasomi na wanasiasa mbalimbali wamemchambua wakisema amepoteza mwelekeo hafai kurejea ndani ya chama hicho.

Wakizungumza na MTANZANIA kwa nyakati tofauti, walisema wana CUF wana changamoto ya kurejea Katiba yao na kuona kama kiongozi huyo anafaa kurejea au la, lakini pia watafakari uamuzi wake wa awali kama ulikuwa na mashiko ndani ya chama.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino, Profesa Mwesiga Baregu  alisema inasikitisha kuona Profesa Lipumba amekosa ukomavu wa siasa.

“Kuna mambo ukiyafanya yana athari zake yanaweza kuleta matokeo chanya au hasi hivyo, kabla hujafanya ni lazima ujitafakari…hivyo Lipumba alitakiwa kubeba madhara yoyote yatakayotokea kwenye uamuzi wake wa awali,”alisema Profesa Baregu.

Alisema kiongozi au mwanachama yeyote ukishafanya   usaliti kisha ukageuka nyuma ni lazima watu wakose imani na wewe.

Makamu Mwenyekiti wa Chadema,  Profesa Abdallah Safari,   alisema Profesa Lipumba anapenda kuabudiwa  hivyo wana CUF wanatakiwa wajiulize tangu ajiuzulu wamepungukiwa nini.

Alisema kwa sasa CUF ni wakaipitia katiba yao na kuona kuna sababu za kumrejesha madarakani.

“Enzi za uongozi wake kwani alifanya nini ndani ya chama? Tunafahamu fika alikuwa na wabunge wachache tofauti na hivi sasa hivyo sioni kama kuna haja ya kumrejesha madarakani,”alisema Profesa Safari.

Akielezea kuhusu Umoja wa Vyama vinavyounda Katiba (Ukawa), alisema Profesa Lipumba alijiuzulu baada ya kubanwa akidai hamtaki aliyekuwa mgombea Urais kwa tiketi ya vyama vinavyounda Ukawa, Edward Lowasa.

“Tunachoshindwa kukiamini ni vipi anataka arejee ndani ya chama wakati Lowasa yupo Kamati Kuu. Atafanyaje naye kazi wakati yeye hamtaki…hatumuamini huyu mtu ni kigeugeu,”alisema Profesa Safari.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Benson Bana,  alisema Profesa Lipumba amepoteza sifa kwa sababu kuyumba siyo sifa ya kiongozi.

“Kiongozi lazima awe na msimamo …kuyumba siyo sifa ya kiongozi, kurejea kwake hakuna tija kwa vile  enzi za uongozi wake hakuna alichokifanya ndani ya chama,”  alisema Dk.Bana.

Alisema waliomshauri wamemshauri vibaya kwa vile sababu zilizomfanya ajiuzulu alipaswa  ajiulize kabla ya kuandika barua kuwa akirejea ndani ya CUF  sababu hizo zitakuwa zimekwisha.

“Hakuna alichokifanya ndani ya miaka 20 ya uongozi wake akiwa CUF na hivyo ni vema akaendelea kuwa mwanachama au mshauri wa chama hicho,”alisema Dk.Bana.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles