Pombe haiongezi damu kwa wajawazito, inaathiri mtoto

0
448

Na VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM

UPUNGUFU wa damu kipindi cha ujauzito ni tatizo linalowakumba wanawake wengi, si tu Tanzania pekee bali hata katika mataifa mengine duniani.

Shirika la Afya Duniani (WHO) linakadiria theluthi moja ya wajawazito hukumbwa na tatizo hilo katika kipindi cha miezi mitatu ya mwisho ya ujauzito.

Tatizo la upungufu wa damu linatajwa kuchangia asilimia kati ya nne hadi 16 ya vifo vitokanavyo na uzazi duniani, linapotokea katika kipindi cha ujauzito huongeza uwezekano wa madhara kwa mtoto ikiwamo kifo.

Hali ilivyo nchini
Matokeo ya utafiti wa afya na viashiria vya malaria wa mwaka 2015/16 yanaonesha upungufu wa damu kwa watoto wenye umri wa kati ya miezi sita hadi 59 ni wastani wa asilimia 58.

Utafiti huo unabainisha kuwa asilimia 26 wanakabiliwa na upungufu wa damu wa kawaida, asilimia 30 wana upungufu wa damu wa kati na asilimia mbili wana upungufu wa damu wa juu.

Aidha, baadhi ya mikoa ukiwamo Shinyanga unaonesha hali ni mbaya zaidi ambapo asilimia 71 ya watoto chini ya miaka mitano wana upungufu wa damu.

Utafiti huo unaonesha asilimia 45 ya wanawake nchini walio katika umri wa kuzaa (miaka 15 hadi 49) wanakabiliwa na tatizo la upungufu wa damu.

Utafiti huo unaeleza asilimia 33 wana upungufu wa damu wa kawaida, asilimia 11 wana upungufu wa damu wa kati na asilimia moja wana upungufu wa damu wa juu.
Kwa mujibu wa utafiti huo, asilimia kiwango cha upungufu wa damu kwa Unguja ni asilimia 60 na Mkoa wa Kaskazini Pemba ni asilimia 72.

Simulizi ya Halima
“Niliolewa mwaka 2015, nimebahatika kupata mtoto mmoja hadi sasa, ujauzito wangu ulikuwa na changamoto nyingi mno hadi najifungua nilimshukuru Mwenyezi Mungu,” anasema Halima Jumanne Mkazi wa Mbezi.

Anasema alipata tatizo la kupungukiwa damu na kwamba ilibakia kidogo tu ujauzito wake ungeharibika.
“Sasa unajua tena huku mitaani kuna ushauri wa kila aina, hospitalini walinieleza napaswa kutumia vidonge maalum ili kuongeza damu na kula mboga mboga za kutosha.
“Lakini rafiki yangu mmoja alikuja na kunishauri niwe nakunywa angalau glasi moja ya pombe kila wiki kwani inasaidia kuongeza damu.

“Nikawa nakunywa kila Jumamosi, lakini kila nilipokwenda kliniki waliponipima waliona bado kiwango changu ni kidogo, ikabidi wanipumzishe hospitali (bed rest) na wakawa wanafuatilia hali yangu kwa ukaribu hadi nilipojifungua.

“Siku moja nikamsimulia daktari wangu kuhusu hilo, alinishangaa mno na kunieleza ningepoteza mtoto kwa sababu pombe ina madhara mengi kiafya,” anasema.

Johari Mbunda anasema kuna simulizi nyingi juu ya faida za pombe kwa mjamzito huko mitaani, kwamba husaidia kuimarisha afya na kusaidia kuongeza damu.

“Ni kweli, ushawishi upo tena kwa kiwango cha juu, hata mimi nilipokuwa mjamzito niliwahi kushawishiwa na jirani yangu ninywe pombe inaongeza damu, sikunywa kwa sababu imani yangu hainiruhusu kutumia kinywaji hicho,” anasema.

Sababu ya damu kupungua

Kipindi cha ujauzito huambatana na mabadiliko mbalimbali ya mwili, moja ya mabadiliko hayo ni ongezeko la maji (plasma volume) katika mzunguko wa damu.

Katika mtandao wa Ackyshine, inaeleza katika hali hiyo ingawa kiasi cha damu huonekana kuongezeka, kiwango cha hemoglobini hupungua hadi kufikia 11.5mg/dl.

Inakadiriwa takribani asilimia 85 ya anaemia (upungufu wa damu) wakati wa ujauzito husababishwa na upungufu wa madini ya chuma mwilini.

Kulingana na mtandao huo, upungufu wa madini ya chuma unaweza kusababishwa na kula chakula chenye kiasi kidogo cha madini hayo au mwili wa mjamzito kushindwa kutunza madini  chuma ya kutosha kutokana na ama mimba zilizopita au kupoteza kiasi kingi wakati wa hedhi kabla ya kushika mimba.

Sababu nyingine ni upungufu wa madini ya folic acid, ugonjwa wa selimundu, lishe duni kabla na wakati wa ujauzito, kupoteza damu kwa sababu ya kuumia au kuwa na minyoo na upungufu wa Vitamin B12.

Mtandao huo unataja sababu nyingine kuwa ni kuugua ugonjwa wa malaria wakati wa ujauzito, ugonjwa wa chembe damu nyekundu uitwao kitaalamu beta thalassaemia ambao huwapata zaidi watu waishio Asia Kusini, Ulaya Kusini na Afrika.

Unataja sababu nyingine kuwa ni ugonjwa sugu wa kuvunjika chembe damu nyekundu (chronic haemolysis), kupoteza hemoglobin kupitia mkojo, saratani ya damu (leukemia), matatizo ya kupoteza damu kwenye njia ya chakula na matatizo ya utumbo wakati wa ujauzito.

Visababishi
Mtandao huo unaeleza zipo sababu za kijamii, kiuchumi na kiafya ambavyo vinaweza kusababisha mama kupata tatizo hilo.

Kuna suala la umri wa mjamzito, kiwango cha elimu na uelewa kuhusu afya yake, mazingira anayoishi na hali ya kiuchumi pia huweza kuchangia.

Sababu nyingine ni afya ya uzazi kwa ujumla, historia ya mimba zake, uzazi wa pacha, uvutaji wa sigara, unywaji wa pombe na kutohuduria kliniki kipindi cha ujauzito, ugonjwa wa kisukari, figo na shinikizo la damu.

 

Madhara mengine

Madhara kipindi cha ujauzito ni kukonda au kuongezeka uzito kwa kiasi kidogo, kuhisi uchungu kabla ya muda, kondo la nyuma kutunga pasipostahili, shinikizo la damu wakati wa ujauzito na chupa kupasuka kabla ya wakati.

Kipindi cha kujifungua ni kupatwa na uchungu usioeleweka na usio wa kawaida, mtoto kuvuja damu ndani kwa ndani, kupatwa mshtuko, hatari ya ganzi (anesthesia risk) kwa anayefanyiwa upasuaji na moyo kushindwa kufanya kazi.

Baada ya kujifungua ni kupata maambukizi, kizazi kushindwa kurudi katika hali ya kawaida au damu kuganda kwenye mishipa. Aidha, kwa mtoto madhara ni kuzaliwa njiti, kuzaliwa na uzito mdogo, ukuaji duni na kupungukiwa damu mara kwa mara.

Dalili
Mtandao huo unaeleza mjamzito mwenye upungufu wa damu wa kawaida mara nyingi anaweza asioneshe dalili zozote.

Hata hivyo, iwapo upungufu ni mkubwa, dalili za awali ni pamoja na uchovu wa mara kwa mara na kupumua kwa shida, kukosa hamu ya kula, mapigo ya moyo kwenda kasi na kuchafuka kwa tumbo.

Wakati wa uchunguzi mjamzito anaweza kuonekana mweupe kuliko kawaida hasa sehemu za viganjani, kucha za vidoleni, ulimi au macho na anaweza pia kuwa na dalili za kuvimba miguu.

Daktari.
Daktari Mashombo Mkamba, anasema hakuna faida yoyote anayoipata mwanadamu (si tu mjamzito) pindi anapokunywa pombe aina yoyote ile (ya kienyeji au ya kisasa).

“Jamii ielewe wazi pombe si tiba wala kinga dhidi ya upungufu wa damu, hakuna faida ya pombe kwa mwili wa binadamu na hatari huongezeka maradufu kwa mwanamke hasa anapokunywa kipindi kabla ya ujauzito, wakati wa ujauzito na baada ya ujauzito.

“Ifahamike vyema, ikiwa mjamzito anakunywa pombe au dawa yoyote ya kulevya vivyo hivyo na mwanaye tumboni hunywa.

“Hii ni kutokana na ukweli kwamba dawa hizi husafiri kupitia damu ya mama na kumfikia mtoto kupitia kondo la nyuma  (Placenta),” anasema.

 

Athari zaidi

Daktari huyo anasema hakuna kiwango salama cha pombe katika ujauzito kwa hiyo ni vyema kuacha kabisa.

“Kwa sababu kibaiolojia viungo vya binadamu huumbwa na kukamilika ndani ya kipindi cha miezi tisa tangu kutungwa kwa ujauzito katika tumbo la mwanamke.

“Sasa pombe ina madhara makubwa kwa mtoto aliye tumboni kwani husababisha kuharibika kwa mfumo wa mishipa ya fahamu na hata kusababisha kasoro mbalimbali za maumbile yake ‘fetal alcohol syndrome’,” anasema.

Kulingana na kituo cha Kudhibiti Magonjwa cha Marekani (CDC), hali hiyo husababisha watoto kuzaliwa wakiwa na kichwa kidogo na hata matatizo ya akili.

Dk. Mkamba anasema hali ya mtoto kuzaliwa na kichwa kidogo ni dalili ya wazi ya kuathirika kwa ubongo na kwamba wengine huzaliwa na uso wenye kasoro nyingi, ugonjwa wa akili au tabia zisizo za kawaida.

Anasema madhara ya pombe na dawa zingine za kulevya mengi huonekana katika hatua mbalimbali za kukua kwa mtoto katika maumbile au viungo vyake.

 

Kuharibika mimba

Anasema unywaji wa pombe kwa kiwango chochote iwe ya asili au ya kisasa huongeza uwezekano mkubwa wa kuharibika kwa mimba.

“Ndiyo maana huyo mama ilibidi apewe ‘bed rest’ ikiwa angeendelea na tabia ile ya kunywa pombe nakuhakikishia ujauzito wake ungeharibika na kutoka,” anasisitiza.

 

Kujifungua mtoto njiti

Anasema unywaji wa pombe unaweza pia kusababisha mtoto kuzaliwa na uzito pungufu na au mimba kupitiliza umri wa kawaida (miezi tisa).

“Hata hivyo, madhara mengine yanaweza kuonekana au yasionekane mara tu mtoto anapozaliwa lakini yataanza kujitokeza kadiri mtoto husika anavyokua.

“Wengi huonesha udhaifu mkubwa katika kufikiri, kusikia, kuamua, kufanya jambo na au kuonekana kuwa na uchangamfu usio wa kawaida,” anabainisha.

 

Ushauri

Anasema matumizi ya pombe yana madhara makubwa kiafya, hivyo jamii inapaswa kupewa elimu sahihi kuanzia ngazi ya kaya, shule za msingi hadi vyuoni.

“Aidha, sheria zilizopo ni vema zikaangaliwa upya kwani hazijaleta matokeo mazuri dhidi ya unywaji pombe nchini na tafiti ziendelee kufanyika kubaini kiwango cha athari ya unywaji pombe katika nyanja mbalimbali,” anasema.

Anasisitiza ni muhimu wanawake kuanza mapema kuhudhuria kliniki pindi tu wanapojihisi kuwa wamebeba ujauzito na wazingatie ushauri wanaopatiwa na wataalamu wa afya si vinginevyo ili kulinda afya zao na mtoto au watoto wao tumboni.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here