26.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

POLISI YAANZA KUSAKA WATOTO 1,300 WALIOTOWEKA KIBITI

NA MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM

JESHI la Polisi mkoani Pwani, limesema limeanza kuwasaka wanafunzi 1,300 wanaodaiwa kutoweka wilayani Kibiti.

Kauli hiyo imekuja siku moja baada ya gazeti dada la hili la MTANZANIA kumnukuu Mkuu wa Jeshi la Polisi, Inspekta Jenerali (IGP) Simon Sirro, akisema kuwa taarifa za kutoonekana kwa watoto hao zimetoka Idara ya Elimu na Wazazi.

IGP Sirro ambaye alizungumzia suala hilo alipokuwa katika ziara ya kikazi mkoani Pwani mapema wiki hii, hata baadaye alipozungumza na chumba hiki cha habari alisisitiza kuwa:-

“Kama mtoto humwoni shuleni wala nyumbani ni lazima uripoti.”

Jana MTANZANIA Jumamosi, lilimtafuta Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Jonathan Shana, ambaye alisema msako wa watoto hao utafanywa kwa kushirikiana na walimu pamoja na wazazi wao.

Kamanda Shana pamoja na kuwataka baadhi ya watu kupingana na hisia kwamba watoto hao wamejiunga na vikundi vya kigaidi, alisisitiza kuwa Jeshi la polisi litakuja na majibu sahihi kuhusu mahali walipo watoto hao.

“Tumekubaliana kufanya operesheni ili kuhakikisha watoto hao wanapatikana, taarifa hii inashtusha kwa kuwa wapo watu ambao wanahusisha kupotea kwa watoto hao na ugaidi, wanadhani wamejiingiza katika vikundi hivyo jambo ambalo si kweli,” alisema Kamanda Shana.

Alisema operesheni hiyo pia itawagusa watoto ambao wanashindwa kuhudhuria masomo yao kwa sababu  ya mashinikizo ya wazazi ikiwemo kuwafanyisha kazi za nyumbani.

“Watoto ambao hawaendi shule tumepanga kushirikiana na walimu kupita nyumba hadi nyumba kuhakikisha tunawashurutisha wazazi kuwaamrisha watoto wao waende shule kama sheria inavyotaka, sheria ipo wazi katika hilo,” alisema Shana.

Taarifa za kupotea kwa watoto hao katika kipindi cha kati ya mwaka 2016 na Julai mwaka huu, zilipatikana juzi wakati IGP Sirro alipofanya ziara ya kikazi wilayani Kibaha, Pwani.

Katika ziara hiyo, IGP Sirro alizungumza na wazazi, walimu, viongozi wa mashirika ya umma, wazee maarufu, wastaafu mbalimbali na kamati ya ulinzi na usalama mkoani Pwani kuhusu taarifa hizo.

Kupitia mkutano huo, IGP Sirro, alieleza taarifa ya wanafunzi zaidi ya 1,300 mkoani humo ambao hadi sasa hawajulikani walipo na hawajaonekana shule wala katika familia zao.

IGP Sirro alisema huenda watoto hao ni watoro, hivyo aliwataka wazazi washirikiane na Jeshi la Polisi kujua walipo.

Pia aliwataka wazazi kusaidiana na walimu wa shule za msingi na sekondari, ambazo wanafunzi walikuwa ni watoro ama hawajaripoti shule kwa miezi kadhaa, kutoa taarifa kwani wapo baadhi ya watoto wanaotumika kufundishwa uhalifu hata wa kutumia silaha na watu wasio wema.

Kutokana na utata wa taarifa hizo, gazeti la MTANZANIA la jana lilizungumza na IGP Sirro, ambaye alisema taarifa za kutoonekana kwa watoto hao zinatokana na Idara ya Elimu na wazazi.

“Ni taarifa ya muda mrefu, kipindi cha mwaka jana na mwaka huu, ni zaidi ya mwaka mmoja niliipata Wizara ya Elimu kule, ndiyo maana nimeelekeza wazazi ambao hawawaoni watoto wao kutoa taarifa.

Hadi sasa haijaelezwa wanafunzi hao waliopotea ni wa shule za msingi au sekondari.

Taarifa hizo zimekuja katika wakati ambao hali ya usalama katika wilaya ya Kibiti na Rufiji imeimarika tofauti na miezi kadhaa iliyopita, lilipoibuka kundi la wahalifu ambao walikuwa wakiua watu wakiwamo askari polisi.

Mauaji yaliyotikisa wilayani humo yalisababisha si tu hofu bali baadhi ya watendaji kukimbia vituo vyao vya kazi.

Hivi karibuni IGP Sirro alisema hali ya usalama imerejea katika maeneo hayo yaliyokumbwa na mauaji na zaidi alisisitiza kuwa wahalifu waliokuwa wakitekeleza vitendo hivyo vya kinyama wamekimbilia katika nchi jirani ya Msumbiji.

MATUKIO YALIYOTIKISA KIBITI

Aprili 14 mwaka huu, askari wanane waliuawa na watu wanaodhaniwa kuwa ni majambazi katika Kijiji cha Makengeni wilayani Kibiti.

Januari 19, mwaka huu, mjumbe wa Serikali ya Kijiji cha Nyambunda, Oswald Mrope, aliuawa baada ya kupigwa risasi mbele ya familia yake.

Februari 3, 2017, watu wasiojulikana walivamia nyumba ya Mwenyekiti wa Kijiji cha Jaribu, Bakari Msanga na kuichoma moto, huku yeye mwenyewe akifanikiwa kutoroka.

Februari mwaka huu, watu watatu akiwamo Ofisa Upelelezi wa Wilaya (OC CID) ya Kibiti mkoani Pwani, Mrakibu wa Polisi, Peter Kubezya, waliuawa kwa risasi.

Machi mosi, Mwenyekiti wa Kijiji cha Nyambunda, Said Mbwana, aliuawa.

Aprili 29 mwaka huu, mkazi wa Kijiji cha Mgomba Kaskazini, Kata ya Mgomba, Ikwiriri, Hamad Malinda, aliuawa kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana.

Mei 5, mwaka huu kada wa CCM Wilaya ya Rufiji mkoani Pwani, Amir Chanjale, aliuawa kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana.

Oktoba 24, 2016 Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Nyambunda, Ally Milandu, alipigwa risasi na kufa na Novemba 6, 2016 Mwenyekiti wa Kitongoji cha Nyang’unda Kijiji cha Nyambunda, Mohammed Thabiti, alipigwa risasi akielekea kwake.

Wengine waliouawa ni Ofisa wa Misitu ambaye alikuwa Mkaguzi wa Kituo cha Ukusanyaji mapato ya ushuru katika Kijiji cha Jaribu, Peter Kitundu na Rashid Mgamba ambaye ni mlinzi, mgambo ambao walipigwa risasi kichwani na begani na walikufa papo hapo eneo la tukio.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles