Imechapishwa: Fri, Oct 13th, 2017

POLISI WANAPOTUHUMU PANYA KUTOWEKA KWA MIHADARATI

TAIFA la India daima huwa haliishiwi na kila aina ya vituko kuanzia katika ngazi za kifamilia hadi taifa.

Mbali ya vituko linaongoza duniani kwa kuwa na watu wenye maajabu fulani yasiyo ya kawaida kama vile miili au viungo vya mwili vya ajabu, uwezo wa kushika moto bila kuungua, ndoa zisizo za kawaida na kadhalika.

Linapokuja suala la watu wenye maajabu fulani au vioja usivyoweza kuvipata popote pale, India inaongoza duniani.

Kwa upande wa vyombo vya usalama ikiwamo polisi navyo haviko nyuma kwa vioja.

Mathalani polisi wa taifa hilo wamewahi mara kadhaa kuwatuhumu njiwa kuwa chanzo cha usalama wa taifa hilo kukaribia kuhatarika kwa kupenyeza taarifa za kijasusi kwa maadui. Ndege hawa wamekuwa wakikamatwa na kuwekwa mahabusu wakisubiri kujibu kesi.

Kadhalika ni katika taifa hili katoto kachanga kamewahi kukamatwa na kuunganishwa katika kesi ya kutishia kuua. Hii ndiyo India!

Kadhalika wamewahi kuwatuhumu panya kuwa washukiwa wa kutoweka kwa maelfu ya lita za pombe zilizokamatwa na kuwekwa kama kidhibiti.

Sasa polisi hao wamewatuhumu panya kuwa washukiwa wa upotevu wa magunia ya mihadarati kilo 34, ikiwa ni hitimisho la uchunguzi wa miaka mitatu, baada ya mihadarati yenye thamani kubwa kutoweka kutoka ghala la serikali huko Sewri mwaka 2014.

Polisi sasa wameifunga kesi wakiitaja kama iliyo ya kweli lakini ambayo haijakamata mshukiwa.

Mihadarati iliyoibiwa ni sehemu ya karibu kilo 200 za ketamine, ambazo Kurugenzi ya Intelijensia ya Mapato (DRI) iliikamata huko Andheri Juni 2011.

Katika tukio hilo mfanyabiashara Abhijeet Konduskar wa kampuni ya usafirishaji ya Konduskar Travels alikamatwa akiwa na wenzake kwa biashara ya dawa haramu.

Polisi walikamata jumla ya kilo 1,000 za  ketamine kutoka Mumbai na Sangli.

Polisi hao wa India wanawatuhumu panya hao kuwa ndio wa kulaumiwa baada ya kupata mabegi hayo yalitobolewa kwa chini.

Uchunguzi wa miaka mitatu umekamilika, wakidai kwamba iwapo ingekuwa binadamu wangechukua mabegi yote hayo.

Hii si mara ya kwanza kwa maafisa wa polisi nchini India kuwalaumu panya kwa kutoweka kwa mihadarati iliyokamatwa.

Ingawa panya wanafahamika kwa uhalibifu wa vitu, polisi wa India ni wepesi kujiweka kando na lawama za kutoweka kwa kitu fulani kizembe au kwa makusudi kwa kutupia lawama kwa vitu vingine hata kama ni vya kufikirika.

Weka maoni yako

XHTML: You can use these html tags: <a href="" title=""> <abbr title=""> <acronym title=""> <b> <blockquote cite=""> <cite> <code> <del datetime=""> <em> <i> <q cite=""> <s> <strike> <strong>

YOUTUBE

POLISI WANAPOTUHUMU PANYA KUTOWEKA KWA MIHADARATI