31.7 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

POLISI WAELEZEA KUPUNGUA KWA MATUKIO YA UHALIFU

Na LEONARD MANG’OHA -DAR ES SALAAM

KAMANDA wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa, amesema matukio ya uhalifu kati ya Januari na Novemba mwaka huu yamepungua ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka jana.

Aliyasema hayo jana katika mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam ambapo alisema matukio yaliyoripotiwa katika vituo vya polisi vya kanda hiyo kwa mwaka huu ni 126,200 ikilinganishwa na matukio 129,602 yaliyoripotiwa katika kipindi kama hicho mwaka uliopita.

Alisema idadi hiyo ni sawa na upungufu wa matukio 3,405 ambayo ni sawa na asilimia 2.6 ya matukio yaliyotokea mwaka jana.

“Katika kipindi cha Januari hadi Novemba 2017, kulikua na jumla ya matukio makubwa ya jinai 9,736 ikilinganishwa na matukio 12,550 yaliyoripotiwa katika kipindi kama hicho 2016 sawa na upungufu wa matukio 2,814 sawa na asilimia 22.4.

“Hali ya uhalifu katika Kanda ya Dar es Salaam ilikuwa ya kuridhisha ingawa kulikuwa na matukio machache ya unyang’anyi wa kutumia silaha, unyang’anyi wa kutumia nguvu, uvunjaji, wizi wa magari na pikipiki,” alisema Mambosasa.

Alisema jumla ya matukio ya unyang’anyi wa kutumia silaha  yaliyotokea mwaka jana ni 127, huku mwaka huu yakiwa ni 59 tu, sawa na upungufu wa matukio 68, unyang’anyi wa kutumia nguvu yalikuwa 757 mwaka jana huku mwaka huu yakishuka na kufikia 328.

“Polisi katika juhudi za kuimarisha usalama wa wananchi, iliimarisha doria na misako mbalimbali sehemu zote za jiji ambapo wahalifu wapatao 18,194  walikamatwa kwa tuhuma mbalimbali.

“Majambazi sugu wapatao 36  walikamatwa kutokana na makosa ya unyang’anyi wa kutumia silaha, nguvu, uvunjaji na wizi wa magari,” alisema Mambosasa.

Alisema katika kipindi hicho jumla ya silaha 27 na risasi 1,147 zilikamatwa,  kati ya hizo SMG 2 na risasi zake 324, bastola 15 na risasi 127, Shortgun 6 na risasi 394 na riffle 4 na risasi 263 na watuhumiwa 25 walikamatwa.

Alisema dawa za kulevya aina ya cocaine yenye uzito wa kilogramu moja na gramu 444, heroine kilogramu 2  na gramu 234, vilikamatwa huku jumla ya watuhumiwa 352 wakitiwa nguvuni.

Pia Mambosasa alisema jumla ya noti bandia 102 zenye thamani ya Sh 53,794,000 zilikamatwa na watuhumiwa 1,124 walitiwa nguvuni.

Wahamiaji haramu waliokamatwa ni 193 ambapo jumla ya kesi 109 zilifunguliwa kwa makosa ya kuingia nchini na kuishi bila kibali kwa raia hao wa nchi za  Kenya, Malawi, Uganda, India, Nigeria, Ethiopia na Somalia.

Wakati huo huo, Mambosasa amepiga marufuku wakazi wa jiji hilo kusherehekea mkesha wa mwaka mpya kwa kuwasha matairi na fataki kwani kufanya hivyo ni kuvunja sheria.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles