30.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

POLISI MWANZA DHIBITINI UUZWAJI, UVUTAJI BANGI VIJIWENI

Na BENJAMIN MASESE-MWANZA

SINA uthibitisho lakini naweza kusema kuna hali ya ubia ama ushirikiano kati ya wauzaji, wasafirishaji wa dawa za kulevya na polisi.

Nisema hakuna ubia wala ushirikiano, je kwanini vitendo vya utumiaji na uuzwaji wa bangi katika maeneo mbalimbali ya jiji la Mwanza havikomi na vinafanyika wazi wazi?

Kama haitoshi, wauza bangi hizo wanajulikana kwa kila kijiwe sanjari na wakala wa usambazaji, je jamii ielewe kwamba mapambano ya kudhibiti madawa ya kulevya yamewashinda polisi? Najua polisi mtakimbilia kusema mnahitaji ushirikiano na wananchi wa eneo husika, shida ni usalama wa mtoa taarifa kwani hakuna uhakika wa uaminifu au ulinzi wake ingawa si kwa wote.

Ndani ya Jiji la Mwanza polisi wanatambua wazi moja ya kata ambayo hadi sasa ina mazingira rafiki kwa wahalifu ni Kishili, isitoshe matukio makubwa yameshatokea huko na hata baadhi ya vikao na mikutano ya hadhara polisi wamekuwa wakiitolea mfano.

Katika suala la uhalifu tunawapongeza polisi Mwanza, kwani hivi sasa hali imetulia kabisa ambapo watu wanafanya shughuli zao bila hofu tofauti na awali ilivyokuwa ikifika saa 12 jioni wafanyabiashara wanafunga maduka yao.

Hakika Mkuu wa Kituo cha Nyakato, Almachius Muchunguzi chini ya Kamanda wa Polisi Mwanza, Ahmed Msangi wamefanikiwa kwa asilimia 90 kuwadhibiti wahalifu, hii inatokana na dhamira yao ya wazi na ushirikiano kwa wananchi pale wanapopiga simu, huzipokea haraka na kuzifanyia kazi tofauti na watangulizi wao.

Mkakati walioweka kuthibiti uhalifu na kuwatambua wahalifu unapaswa kuwa endelevu kwani kata hiyo ni moja ya maeneo yanayokuwa kwa kasi huku kukiwa na ongezeko kubwa la watu wa aina mbalimbali, lakini kubwa linaloliliwa hivi sasa ni namna ya vijana wanavyovuta bangi, je polisi wameshindwa kudhibiti vile vijiwe?

Kuna taarifa za chini chini kuwa ndani ya kata hiyo zinadai kuwa eti wakala wa dawa hizo ni ‘kigogo’ mstaafu hivyo ni vigumu polisi kumkamata, kama ni kweli ni ajabu kabisa.

Lakini tukumbuke katika utawala wa awamu ya tano umekuwa ukijitanabaisha kuwa hauangalii kigogo wala mwenye ukwasi wa pesa.

Itakumbukwa aliyewahi kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Magessa Mulongo kabla ya John Mongella wa sasa, akiwa katika ziara aliwahi kupita ndani ya kata hiyo na alipofika senta watu wote waliokuwa katika msafara huo walianza kutazama kwa sababu ya harufu ya bangi.

Kutokana na hali hiyo siku iliyofuata polisi walifanya msako wa kuwakamata watumiaji kitendo kilichofanya kijiwe kuhamishwa kutoka mbele ya barabara na kujisogeza nyuma kidogo, haitoshi wapo baadhi ya wananchi waliojitolea kuwaonyesha polisi kijiwe kilipohamishiwa.

Ni kweli msako wa kushtukiza uliendelea ingawa haukuweza kuwadhibiti ilivyo wauzaji na watumiaji kwani vijana wengi wa kata hiyo wanajishughulisha na kazi ya kupasua mawe, kuchimba mchanga, kupiga debe na kufyatua matofali, hivyo wanadai kwamba bila dawa hizo, shughuli zao haziwezi kufanyika vizuri.

Si kwamba vitendo hivyo vinafanyika ndani ya kata ya Kishili pekee la hasha, bali kata nyingi ndani ya jiji la Mwanza. Ni wakati muafaka wa polisi kufanya msako ama ukaguzi katika vibanda vyote vilivyo mbele ya barabara kwani wapo wengine wanajifanya wanauza soda, pipi, sigara ama kufanya miamala ya fedha kama M-Pesa au Tigopesa, lakini kumbe ndio wauzaji wa bangi.

Mbali ya vibanda hivyo, kuna haja ya polisi kwa kutumia mbwa wao wa kunusa dawa hizo kufanya upekuzi wa baadhi ya nyumba watakazoweza kuhisia ili kubaini uwezo wa dawa hizo kwani inadaiwa nyingi zinahifadhiwa katika majumba ya watu na kutoa kidogo kidogo kwa wauzaji.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles