29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

Polisi lawamani kesi za mimba

Mwandishi Wetu -Maswa

JESHI la Polisi wilayani Maswa mkoani Simiyu, limelalamikiwa kuwafumbia macho watuhumiwa wanaowapa mimba wanafunzi na kuharibu kesi zinazotolewa taarifa katika vituo vya polisi.

Malalamiko hayo yametolewa juzi kwa waandishi wa habari na baadhi ya wananchi waliokuwa nje ya viwanja vya Mahakama ya Wilaya ya Maswa waliokuwa wakifuatilia kesi za wanafunzi kupatiwa ujauzito.

Akitoa malalamiko hayo, mkazi wa Kijiji cha Mpindo, Shigela Golani, alisema licha ya Serikali kupambana na watu wanaowapatia ujauzito wanafunzi wa shule, lakini jitihada zimekuwa zikivunjwa nguvu na askari wa kituo cha polisi cha wilaya hiyo.

“Serikali Wilaya ya Maswa imekuwa ikipambana na watu wanaowapatia mimba wanafunzi, cha kushangaza Kituo cha Polisi Wilaya ya Maswa ukipeleka kesi ya mimba, wamekuwa kikwazo kwa kuharibu ushahidi, hata zikienda mahakamani zinakosa nguvu,” alisema.

Alisema kutokana na mazingira hayo, inawakatisha tamaa wananchi, hasa wazazi na walezi wa watoto wanaopatiwa ujauzito na kuondoa imani kwa jeshi hilo.

“Ni vizuri mkuu wa kituo cha polisi wilaya ya Maswa afuatilie malalamiko haya na kukisafisha kituo hiki, maana wananchi tunakosa imani na askari wanaoshughulikia kesi za mimba za wanafunzi, wamegeuza mtaji na waathirika kutopatiwa haki,” alisema.

Alisema vitendo hivyo vinaashiria kuwapo vitendo vya rushwa na kuiomba Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kuingilia kati kesi hizo ili haki ipatikane kwa walalamikaji na washtakiwa wakapata adhabu stahiki.

Ofisa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Wilaya ya Maswa (OC-CID), Mratibu Msaidizi wa Polisi (ASP) Mily Mathias, alisema kesi zote za mimba za wanafunzi zinashughulikiwa na Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai ambayo anayoiongoza, na kusisitiza kuwa wamekuwa wakizipeleka mahakamani.

“Kesi zote za mimba zinashughulikiwa na mkuu wa upelelezi wa makosa ya jinai na si mkuu wa kituo, niwahakikishie mimi ndiye mkuu wa

idara ya upelelezi, tunajitahidi kuzipeleka mahakamani kwa haraka zaidi, iwapo yupo askari anaharibu kesi zinazoripotiwa, naomba mlalamikaji aje tuwasiliane,” alisema.

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Maswa, Fredrick Lukuna, alisema kumekuwa na kasumba iliyojengeka miongoni mwa wazazi na walezi ya kuripoti matukio ya mimba kwa watoto wao katika vituo vya polisi, lakini mashauri yanapofikishwa mahakamani wamekuwa wakikacha kufika kutoa ushahidi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles