27.5 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

POLISI: ALIYETAKA KUNUNUA MAHEKALU YA LUGUMI HAFANANI HATA NA SH MIL MOJA

  • Sasa wapanga kumfikisha mahakamani

 

Na AZIZA MASOUD- DAR ES SALAAM

JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, limesema mnunuzi aliyejitokeza kununua nyumba tatu zenye thamani ya Sh bilioni 2.3 zinazomilikiwa na mfanyabiashara maarufu, Said Lugumi, Dk. Louis Shika (48), hafanani hata na Sh milioni moja.

Kauli hiyo ilitolewa jana na Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa, baada ya Dk. Shika kufikishwa katika Kituo Kikuu cha Polisi juzi kwa kushindwa kulipia asilimia 25 ya fedha za manunuzi ya nyumba hizo ambazo ni sawa na Sh milioni 800 na Kampuni ya Udalali ya Yono ambayo ilikuwa ikisimamia mnada huo kwa amri ya Mamlaka ya Mapato nchini (TRA).

Kwa mujibu wa Mambosasa, Dk. Shika ambaye anatuhumiwa kuvuruga mnada wa nyumba hizo tatu ambazo mbili zipo  eneo la Mbweni JKT na nyingine Upanga, bado anaendelea kushikiliwa na jeshi hilo kwa ajili ya upelelezi zaidi baada ya kufikishwa kituoni hapo juzi saa 12 jioni na Mkurugenzi wa Kampuni ya Yono, Stanley Kevela.

“Huyo Dk. Louis Shika, nadhani mtakuwa mmemwona kwenye magazeti leo (jana), amevaa kienyeji na sandozi za ndala, kila mnada alikuwa anashinda na alikuwa anaahidi kulipa mamilioni  japokuwa ukimwangalia huyo bwana hafanani hata na shilingi milioni moja.

“Alikuwa anavuruga mnada tunaweza kusema ni tapeli, katika nyumba zote alikuwa akijitokeza na kutaja fedha kubwa hadi watu waliofika kwa nia ya kununua aliwashinda wakati hakuwa na fedha, lengo lake kubwa lilikuwa ni kuhakikisha zile nyumba hazinunuliwi,” alisema Mambosasa.

Alisema alipokuwa akiahidi fedha hizo waendesha mnada waliona wamefanikiwa kwa kuuza nyumba zote, lakini baada ya kumtaka kulipia kiasi kidogo kama ilivyoelekezwa alidai fedha zake zipo nchini Urusi hivyo wanapaswa kusubiri mpaka zitakapofika.

Alisema uchunguzi wa Jeshi la Polisi walioufanya tangu walipomshikilia  umeonyesha kuwa Dk. Shika ambaye anadai kuishi eneo la Tabata, Dar es Salaam, hana kiasi hicho cha fedha anazopaswa kulipa.

“Hatuna uhakika lakini huyu mtu atakuwa amepangwa na mwenye nyumba kuvuruga biashara hii, katika akili ya kawaida ukijaribu kumfikiria mtu huyu kwanini afanye hivi na ukiangalia nani anapoteza hapa utakuta mwenye nyumba ndiye mwenye nafasi ya kufanya haya yote yaliyotokea,” alisema Mambosasa.

Alisema Jeshi la Polisi bado linaendelea na uchunguzi kuhusu suala hilo ili waweze kumjua mtu aliye nyuma ya  mtuhumiwa huyo kabla ya kufikishwa mahakamani.

Akizungumzia suala hilo Mkurugenzi Mkuu wa Yono, Scolastica Kevela, alisema tukio hilo limemshangaza kwa kuwa ni mara ya kwanza kutokea tangu waanze kufanya minada.

“Tangu tuanze kufanya minada hatujawahi kukutana na tapeli kama huyu pamoja na kwamba hakuwa na fedha lakini aliahidi kununua zile nyumba kwa ujasiri,” alisema Kevela.

Alisema baada ya mtuhumiwa huyo kudai kuwa anasubiri fedha kutoka nchi za Urusi na Canada, ndipo walipoamua kumpeleka kituo cha polisi.

“Amepelekwa kituoni kwa sababu mbili kwanza katuharibia mnada, kulikuwa na watu pale walitaka kununua akawazuia lakini pili alitoa ahadi ya kulipa fedha hizo ndani ya saa 48, atakuwa ameenda kinyume na masharti ambayo tuliyaweka wazi hivyo tumemshtaki,” alisema Kevela.

Kevela alipoulizwa kama mtu huyo endapo atapata fedha ndani ya saa alizozitaja anaweza kukabidhiwa nyumba hizo alisema haitawezekana kwa kuwa atakuwa nje ya masharti labda kama atafanya makubaliano maalumu na TRA.

“Masharti ya mnada wetu ulikuwa ni kulipa hiyo asilimia 25 baada tu ya kumalizika mnada, ndiyo maana katika matangazo tulikuwa tunaelekeza mtu kuja na fedha akiwa na ulinzi ama kuhakikisha anaambatana na maofisa wa TRA na Yono hadi benki kwa ajili ya malipo hayo baada ya mnada,” alisema Kevela.

Akimzungumzia mnunuzi huyo ambaye kwa mara ya kwanza alimwona juzi, Kevela alisema wakati wakifanya mnada huo hawakuwa na wasiwasi na mwonekano wa mnunuzi huyo kwa sababu alikuwa kawaida kama walivyokuwa wanunuzi wengine.

“Huyu mnunuzi hatujawahi kumwona, ndiyo mara ya kwanza, lakini pia mwonekano wake haukutushangaza kwa kuwa tulimwona ni mtu mwenye akili timamu,” alisema Kevela.

Alipoulizwa kama anadhani mnunuzi huyo atakuwa ametumwa na mmiliki wa nyumba na sheria inasemaje endapo mwenye nyumba atataka kuzinunua mwenyewe alisema:

“Bado sijajua kama mnunuzi huyo anahusika moja kwa moja, hiyo ni kazi ya polisi, lakini pia sheria haimruhusu mmiliki kununua mwenyewe nyumba zake, haiwezekani,” alisema Kevela.

Kevela alisema mnada huo utarudiwa tena katika tarehe itakayopangwa na yeyote atakayehusika kuharibu mnada huo atachukuliwa hatua kali za kisheria.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles