23.7 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Polepole: tuna kadi milioni mbili za wanachama wapya

Mwandishi Wetu, Dar es Salaam



Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimesema kina kadi zaidi ya milioni mbili kwa ajili ya wanachama wapya wanaotaka kujiunga na chama ambapo kwa Dar es Salaam pekee tayari kadi zaidi ya 13, 000 ziko Makao Makuu ya chama hicho zikisubiri wanachama hao.

Katibu wa Itikadi na Uenezi, Humphrey Polepole, amesema hayo jana Temeke jijini Dar es Salaam, katika mkutano mkuu wa CCM wilayani humo ambapo pia walipokea wanachama wapya zaidi ya 20 ambao ni viongozi kutoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), ACT-Wazalendo na Chama cha Wananchi (Cuf).

Katika wanachama hao, wako wenyeviti wa Wilaya na Kata katika za Kurasini, Chang’ombe, Toangoma na Mtoni na Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake wa ACT-Wazlendo.

“Kuna wanachama mamilioni walioomba kujiunga na CCM na ndiyo maana tumeamua kuchapa kadi zaidi ya milioni mbili, kwa sababu watu watajiuliza wanaohamia CCM ni viongozi tu hawa tunaowaona, mimi nataka niwaambie viongozi hao mnaowaona na wengine ni wachache mno ukilinganisha na idadi ya wanachama wanaojiunga na sisi ndiyo maana nasema kuna kadi milioni mbili.

“Lakini tunajivunia mageuzi ya kiuongozi unaokwenda na mahitaji ya sasa ambao umejikita katika misingi ambayo chama kilianzisha, aina hii ya viongozi ni lazima wawe wanyenyekevu wanaochukizwa na rushwa na mambo ya ovyo na waaminifu, wanaoheshimu wanachama, mfano bora wa kuigwa,” amesema Polepole.

Alisema mageuzi mengine ni ya muundo wa chama ambapo mwanzo kulikuwa na Mkutano Mkuu mkubwa ambapo walitazama tija na sasa wana mkutano ambao wanaweza kukakaa kujadiliana.

“Mwanzo ulikuwa mkubwa sana watu 388 mkikaa mule ndani hadi muelewane vizuri wakati mwingine mtihani, tumerudi kwenye misingi sasa tuna wajumbe 167 wakikaa wajumbe wanatazamana macho kwa macho bila haya wala soni wanaelezana mambo ya kuleta tija ndani ya chama.

“Na mageuzi mengine ni ya kiutendaji sasa hivi tunahakikisha mali za CCM zinatumika kwa maslahi ya chama na si mtu mwingine, sasa hivi fedha ikikusanywa inapelekwa benki tofauti na zamani inaingia mfukoni mwa mtu anaitunza kwa moyo mwema sasa fedha huwa haitunzwi kwa moyo mwema inatunzwa benki.

“Mageuzi haya ni machungu kwa watu ambao hawapendi kufuata utaratibu lakini ni matamu kwa wanachama wanaopenda kuona chama chao kinakua siku hadi siku,” amesema.

Akizungumza baada ya kukaribishwa CCM, aliyekuwa Katibu Mwenezi wa ACT-Wazalendo, Steven Shekumkaye, amesema kuna taarifa zinasema wamenunuliwa jambo alilokanusha.

“Vyama vyetu vya upinzania vikiishiwa hoja vinasema CCM inanunua watu, hiyo CCM ina mfuko gani hadi inunue watu kiasi hicho.

“Nasema sijanunuliwa mimi, nilitafakari nikamuuliza Mungu CCM nilitoka mika 55 iliyopita nitarudije juzi nikaiskia sauti ya Mungu ikaniambia mwaka 1956 huko Chato amezaliwa mtoto mwanamume anaitwa Magufuli, Shekumkaye nenda CCM kumenoga, nikafunga safari kwenda kwa Katibu wa CCM nalia, akaniambia usilie umerudi nyumbani, karibu,” amesema.

Kwa upande wake aliyekuwa Diwani wa Kata ya Mtoni na Mweneyekiti wa Chadema Wilaya ya Temeke, Bernard Mwakyembe, amesema ameshika nafasi nyingi Chadema pamoja na kusaidia kupata wenyeviti wa mtaa ambao awali hawakuwapo lakini sasa imetosha amerudi nyumbani.

“Hadi Septemba 15, mimi niko bega kwa bega na Mbowe, nikamwambia Mwenyekiti mimi naondoka ninakokwenda sikujui ila utaona kwenye TV.

“Sasa kumekuwa na maneno mengi kwamba Mwakyembe amenunuliwa mara milioni 300, nawaambia Watanzania CCM hainunui watu ila watu tunaangalia ilani ambayo tumeipigania mwaka 2015 kama elimu bure ambayo leo iko mtaani, tulikuwa tunalalamika umeme leo tunaona mabwawa makubwa ya Stigler’s Gorge yanajengwa pale Morogoro, Mamfugale flyover yanajengwa Tazara na sasa Ubungo,” alisema Mwakyembe.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles