23.7 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

POLEPOLE: BADO NAAMINI MUUNDO WA SERIKALI TATU

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Humphrey Polepole, akizungumza na waandishi wa habari wakati akikabidhiwa ofi si na mtangulizi wake Nape Nnauye (kulia), Dar es Salaam jana.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Humphrey Polepole, akizungumza na waandishi wa habari wakati akikabidhiwa ofi si na mtangulizi wake
Nape Nnauye (kulia), Dar es Salaam jana.

Na waandishi wetu – dar es salaam

KATIBU wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Humphrey Polepole, amesema hawezi kupindisha maneno kuhusu msimamo wake wa muundo wa Serikali tatu.

Polepole alikuwa mmoja wa wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba chini ya Mwenyekiti wake, Waziri Mkuu mstaafu, Joseph Warioba, ambao pamoja na mambo mengine, waliridhia uwapo wa muundo wa Serikali tatu ambazo ni Serikali ya Muungano, Tanganyika na Zanzibar.

Akizungumza baada ya kukabidhiwa ofisi na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye, katika ofisi ndogo za CCM zilizopo Lumumba, Dar es Salaam jana, Polepole alisema ataendelea kusimamia hoja yake.

“Siwezi kupindisha maneno yangu kuhusu muundo wa Serikali tatu katika Katiba mpya, nitaendelea na kusimamia hoja yangu kama nilivyokuwa mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.

“Kama kuna watu wanataka kubadilisha hoja ya CCM katika kipindi hiki ambacho kinasimamia kuleta maendeleo kwa wananchi, hawatafanikiwa.

“Tutaendelea kuwatumikia wananchi kama ilivyokuwa kwenye ilani ya CCM wakati chama hiki kinaanzishwa, muda wa siasa za madaraka umekwisha baada ya kumalizika uchaguzi mkuu mwaka jana,” alisema Polepole.

Alisema pamoja na kuwapo mabadiliko ya wajumbe wa Kamati Kuu yaliyotangazwa hivi karibuni na Rais Dk. John Magufuli, CCM itaendelea na misimamo yake kama ilivyokuwa kwenye misingi ya uanzishwaji wake.

“Kuanzia sasa, CCM itarudi katika misingi yake, ikiwa ni pamoja na kuwatumikia wananchi bila ya kujali tofauti zao za kisiasa, dini wala rangi,” alisema.

Kuhusu nafasi yake ya ukuu wa wilaya, Polepole alisema hadi sasa hajapewa barua ya kutenguliwa nafasi hiyo.

Polepole alisema kuwa alimuomba Rais Magufuli kumpa mwezi mmoja ili aweze kumaliza kero za wananchi wa Wilaya ya Ubungo, kwa sababu wana migogoro mingi, ikiwamo ya ardhi.

Alisema anatamani kumaliza kero hizo ili aweze kuondoka bila ya kuwa na deni, jambo ambalo linaweza kumpa sifa Rais Magufuli na Serikali yake kuliko akiondoka sasa hivi wakati wananchi bado wana malalamiko.

 NAPE

Naye Nape aliwashukuru Mwenyekiti mstaafu wa chama hicho, Jakaya Kikwete na Katibu Mkuu, Abdulrahman Kinana kwa kumlea, kumwongoza na kumfundisha kazi, kwa sababu bila wao asingeweza kufika halipo sasa.

“Licha ya kuwapo kwa changamoto mbalimbali ndani ya chama, lakini viongozi hawa wakuu waliweza kunilea vizuri, kuniongoza na kunisaidia hadi hapa nilipofika, nawashukuru sana, kwa sababu chini ya mikono yao nimeweza kujifunza mambo mengi ambayo yataendelea kunisaidia niendako,” alisema Nape.

Aliviomba msamaha vyama vya upinzani kutokana na migongano ya kisiasa iliyokuwa inajitokeza, jambo ambalo lilichangia kutoleana maneno ya hapa na pale lakini lengo likiwa ni kuhakikisha Watanzania wanapata viongozi bora kwa maendeleo yao.

“Nita-miss nguo za CCM, lakini sitaki-miss chama, kwa sababu mimi ni mwana CCM, nimeteuliwa ili kuwatumikia wananchi, hivyo basi nitaendelea kutimiza majukumu yangu kama waziri ili kuhakikisha kuwa Watanzania wanapata maendeleo,” alisema Nape.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles