30.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Poleni wana-Ukara, ubani wenu mtaukuta kwenye Kituo cha Afya Bwisya

Na ANDREW MSECHU

MAOMBOLEZO yamemalizika, wana-Ukara katika Wilaya ya Ukerewe waliopoteza ndugu zao wanajaribu kurejea katika maisha ya kawaida, wakibaki na kumbukumbu ya mema na matarajio waliyokuwa nayo kupitia ndugu hao, ambayo yamepotea.

Kwa wenye desturi ya kuhitimisha matanga baada ya siku 40 wanaendelea kusubiri kutimiza wajibu wao, kuonesha upendo walionao kwa wale waliotangulia mbele ya haki, Mwenyezi Mungu awarehemu.

Binafsi, napenda kutumia fursa hii kutoa pole kwa wote waliopoteza ndugu zao. Wamepata maumivu, wamepoteza ndugu zao wa karibu, wamepoteza wapendwa wao, wamepoteza wazazi. Mwenyezi Mungu awalaze mahala pema wanapostahili, wote waliotangulia mbele ya haki.

Wakati mwingine, kutokana na ukubwa wa ajali hiyo iliyosababisha vifo vya zaidi ya watu 225 kupitia ajali ya Kivuko cha MV Nyerere iliyotokea Alhamisi Septemba 20, mwaka huu unaifanya kuwa janga la Taifa.

Hii ni katika hali ya kujaribu kubebeana mizigo, ila kwa ukweli mzigo wa maumivu hasa yanayotokana na vifo na msiba huo yanakwenda moja kwa moja kwa familia zilizopoteza ndugu zao na kuguswa moja kwa moja na janga hilo, ambao ndio waliobeba miili ya wapendwa wao na kutafuta mahala pa kuihifadhi.

Kwa asiyewahi kupata msiba unaomuhusu moja kwa moja, wa aidha mzazi, ndugu, mke, mume au mpendwa wa karibu anaweza asijue hali halisi wanayopitia wale walioachwa katika janga hili, kwa waliowahi kuguswa moja kwa moja wanaweza kuwa na ushuhuda ndani yao.

Vilio katika msiba huu vinatofautiana. Maumivu yanatofautiana. Wapo waliopoteza tu upendo wa wale wa karibu yao kwa kuwa tayari walishamaliza majukumu yao ya muhimu na wamewaacha wakiwa tayari wanaendesha maisha yao.

Msiba mzito zaidi ni kwa wale ambao wamepotelewa na wazazi, walezi, ndugu  wakiwa bado ni tegemezi, wakitegemea mkate wa kila siku, ada za shule, mavazi na malazi kwa wale waliofariki dunia kupitia ajali hiyo, ambayo kimsingi ni kifo cha lazima kilichosababishwa na uzembe wa watu wachache.

Kwa waliofariki dunia, si haki yao kufa kwa wakati huu kwa namna iliyotumika kuwaondolea uhai, kwa kuwa kama wangepata fursa ya kuulizwa wangeeleza wazi kupigania uhai wao kwa ajili ya kutimiza ndoto za wale wanaowategemea.

Pamoja na hayo, Serikali imesimamia upatikanaji wa fedha kwa ajili ya rambirambi, kwa mujibu wa gazeti hili, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwele alisema zinafikia zaidi ya Sh. milioni 949.6 ambazo baada ya kutoa malipo wanayoyaona muhimu, Sh. milioni 689.99 zinazobaki zimetakiwa kutumika kujenga majengo matatu ya Kituo cha Afya cha Bwisya, kilichopo Ukara wilayani Ukerewe.

Inawezekana rambirambi iliyochangishwa na Serikali si haki ya wafiwa, hasa kwa kuzingatia kuwa iwapo kila mmoja angefariki kwa wakati wake na kwa sababu za kawaida wangeweza kuchangiwa na ndugu na marafiki wachache na kuhitimisha msiba wao kwa amani, wakijua kuwa tayari yameshawakuta na hakuna msaidizi.

Kwa Serikali pia, iwapo vifo vya Watanznaia hao vingekuwa ni mtaji wa kuiwezesha kutimiza majukumu yake ya kijamii si haki yake kuitisha michango ya rambirambi kwa kutumia kisingizio cha ajali hiyo kwa kuwa kupitia Mfuko wa Maafa chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, unatakiwa kuwa na fungu la dharura ambalo linatakiwa liwepo wakati wote, kwa ajili ya kukabiliana na maafa ya namna hiyo.

Kwa Serikali, ni aibu kuitisha mchango wa rambirambi kwa kuzibana kampuni na mashirika kwa kisingizio cha kuwasaidia waathirika, ambao kimsingi ni wale waliobaki hai wakiwamo wanafamilia, ndugu na jamaa kisha kutumia fedha hizo si kuwapoza wafiwa, bali kutimiza jukumu lake la msingi la ujenzi wa zahanati, linalotakiwa kutekelezwa kupitia mapato ya kodi zinazokusanywa kila siku.

Serikali inawajibika kutumia fedha zake za dharura kwa kuzipitisha kwenye Bajeti, si za kukusanya rambirambi kwa kuwa tukio hilo linatokana na uzembe wa watendaji wake, ambao kimsingi ndio chanzo cha maafa hayo.

Ikumbukwe haya si maafa yatokanayo na tukio la asili kama ilivyo vimbunga au matetemeko ya ardhi, ambayo unaweza kutumia visingizio hafifu kuwanyima watu misaada na rambirambi.

Japokuwa tayari imeshakuwa, maagizo kutoka mamlaka ya juu kabisa yameshatolewa na kinachofuata ni utekelezaji, ni upofu wa fikra na dhambi isiyosameheka kukaa kimya katika mambo ambayo hayastahili kukaliwa kimya, japokuwa ninaamini kuwa Serikali si taasisi ya bima kwamba itawalipa fidia waathirika wote wa tukio hilo.

Ni kwa uzembe wa waendeshaji wa chombo ambao wako chini ya Serikali, maisha ya wazazi, ndugu na jamaa ambao walikuwa wakilea na kutunza familia zao wamepotea.

Walioondoka wamekatishwa jukumu lao la kutunza na kulea wategemezi wao, wategemezi waliobaki wamebaki wakiwa hawajui nini kitaendelea katika maisha yao, kwa watoto na vijana waliopo shule na vyuo, hawajui maisha yao yataendeleaje, kwa wazee wasiojiweza waliokuwa wakiwategemea, hawajui hatima yao iko wapi.

Rambirambi hizo zinatakiwa iwe chanzo cha kuwajengea maisha mapya wale waliobaki, ambao sasa wanaanza maisha mapya, wakiwa hawajui watakapopata mlo wao wa kila siku, wakiwa hawajui watakapopata ada, wakiwa hawajui watakapopata huduma nyingine za malezi.

Nimejaribu kujiuliza mara kadhaa bila kupata majibu ya moja kwa moja, nini maana ya rambirambi? Kwa mujibu wa kamusi iishiyo ya Kiswahili ya Oxford, rambirambi ni salamu za kuonesha masikitiko kwa maafa yaliyomfika mtu na Kamusi Teule ya Kiswahili: Kilele cha Lugha inaeleza kuwa rambirambi ni ujumbe wa majozi kwa maafa yaliyomfika mtu.

Nikajiuliza tena, iwapo rambirambi zinatumika kujenga kituo cha afya, Je ndiyo salamu za majonzi kwa waliofikwa na maafa? Na hapa, kodi za wananchi wanazolipa kupitia michango mbalimbali kwa ajili ya kuiwezesha Serikali kutimiza majukumu yake hasa huduma za jamii zina maana gani, au zinafanya kazi gani kwa sasa?

Iwapo chombo kilichosababisha vifo vya mamia haya ya Watanzania kinamilikiwa na Serikali, Watanzania wamepoteza maisha, wameacha yatima, wameacha wategemezi ambao kwa sasa hawana msaada waliokuwa wakiupata moja kwa moja, Serikali inawajibika vipi kwa kundi hili la hawa waliobaki, walioathiriwa na ajali hiyo?

Ninawafikiria zaidi watoto walioachwa na wazazi wao,hasa kwa namna watakavyoendelezwa kielimu, watakavyopatiwa huduma nyingine zote za kijamii zinazohitaji malipo, ninapata jibu kwamba zaidi ya kufikiria kutumia fedha hizo kukarabati zahanati, kuna sehemu zenye matumizi mazuri zaidi ya fedha hizo.

Ninajaribu kuangalia iwapo waliofariki dunia wameacha pengo kwa nani, ninabaini kwamba pengo lililobaki ni kwa familia zao, kwa Serikali hakuna pengo, ni suala la kufa kufaana, rambirambi ambayo labda ingeweza kusaidia kuwanasua watoto walioachwa yatima au kuachwa na mzazi mmoja kusaidiwa kuendelezwa, inakuwa ni ahueni kwa Serikali kuisaidia kutimiza majukumu yake ya msingi ambayo labda kutokana na ufinyu wa kodi na Bajeti, vifo hivyo vimeleta ahueni.

Inaweza kuwa mchezo wa ‘bora wafe wengine’, tupate rambirambi za kutosha, tutekeleze majukumu mengine katika maeneo ambayo Bajeti ya Serikali inayotokana na kodi na vyanzo vingine rasmi imeshindwa kuyafikia kwa wakati, ilitokea kwa maafa ya tetemeko la ardhi Bukoba, sasa kwa maafa ya ajali ya MV Nyerere huko katika Kisiwa cha Ukara.

Ninabaini kwamba kwa mujibu wa sheria namba 7/2015 inayoanzisha Mfuko wa Maafa chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, vyanzo vya mapato kwa mujibu wa kifungu cha 31(b) na (f) ni pamoja na fedha za rambirambi kutoka maeneo mbalimbali.

Kwa maana hiyo, fedha znazotokana na vyanzo vyote katika mfuko huo wa maafa ndizo zinazotakiwa kutumika, kwa mujibu wa tukio hili la ajali ya MV Nyerere, kujenga mnara wa kumbukumbu, kutoa pole kwa walioathiriwa na tukio hilo pamoja na wafiwa na kulipia posho za waopoaji.

Katika hayo, hayo maelekezo yako wazi katika kifungu cha nane cha sheria ya maafa namba 7/2015, kwamba fedha zote zinazotolewa kwa ajili ya maafa ni kwa ajili ya maafa, lakini jambo lililofanywa tofauti ni uamuzi wa kutumia fedha hizo za rambirambi kujenga kituo cha afya, ambacho kimsingi Serikali inawajibika kuhakikisha inatumia fedha zake kutoka katika vyanzo vingine vya kodi au vya mapato kutekeleza jukumu hilo.

Ninaona ipo haja ya kufanya tofauti, tofauti yenye tija na kujali utu, tofauti yenye kuonesha kuwajibika kwa watu wanaoathiriwa na maafa ya aina hii, ambayo moja kwa moja watendaji wa Serikali au vyombo vyake wanahusika kuyasababisha na kugharimu uhai wa Watanzania.

Nikiwa na mamlaka ya juu katika nchi, nitafanya tofauti katika maamuzi ya aina hii, nitahakikisha kwamba pamoja na kusimamia kuchukuliwa hatua za kisheria kwa wote wanaohusika na kusababisha maafa yanayogharimu uhai wa Watanzania na mali, za wananchi na za Serikali, ninabaini waathirika wa moja kwa moja wa maafa hayo.

Nitafanya tofauti, nitahakikisha watoto wote waliobaki yatima walio katika umri wa utegemezi, rambirambi inayotokana na vifo vya wasimamizi wao inatumika kuhakikisha wanapata elimu hadi ukomo wao.

Hakika, nitafanya tofauti, kwa kuhakikisha kwamba pamoja na kujenga kumbukumbu ya tukio hilo ambayo si jambo jema sana, ninawajengea waathirika wote kumbukumbu mioyoni mwao kwamba katika madhila waliyoyapata, Serikali imetumia rambirambi kuwafuta machozi, kwa kuwapa mkono wa pole utakaowawezesha ‘wale waliofikwa na maafa’ kuanza maisha mapya, kwa kutambua kwamba Serikali inawajibika kwa kufidia uzembe wa watendaji wake wazembe.

Nitafanya tofauti kwa kuhakikisha kwamba iwapo kuna uhitaji wa haraka wa ujenzi wa vituo kwa ajili ya huduma za jamii, natumia uwezo na fursa niliyonayo kuagiza fedha kutoka katika vyanzo kedekede, ambavyo vingine naweza kuvibuni papo hapo bila kugusa rambirambi za waathirika wa maafa.

Nitafanya tofauti kwa kuhakikisha kwamba familia zote zilizoguswa moja kwa moja na msiba huo zinafutwa machozi kwa kupewa ahueni ya itakayowapa kumbukumbu ya namna Serikali ilivyoguswa na namna uzembe wa watendaji wake ulivyowasababishia maumivu na kadhia kwa kusababisha kuondokewa na wapendwa wao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles