30.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Pluijm aelekeza mitutu Msimbazi

hans-pluijmNA ABDUCADO EMMANUEL, DAR ES SALAAM

KOCHA Mkuu wa timu ya Yanga, Hans van Pluijm, amesema haofii lolote kuelekea mechi dhidi ya hasimu wake, Simba Jumamosi hii kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam huku akitamba yupo tayari kwa vita ya kuwachakaza wekundu hao.

Msimu huu pambano hilo limetabiriwa kuwa litakuwa ni la kukata na shoka kutokana na timu hizo kupata matokeo ya ushindi kwenye mechi za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) walizocheza mpaka sasa.

Yanga iliyo kileleni mwa Ligi Kuu kwa pointi tisa sawa na Simba, Azam na Mtibwa Sugar zinazofuatia imeshinda mechi zake zote dhidi ya Coastal Union (2-0), Tanzania Prisons (3-0) na juzi ikailaza JKT Ruvu 4-1 zote ikicheza Uwanja wa Taifa.

Pluijm aliliambia MTANZANIA kuwa anauchukulia kawaida mchezo huo na hata maandalizi yake atakayofanya ni sawasawa na yale atakayofanya wakati akicheza na timu nyingine.

“Kwangu mimi ni mechi ya kawaida kama nyingine, lakini huwa na mashabiki wengi zaidi, vile vile ni kama vita kama usipoua, basi utauliwa wewe. Tutafanya maandalizi yetu kawaida kama kwenye mechi nyingine.

“Binafsi naamini ya kuwa tutacheza mpira wetu mzuri kwani timu inapofanikiwa kumiliki mpira, kufanya mambo yote uwanjani kwa kasi na umakini, tutaiweka Simba pabaya na kuipa wakati mgumu kwenye mchezo huo,” alisema.

Mholanzi huyo tokea aanze kuifundisha Yanga, hajawahi kupata ushindi kwenye mechi zote mbili alizocheza dhidi ya Simba, alitoa sare ya bao 1-1 msimu wa 2013-14 kabla ya kufungwa 1-0 msimu uliopita, mara zote hizo alikabidhiwa timu hiyo kwenye mechi za mzunguko wa pili.

Pluijm aligoma kuzungumzia rekodi yake hiyo mbaya dhidi ya Simba akidai kuwa: “Hiyo ni historia na sitaki kuangalia huko, ninachoangalia ni hiki kilichoko mbele yangu. Niweke wazi kuwa siiogopi Simba na hata timu nyingine yoyote, lakini zote naziheshimu.”

Hata hivyo, Pluijm akizungumzia ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya JKT Ruvu alisema bado vijana wake hawajacheza katika kasi anayoihitaji, wamekuwa wakicheza kasi ya chini lakini akadai huo ni mwanzo tu na timu yake imekuwa ikiimarika kadiri siku zinavyosogea.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles