28.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Pinda ashangaa mikoa inayozalisha vyakula vingi kuwa na udumavu

Ramadhan Hassan -Dodoma

WAZIRI Mkuu mstaafu, Mizengo Pinda, ameonyesha kushangazwa na mikoa yenye vyakula vingi kuwa na ugonjwa wa udumavu.

Kutokana na hali hiyo, ameiomba Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, kutoa elimu kuhusu lishe inataka ulaji wa vyakula gani.

Akizungumza jana jijini hapa wakati wa uzinduzi wa ripoti ya matokeo ya lishe nchini ya mwaka 2019, Pinda alisema ni jambo la kushangaza mikoa yenye vyakula vingi kuwa na ugonjwa wa udumavu, huku akitolea mfano wa mikoa ya Katavi na Rukwa.

“Ni jambo la kushangaza kidogo mikoa inayozalisha chakula cha kutosha kama Katavi na Rukwa kuwa na ugonjwa kama ule. Mimi nakataa, lazima tuelimishwe lishe inataka nini.

“Mjadala ulivyofika Rukwa nusura tushikane mashati, nilimpigia simu mkuu wa mkoa na nikamwambia aitishe RCC kwani sisi chakula tunacho kwanini tunaambiwa hivyo, hapa inahitajika elimu tu,” alisema Pinda.

Aidha, alisema vyama vya siasa vina nafasi kubwa ya kukabiliana na ugonjwa wa udumavu kwa wabunge na madiwani kupaza sauti juu ya jambo hilo.

“Hili bila kuweka tofauti zetu, bila kuweka dini zetu, bila kuweka rangi zetu jambo la udumavu tuone ni adui na tuhakikishe anaondoka,” alisema Pinda.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Zainabu Chaula, alisema kuna haja ya kuangalia namna bora ya kutoa elimu kwa Watanzania kuhusu suala la lishe.

Alisema wengi wamekuwa hawajui lishe ni nini, hivyo utafiti huo unatakiwa kutumiwa vizuri ili uwafikie watu wengi na waliopo katika maeneo ya vijijini.

“Lazima tuweke mikakati katika suala la lishe katika mikoa, tuna kazi ya kutembea pamoja katika hili, lazima tuwe na njia nzuri ya kutoa lishe, lakini ni lazima tuangalie aina ya vyakula ambavyo tunavyo,” alisema Dk. Chaula.

Mkurugenzi wa Chakula na Lishe kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Germana Leyna, alisema lengo la kuzindua ripoti hiyo ni kuona Tanzania imefikia wapi katika mpango wa kutatua changamoto ya lishe nchini.

Dk. Leyna alisema walichoangalia katika utafiti huo ni pamoja na hali ya lishe, udumavu, uzito uliopitiliza, afya ya kinamama wakati wa ujauzito na wa kujifungua, hususani siku 1,000  na jinsi ya kuweza kutatua changamoto hizo.

Alisema wamejipanga kusambaza taarifa zaidi katika mikoa mbalimbali lengo likiwa ni Watanzania wajue lishe ni nini.

Hata hivyo, alisema bado kuna changamoto ya ugonjwa wa udumavu katika mikoa 15 nchini.

Kwa upande wake, Ofisa Lishe kutoka Manispaa ya Morogoro, Elina Kweka, alisema changamoto kubwa wanayokutana nayo ni jamii kutokuwa na uelewa wa vyakula vyenye lishe ni vipi. Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Nutrition International, Dk. Daniel Nyagawa, alisema matatizo ya ukosefu wa lishe nchini yamenza kupungua kutoka asilimia 34 mwaka 2016 hadi 32 mwaka jana, huku akitaka jitihada za ziada katika kutatua tatizo hilo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles