30.2 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

PICHA YA ‘SHULE YA UDONGO’ YAMKERA MKURUGENZI, AAGIZA IBOMOLEWE

Na Florence Sanawa

Mtwara

Picha iliyosambaa katika mitandao ya kijamii ikionyesha madarasa ya udongo yaliyoezekwa kwa makuti ya Shule ya Msingi Mitambo iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara, mkoani hapa imesababisha Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya hiyo, Omary Kipanga kuagiza madarasa hayo kubomolewa haraka ili kupisha ujenzi wa madarasa mapya.

Kipanga amesema majengo hayo yalijengwa kwa utashi wa wananchi bila kushirikisha halmashauri hiyo.  

“Kile kilichokuwa kimejengwa si kwa maagizo ya ofisi yangu, mimi nilipita Oktoba mwaka jana na kukagua shule zote lakini sikuona majengo kama yale, kama ni kujenga wamejenga wananchi tena kama si Novemba itakuwa Desemba.

“Hata mwongozo wa Wizara ya Elimu hausemi tujenge darasa kama lile, hata jiko hatukuambiwa tujenge kwa mfano ule hatukuagiziwa yale, hata kama yangekuwa madarasa ya muda yale si madarasa ule ni uchafu ulipo si mahala pake ndiyo maana nimeagiza yabomolewe,” amesema. 

Mkurugenzi huyo amesema ukiangalia vizuri katika eneo la shule kuna misingi imeshaanza kuchimbwa ili kuanza ujenzi wa madarasa mazuri lakini ameshangaa kuona madarasa ya udongo yamejengwa. 

“Tunazo shule 10 zinahitaji ujenzi na ukarabati wa hali ya juu, hivi sasa katika Shule ya Msingi Mitambo tutajenga madarasa matatu ili yawe sita ambapo gharama ya darasa moja ni Sh milioni 20 huku tukitenga Sh milioni 40 kwa ajili ya nyumba za walimu lakini wananchi pia watajenga hivyo kutakuwa na madarasa manne,” amesema Kipanga. 

Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Rashid Chalido amesema baada ya kikao cha wazazi na walimu kilichofanyika mwaka jana mwishoni walikubaliana kujenga madarasa hayo ili kuwanusuru watoto na kero za mvua zinazokuwa zinawakabili.  

“Mwaka jana tulifanya kikao tuliona tatizo ni kubwa na watoto wanaathiriwa na mvua shuleni ndiyo maana tuliamua kujenga nyumba za udongo za muda ili watoto wapate pa kujishikiza lakini tumepata agizo kutoka uongozi wa juu ikitutaka tuvunje nyumba hizo ili kupisha ujenzi wa madarasa manne ambao umeanza,” amesema Chalido.

- Advertisement -

Related Articles

1 COMMENT

  1. Huu ndio ukweli wa mambo haukwepeki. Mpaka leo watoto wanasoma chini ya mti. Na viongozi wamekaa Dodoma kupokea mamilioni kwa mwezi. Kwa vipi? Na tunanunua ndege za bombardia. Je lipi ni muhimu. Mnashindwa kuiweka tume mletewe picha ya kila shule. Mpaka mtoke huko Dodoma mpoteze tena pesa za umma wakati social media nyingi tu. Waambieni kila kijiji wawatumie picha za shule. Within one day zote mnazo. kwa nini mnashindwa kuzitumia social media kuleta maendele vijijini.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles