27.5 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Panya Road 500 mbaroni

Pg 1 kova

Na Waandishi Wetu, Dar es Salaam
JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, limewatia mbaroni vijana 500, maarufu Panya Road ambao wamekuwa wakijihusisha na vitendo vya uhalifu wa kutumia silaha na uporaji.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Suleimani Kova, alisema vijana hao walikamatwa katika operesheni maalumu iliyofanyika katika mikoa mitatu ya kipolisi ya Ilala ambako walikamatwa vijana 104, Temeke (168) na Kinondoni (202).
Alisema operesheni hiyo ilitokana na tukio la Januari 2, mwaka huu katika eneo la Magomeni Kagera ambapo vijana hao walipambana na polisi. Katika tukio hilo vijana 36 walikamatwa.
Alisema vijana wawili walikamatwa baada ya mazishi ya kijana mwenzao aliyefariki kutokana na matukio ya wananchi kujichukulia sheria mkononi Januari mosi, mwaka huu katika eneo la Mwananyamala.
“Uchunguzi uliofanyika umebaini wapo viongozi watatu ambao ni Halfan Nurdini (24), Said Mohamed (22) wakazi wa Tandale Sokoni na Mohamed Nangula (19) mkazi wa Mburahati kwa Jongo.
“Imegundulika kila inapotokea kijana ameuawa, wakati wa mazishi viongozi hao, huwa wanakuwepo na huwachochea wenzao kufanya vurugu kama ilivyotokea Januari 2, mwaka huu,” alisema Kova.
Alisema msako mkali unaendelea katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam na makamanda wa polisi wa mikoa yote ndio wasimamizi wakubwa wa kuwasaka na kuwakamata vijana hao.
Kova alisema kikosi cha askari wa upelelezi na intelijensia wanaendelea na kazi hiyo mtaa kwa mtaa.
Alisema pamoja na msako huo, polisi wana mpango wa kuwashirikisha watendaji kuanzia ngazi ya mtaa, kata na tarafa ili waweze kushirikiana kukabiliana na mtandao wa kihalifu.
“Hivi karibuni itafanyika mikutano au semina kutoa mafunzo kwa watendaji ili kukabiliana na tatizo hili… tunaamini kwa njia hii tutafuta mtandao wote.
“Suala la kukosa kazi kwa vijana lisiwe kisingizio cha kufanya makosa ya jinai, msako unaendelea pamoja na kubaini vyanzo vya uhalifu na kuvunja vijiwe vya wahalifu,” alisema Kamanda Kova.
Alisema vielelezo walivyokamatwa navyo vijana hao ni pamoja na puli za bangi 113, kete 676, misokoto 294, mirungi bunda tatu na gongo lita 150 ambavyo vijana hao hutumia kwa lengo la kuamsha vichocheo vya uhalifu.
Alisema watuhumiwa wote watafikishwa mahakamani upelelezi utakapokamilika na hakuna atakayedhaminiwa katika kituo chochote cha polisi hadi upelelezi utakapokamilika.
Aliwaomba wananchi kushirikiana na polisi kutoa taarifa pale wanapoona kuna dalili ya kufanyika matukio ya kihalifu.
Wiki iliyopita, kundi la vijana hao walivamia mitaa mbalimbali ikiwamo Sinza, Tandale, Kinondoni na Mwananyamala.
Katika mitaa hiyo, vijana hao walikuwa wakipora vitu mbalimbali kwa kila mtu waliyekutana naye mbele yao.
Kabla ya tukio hilo, vijana hao walidai mwenzao Ayub Mohamed ‘Diamond’ aliuawa kwa kuhusishwa na matukio ya uhalifu.
Katika hatua nyingine, mtu mmoja anayehusishwa na kundi la Panya Road, amelazwa katika Taasisi ya Mifupa na Mishipa ya Fahamu (MOI) kutokana na kuvunjika mguu na kuumia maeneo ya kichwani.
Kijana huyo ambaye jina lake halikufahamika mara moja, anayekadiriwa kuwa na umri kati ya miaka 18 na 20, alipelekwa hospitalini hapo Januari 3, mwaka huu saa 6:30 usiku.
Akizungumza na MTANZANIA, Meneja Uhusiano wa MOI, Almas Jumaa, alisema tangu afikishwe hospitalini hapo kijana huyo amekuwa akitamka majina tofauti bila ya kujua jina lake ni nani.
“Amefikishwa hapa akitokea Muhimbili tangu Januari 3, mwaka huu akiwa hana fahamu, tunajaribu kumuuliza jina lake nani mara anasema anaitwa Richard, wakati mwengine anasema anaitwa GoodLuck ingawa hatujui anakaa wapi hadi sasa,” alisema Jumaa.
Alisema kijana huyo alifikishwa hospitalini na polisi, ingawa hakupewa PF3 kama ilivyo kawaida kwa wagonjwa wa ajali wanaopelekwa hospitalini.
Jumaa alisema hadi sasa yupo chini ya uangalizi wa madaktari kwa ajili ya matibabu zaidi hadi kumbukumbu zake zitakaporudi katika hali ya kawaida.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles