27.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

PAMBANO LA WATANI AJIB AWATOA UNYONGE YANGA

Na ABDUL MKEYENGE-DAR ES SALAAM

KIUNGO mshambuliaji wa Yanga, Ibrahim Ajib, amewataka mashabiki wa timu yake waje uwanjani kwenye mchezo wao dhidi ya Simba Jumamosi katika Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam, akiwaambia wasiwe na hofu.

Ajib aliyejiunga Yanga akitokea Simba, amesema wamejipanga vyema kufanya vizuri kwenye mchezo huo na wala hakuna sababu ya mashabiki wa Yanga kuwa na wasiwasi wa kuja uwanjani.

Akizungumza na MTANZANIA jana, nyota huyo aliyefunga mabao matano katika michezo ya Ligi Kuu Tanzania Bara mpaka sasa, alisema haoni sababu ya mashabiki hao kuwa na hofu kwani Yanga wako vizuri.

Alisema kwa maandalizi waliyonayo haoni sababu ya kupoteza mchezo huo na kwamba kocha wao George Lwandamina, amewaandaa vyema kwa ajili ya mchezo huo na mingine.

“Yanga iko vizuri sana tena sana na sioni sababu ya mashabiki wetu kutokuja uwanjani kutushangilia. Niwaambie tu kuwa Yanga iko vizuri ndiyo maana mpaka sasa haijapoteza mchezo, sasa kuna haja gani ya mashabiki kutokuja uwanjani kutuona wachezaji wao tukifanya mambo.

“Tuko katika kiwango kizuri japo watu wanatubeza, kocha wetu Lwandamina ameiweka timu katika mazingira mazuri na sisi (Yanga) hatujiandai kwa ajili ya mchezo mmoja, tumejiandaa kucheza michezo yote ambayo iko mbele yetu,” alisema Ajib.

Alisema anashukuru kuwa na msimu mzuri tangu amejiunga na kikosi hicho na kwamba ni bidii ya mazoezi na maelewano na wachezaji wenzake ndiyo inayomfanya awe katika kiwango bora.

“Hakuna kingine kilichofanya niwe hivi zaidi ya mazoezi ya timu na mazoezi yangu binafsi ambayo yamenisaidia kuwa katika kiwango nilichonacho sasa, lakini kubwa ni ushirikiano ninaoupata kutoka kwa wachezaji wenzangu ambao tunashirikiana pamoja kama timu.

“Unapotaka kufanikiwa unahitaji kujenga ushirikiano ambao mimi nimeujenga kwa kiwango kikubwa ndani ya timu na nashukuru kwa hili, natamani hali hii iliyoko sasa iendelee siku zote ndani ya Yanga,” alisema Ajib.

Ajib amekuwa moja ya wachezaji muhimu kwenye kikosi cha Yanga kwa kuisaidia timu hiyo kufunga mabao na kupatikana kwa mabao mengine yanayofungwa na nyota tofauti kikosini humo.

Mchezo wa mwisho kukutana kwa timu hizo ulimalizika kwa Simba kushinda kwa changamoto ya mikwaju ya penalti ambapo Simba ilipata  nne, wakati Yanga ikipata  tatu katika Uwanja Taifa, Dar es Salaam, ukiwa ni mchezo wa Ngao ya Jamii.

Tayari timu hizo zimeshaingia kambini kila moja kujiandaa na mchezo huo unaosubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wa soka nchini.

Yanga waliokuwa Shinyanga wataweka kambi mkoani Morogoro, wakati Simba tayari wamejichimbia visiwani Zanzibar kujiandaa na mchezo huo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles