30.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Pamba zakwama katika maghala

*Wakulima wazuia magari, wadai fedha zao, Serikali yatoa kauli, wanunuzi wakubali kuingia sokoni

DERICK MILTON NA SAMWELI MWANGA-SIMIYU

IKIWA imepita miezi miwili tangu Serikali kupitia Bodi ya Pamba Tanzania (TCB) itangaze kuanza kwa msimu wa ununuzi wa zao hilo 2018/19, imeibuka sintofahamu baada ya wanunuzi kushindwa kuanza kununua zao hilo kutoka kwa wakulima kupitia vyama vya msingi vya ushirika.

Hali hiyo imewaacha njia panda wakulima wengi, hasa katika Mkoa wa Simiyu ambao uzalisha zaidi ya asilimia 60 ya zao hilo nchini, kutokana na pamba yao hadi sasa kushindwa kununuliwa.

Tangu kuanza kwa msimu wa ununuzi, wakulima wamekuwa wakipeleka pamba yao katika Vyama vya Msingi vya Ushirika (Amcos) bila ya kulipwa fedha zao kinyume na sheria.

Hali hiyo imewalizimu wakulima wengi kila siku kushinda na kulala kwenye maghala ya kuhifadhia zao hilo, huku wakisubiri hatima ya kulipwa fedha zao  na wengine wakizuia magari ya kubeba pamba yasiondoke.

MTANZANIA iliyotembelea baadhi ya vituo vya kununualia zao hilo katika vijiji vya Buhungukila, Bugarama, Malampaka, Badi na Njiapanda katika wilaya Maswa na kubaini hakuna kampuni hata moja iliyoingia sokoni kununua zao hilo kupitia Amcos jambo ambalo ni tofauti na matarajio ya wakulima.

WAKULIMA

Katika Mtaa wa Nyakabindi, Halmashuari ya Mji wa Bariadi, wakulima walizuia gari ambalo lilipakia pamba lisiondoke hadi pale watakapolipwa fedha zao na viongozi wa Amcos.

Gari hilo lenye namba za usajili T 316 AVN aina ya Scania mali ya Kampuni ya Rugeye ya mkoani Mara, lilizuiwa na wananchi kwa kuwekewa mawe.

Wakizungumza na MTANZANIA, wakulima hao walisema kuwa waliamua kuzuia gari hilo, kutokana na wao kuleta pamba takribani mwezi mmoja bila ya kulipwa na bado hawajui hatima ya malipo yao.

“Mimi nimeleta pamba yangu hapa kwenye ghala la Amcos mwezi sasa, lakini hadi sasa ninazungumza nawe sijalipwa hela zangu, nadai zaidi ya laki nane, hatujui huu ni utaratibu gani, wakulima tunakufa na njaa, hatuna chakula, tunategemea hii pamba.

“Sheria ya ushirika inasema mkulima anatakiwa kulipwa ndani ya saa 24, lakini leo ni mwezi mzima wakulima hatujalipwa, tumekopwa pamba yetu, maisha ni magumu, tunamuomba Rais Magufuli aingilie kati suala hili,” alisema Thomas Masunga.

Katika Mtaa wa Sesele, Kata ya Nyakabindi, wakulima wamekuwa wakilala nje ya ghala wakilinda pamba yao ambayo imehifadhiwa hadi nje ya ghala baada ya kujaa.

“Tumelazimika kulala hapa hapa kwa kupokezana ili kulinda pamba yetu ili isipelekwe bila ya kulipwa, maisha yetu yamekuwa magumu sana, hatujui hatima yetu.

 “Tunamuomba Rais Magufuli kama alivyoingilia korosho, aingilie hata pamba, wakulima tunakufa na njaa,” alisema Hassan Deus.

Suzana Maduhu, ambaye alikutwa kwenye ghala hilo akiwa na vifurushi viwili vyenye pamba, alisema kuwa ameileta auze ili apate fedha ya kumpeleka mtoto wake hospitali kwani anasumbuliwa kiafya kwa muda sasa, lakini amekwama kutokana na kukosa fedha za matibabu.

“Nimemwacha mtoto wangu mgonjwa, nimeleta pamba yangu hapa nikauze ili nipate pesa ya kumpeleka hospitali, lakini nimeambiwa niache pamba maana hakuna pesa, sasa sijui nafanya nini mtoto wangu naweza kumpoteza,” alisema Suzana.

KUUZA KWA WALANGUZI

Uchunguzi wa MTANZANIA umebaini kuwa wakulima katika Wilaya ya Maswa, vijiji vilivyo mpakani na Wilaya za Kwimba mkoani Mwanza na Kishapu mkoani Shinyanga wamekuwa wakiuza pamba yao usiku kwa walanguzi kinyume cha sheria.

Wakulima hao wamekuwa wakiuza pamba hiyo kwa walanguzi, hasa wafanyakazi wa viwanda vya kuchambua pamba kwa bei ya chini kama njia ya kuwawezesha kupata fedha jambo lililoibua malalamiko miongoni mwao.

“Hatuna ujanja kwa sasa, tumevuna pamba lakini hakuna wanunuzi, hivyo hawa wamachinga ambao ni walanguzi wakifika tunawauzia pamba na inabidi tuiuze kwa kujificha nyakati za usiku na kilo moja wananunua Sh 700 hadi 800 na tunafanya hivi ili tuweze kupata fedha za matumizi,” alisema Kisenha Sodoka.

PAMBA VIWANDANI

Baadhi ya wakulima wameamua kusafirisha wenyewe pamba yao hadi viwandani na kuuza ili wapate pesa kwa ajili ya kutatua changamoto zinazowakabili na familia zao.

Moja ya kiwanda kilichopokea idadi kubwa ya wakulima kutoka katika wilaya za Bariadi, Itilima na Meatu ni NGS Co. Ltd kilichopo Bariadi.

MTANZANIA ilifika kiwandani hapo na kukuta idadi kubwa ya wakulima wakiwa na mikokoteni iliyojaa pamba, ambao walisema kuwa wameamua kusafirisha wenyewe kutokana na Amcos kutokuwa na fedha za kuwalipa.

“Kwenye Amcos hakuna pesa, sisi tunakuwa na shida nyingi, watu hatuna chakula nyumbani, familia zetu zinateseka, tumeamua kuleta hapa tuone kama tutapata pesa hata kidogo ili zitusaidie kusogeza maisha,” alisema Kalunde Magasha.

SERIKALI YAZUIA

Wakati wakulima hao wakiamua kusafirisha pamba hadi viwandani, Serikali imetoa agizo la kuvitaka viwanda kutonunua zao hilo kutoka kwa wakulima na badala yake wanatakiwa kununua katika Amcos.

Ofisa Kilimo, Umwagiliaji na Ushirika wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa, Robert Urassa, alipiga marufuku wakulima kuuza pamba kwa machinga, huku akiwataka kuwa na subira wakati Serikali ikitafuta ufumbuzi wa jambo hilo.

Lakini hali hiyo imeonekana kuwaumiza wakulima hao ambao walimuomba Rais Magufuli kuingilia kati saula hilo huku wakiukataa mfumo wa kununua pamba kutoka Amcos.

 “Bodi ya Pamba na Serikali wanatulazimisha kupeleka kwenye Amcos ambazo hazina hela, wanaturudisha kwenye enzi za Shireku na Nyanza, watu tunateseka, wengi hapa tunategemea hii pamba kuendesha maisha yetu, hatuzitaki hizi Amcos,” alisema Yohana Mageme.

Meneja wa NGS Co. Ltd, Emmanuel Dandu, alikiri kampuni yake kununua pamba kutoka kwa wakulima, lakini wamesitisha baada ya Serikali kuwapiga marufuku.

“Wakulima wenyewe wameleta pamba sisi tusingelikataa kununua, maana imetupunguzia gharama za usafiri, ila kuanzia leo tumesitisha baada ya agizo la Serikali,” alisema Dandu.

KAULI YA WANUNUZI

Katibu wa Chama cha Wanunuzi wa Pamba nchini, Boaz Ogola, alikiri kuwepo kwa kasi ndogo ya ununuzi wa zao kutoka kwao tangu msimu utangazwe.

Ogola alisema wanunuzi wengi wameshindwa kuanza kununua pamba kutokana na soko la dunia kushuka kutoka senti 76 hadi 60 hali ambayo inaweza kuwaingiza hasara ikiwa watanunua kwa bei iliyotangazwa na Serikali.

Alisema kuwa benki ziligoma kuwakopesha wanunuzi kutokana na hali hiyo ya bei ya soko la dunia kushuka, na kuwafanya washindwe kuingia sokoni kuanza kununua pamba.

“Siyo kweli kama kuna mgomo ila tatizo ni bei, tunatambua kuwa wakulima wanateseka maana pamba ndiyo maisha yao, lakini tupo kwenye mazungumzo na Serikali na tumefika hatua nzuri, ndani ya wiki moja au mbili tutaanza kununua pamba,” alisema Ogola.

NAIBU WAZIRI

Naibu Waziri wa Kilimo, Omary Mgumba, akizungumza juzi, alikiri kusuasua kwa ununuzi wa pamba katika msimu huu, tangu Serikali itangaze bei ya Sh 1,200 kwa kilo moja.

Mgumba alisema kuwa wanunuzi wameshindwa kuingia sokoni kuanza kununua pamba, kutokana na kushuka bei ya zao hilo kwenye soko la dunia hali iliyohatarisha kupata hasara ikiwa watanunua kwa bei elekezi ya Serikali.

“Siku tatu zilizopita tumemaliza kikao na wanunuzi, tumekubaliana kuwa wanunuzi waingie sokoni na kununua kwa bei ile ile ambayo Serikali tulitangaza, na tumewadhamini kwenye mabenki.

“Lakini tumetaka wasiuze pamba yao hadi mwezi Agosti, kama bei ya soko la dunia itaendelea kuwa chini Serikali tutafidia hiyo hasara ambayo watakuwa wamepata,” alisema Mgumba.

Alisema baada ya mazungumzo hayo, benki zimekubali kuwakopesha wanunuzi hao na wako kwenye hatua za mwisho za kupata fedha ili waanze kununua na aliwahakikishia wakulima kuwa ndani ya siku chache pamba itanunuliwa yote.

WAKUBALI KUINGIA SOKONI

Wanunuzi wa pamba mkoani Simiyu wamemhakikishia Mkuu wa Mkoa, Antony Mtaka kuwa kuanzia sasa wataingia sokoni kununua pamba ya mkulima kwa bei elekezi ya Serikali ya Sh 1,200 kwa  kilo moja kwa masharti.

Wamefikia uamuzi huo ikiwa imepita mwezi mmoja na siku 28 tangu Serikali kutangaza bei hiyo elekezi ya kununua zao hilo na wao kusita kuingia sokoni kwa kile kilichoelezwa kushuka kwa bei ya pamba katika soko la dunia.

Wakizungumza jana kwenye kikao cha wadau wa pamba kilichofanyika katika ukumbi wa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, wafanyabiashara wa kuchakata pamba walisema  kuwa hawajagoma kununua zao hilo kama inavyoelezwa na baadhi ya wadau wengine wa zao hilo, lakini kinachowakwamisha kuingia sokoni ni kushuka kwa bei katika soko la dunia na si vinginevyo.

Walisema kuwa kama Serikali ingewaeleza wakulima ukweli kuwa bei ya zao hilo imeshuka katika soko la dunia wasingeweza kukataa kuuza Sh 800 kwa kilo moja.

“Hakuna aliyegoma kununua pamba, bei yake iko chini katika soko la dunia na kama wakulima wakitangaziwa bei imeshuka sokoni, hawawezi kukataa na inawezekana hakuna mnunuzi aliyeingia sokoni na suala la kupewa fidia na Serikali hilo binafsi sikubaliani nalo kabisa,” alisema Jeremiah Malongo ambaye ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Vitrecs Oil Mill.

Walisema sasa umefika wakati kwa Serikali kupunguza makato mbalimbali katika zao la pamba ili mkulima aweze kufaidika nalo kwa kuondoa Sh 30 inayokatwa katika kilo moja ya mkulima kwa ajili ya Mfuko wa kuendeleza zao la pamba (CDTF).

 “Sioni sababu ya kuwepo kwa mfuko huu wa CDTF ambao wanachukua Sh 30 katika kila kilo moja ya pamba inayouzwa na mkulima, ni vizuri fedha hizo zikaongezwa katika mapato ya mkulima ili aweze kunufaika na kilimo anacholima, lakini sisi tununue kwa bei elekezi iliyotolewa na Serikali,” alisema Emanuel Gungu mkurugenzi wa Kampuni ya NGS.

Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Festo Kiswaga alisema baadhi ya kampuni zimeanza kuhujumu wakulima kwa kununua pamba tofauti na bei elekezi ya Serikali kwa kutumia madalali.

Alisema baadhi ya kampuni zimeanza kuvunja sheria kwa kununua pamba kinyume na taratibu na atakayekamatwa atafikishwa kwenye vyombo vya dola.

KAMPUNI 12 ZAPONGEZWA

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mtaka alisema kuwa anazipongeza kampuni 12 zilizokubali kuingia sokoni kununua pamba kwa, huku akizionya baadhi ya Amcos zinazochezea mizani kwa lengo la kuwaibia wakulima.

Aidha aliwataka wakala wa vipimo (WMA) kuhakikisha wanakagua mizani ili wasiruhusu Amcos hizo kuwaibia wakulima.

Alisema Serikali imetoa bei elekezi ya shilingi 1,200 ambayo haina mjadala na wanunuzi wanatakiwa kuwanunulia wakulima zao hilo wakati wakisubiri kupanda kwa bei katika soko la dunia.

“Kwenye suala la uadilifu na hela za watu tusiweke siasa za vyama, wanunuzi msitoe fedha kwa mawakala vijijini kuwanunulia wakulima chini ya Sh 1,200 kwa kilo kwani Serikali imetoa mapendekezo tushikilie marobota yetu ya pamba kwa muda fulani, tuingie sokoni kununua pamba na mapato ya ndani lazima yapatikane, hivyo kesho tuanze  kununua pamba hiyo tena bila kuwakopa wakulima,” alisisitiza Mtaka.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles