26.9 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

PADRI AOMBA JAMII KUWATEMBELEA WAFUNGWA GEREZANI


Na CLARA MATIMO – MWANZA

JAMII imetakiwa kujenga utaratibu wa kuwatembelea wafungwa na kuwapa mahitaji mbalimbali  pamoja na kuwaombea ili waboreshe hali ya maisha yao wawapo gerezani.

Wito huo umetolewa jijini Mwanza na muhudumu wa kiroho katika Gereza la Butimba, Padri  Bernadini Mtuli, alipozungumza katika magereza hayo baada ya wadau mbalimbali kutoa msaada wa vyakula kwa wafungwa wa gereza hilo ili nao waweze kusherehekea sikukuu ya mwaka mpya.

Padri Mtuli  alisema baadhi ya watu huwaona wafungwa kama si binadamu wanaostahili kuishi katika jamii jambo ambalo si sahihi kwani na wao wanastahili kuheshimiwa na kupewa huduma zote.

“Tusiwaone wafungwa kama ni watu ambao ni wa ajabu na hawatakiwi katika jamii, hawa ni ndugu zetu, wengine ni ndugu wa damu pia wote tumeumbwa na Mungu mmoja hivyo tuendelee kuwathamini na kuwatembelea na tuthamini utu wao kwamba wako hapa kwa kipindi kifupi ama kirefu kwa ajili ya kujirekebisha.

“Mara nyingi tumeona kwamba wanapomaliza vifungo vyao na kurudi katika jamii kweli wanakuwa wamejirekebisha na wanaendelea kushirikiana vyema na wanajamii wenzao kwa hiyo tuendelee kuwasaidia hasa pale wanapohitaji msaada wetu,”alisema Padri Mtuli.

Mkuu wa Gereza la Butimba,  Idd Mbaga, alisema wafungwa wana haki zao za kisheria ikiwemo haki ya kupata  matibabu na chakula ndiyo maana jeshi la magereza limetoa  vibali maalum kwa madhehebu mbalimbali ya dini ili yaweze kurudisha  nyoyo zao ambazo zimepondeka na kuwasaidia kwa maombi na mahubiri warudi katika mstari.

Alisema lengo ni kuwafanya  wanapomaliza vifungo vyao waweze kujumuika na jamii  kuleta maendeleo katika familia zao na  taifa kwa ujumla.

Mwenyekiti wa mashirika yasiyo ya kiserikali mkoani Mwanza, Gozbert Mutta, alisema wameweza kuwapelekea wafungwa hao vyakula mbalimbali kwa ajili ya sikukuu ya mwaka mpya.

Diwani wa Kata ya Butimba, John Pambalu, alisema ipo haja kwa jamii kuwatembelea wafungwa na kuwajulia hali maana wao ni sehemu ya jamii na wanahaki ya kutembelewa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles