25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

OMBAOMBA: ZAO LA WAVUTA DAWA ZA KULEVYA, MAJAMBAZI

Na KOMBA KAKOA


NI mchana wa jua kali, katikati ya barabara ya Lumumba, anaonekana mtoto akihangaika kugonga dirisha la moja ya gari lililoko mbele ya macho yake, mara anafuata gari nyingine ambayo pia haikufunguliwa.

Anaendelea na utaratibu huo bila hata kujali kuchomwa na jua ilhali hana hata kofia wala viatu vya kumwepusha kuchomwa na mionzi mikali ya jua.

Namsogelea na kumpa Sh 2,000 ambayo inamfanya akimbilie kwa muuza juisi. Baada ya kununua alinigeukia kwa tabasamu ambalo lilinipa mwanga wa kuendelea kuzungumza naye kujua kilichomsibu na kumsababishia kuingia mtaani kuwa ombaomba.

Anataja majina yake kuwa ni Mahamudu Kileo, mtoto wa pekee katika familia ya marehemu Kileo aliyekuwa akiishi mkoani Dodoma ambaye alifariki katika ajali ya gari akiwa safarini na mama yake.

“Nilizaliwa mwaka 2009 mkoani Dodoma, lakini baadae baba na mama walifariki kwa ajali hali iliyomfanya shangazi anichukue na kuishi naye mkoni Morogoro.

“Hata hivyo, hakunijali kama mwanawe – alinitesa mno, alikuwa akinipiga mara kwa mara bila kosa huku akinishindisha na kunilaza njaa,” anasema Kileo.

Anasema wakati mwingine majirani walimuonea huruma na kumsaidia chakula lakini pindi tu shangazi yake alipogundua aliambulia kipigo na matusi.

Anasema manyanyaso kutoka kwa shangazi yake yalimfanya aamue kutoroka nyumbani na kukimbilia jijini Dar es Salaam, ambako hakuwa na mtu wa kuishi naye hivyo kujiunga na watoto wa mtaani ambao walimtembeza katika maeneo mbalimbali.

“Nilifikia Kariakoo sokoni ambako nililala siku hiyo na kesho yake sikujua sehemu ya kwenda lakini ghafla nilikutana na watoto wengine ambao niliongozana nao huku wakinionyesha maeneo mbalimbali ya kulala kama vile Kigogo, Mchikichini na siku nyingine Upanga,” anasema.

Anasema kwakuwa hakuwa na fedha ya kula, alilazimika kujiunga na watoto wengine kuingia mitaani kuomba msaada kutoka kwa wasamaria wema.

Kuhusiana na kiasi cha fedha anachopata; anasema awali alikuwa akipata Sh 30,000 kwa siku, lakini siku hizi hali imebadilika.

“Nilivyofika zamani nilikuwa nikipata hadi Sh 30,000 kwa siku, lakini sasa hivi hali ni mbaya, nazunguka siku nzima katika maeneo mbalimbali lakini napata Sh 7,000 hadi Sh 8,000,”anasema.

Anaongeza kuwa kutokana na hali ngumu iliyopo, kila siku ya Ijumaa akiwa na wenzake huenda kuomba misikitini baada ya ibada ambako hupata fedha nyingi hadi Sh 25,000.

Anasema licha ya kupata kiasi hicho cha fedha, kuna vijana wakubwa ambao huwaita na kuwapora kisha kukimbia bila kuwaachia kitu.

Anasema nyakati za usiku huwa kuna vijana wakubwa ambao huwaamuru kuwapatia fedha zote walizokusanya kwa siku.

“Kuna jamaa wanavuta bangi zao halafu wanatuita, kutuomba fedha, ukiwaambia huna wanakusachi na kuchukua zote na ukipiga kelele wanakutishia kisu na kukupiga,” anasema.

Anasema awali alikuwa na ndoto ya kuwa daktari, lakini imezima kwa kukosa msaada.

“Nilitamani kuwa daktari lakini haitawezekana kwa sababu sina mtu wa kunisomesha hivyo nitaendelea kuwa mtaani,” anasema.

 

Hujifunza wizi

Jambo la kusikitisha ni kwamba licha ya watoto hao kuomba mtaani lakini pia hujifunza wizi, matumizi ya dawa za kulevya, uvutaji bangi, kunywa pombe aina ya konyagi ambazo hupimwa kwenye vikombe vinavyotumika kuuzia kahawa katika vituo vya daladala.

“Wengine wamejifunza kuvuta bangi, kula unga kwani wanatumwa na wale mateja na wakirudi wanavuta pamoja… siku nyingine wakikosa bangi wanavuta gundi na kulewa,” anabainisha Kileo.

 

Wengine hutumwa na wazazi

Kiama Mseji naye ni miongoni mwa watoto wa mtaani ambaye hutumiwa na bibi yake kufanya kazi ya kuomba.

Anasema huwa wanalala Mchikichini na asubuhi huingia mtaani kwa ajili ya kuomba, hii ni kwa sababu bibi yake hana kazi ya kufanya.

“Niko na bibi yangu tunatokea Mchikichini, tukifika huku ananituma naomba nikipewa fedha nampelekea ili ahifadhi kwa sababu wenzangu wanaweza kunipora,” anasema Mseji.

Alipoulizwa kuhusu kiasi cha fedha anachopata kwa siku, alishindwa kufahamu kwa kuwa yeye kazi yake ni kuomba na bibi huzichukua na kuzihifadhi.

Hata hivyo, bibi wa mtoto huyo aligoma kuzungumzia suala hilo huku akimtukana mjukuu wake na kumwamuru waondoke katika eneo hilo kwa madai kuwa limeingia mikosi.

“Kwanini unazungumza na watu wasiokupa pesa? Umenunuliwa kijuisi cha 500, unaacha kufanya kazi unaongea utumbo hebu tuondoke eneo lenyewe limeingia mkosi,” alimsema mjukuu wake kwa lugha chafu.

 

Hutumia majeraha kama mtaji

Kuna kundi lingine ambalo ni majeruhi wa ajali mbalimbali, hawa hutumia majeraha yao kama fursa ya kupata huruma ya wapita njia.

MTANZANIA limemshuhudia kijana mmoja wa makamo katika kituo cha daladala Makumbusho akitumia mguu wake uliovunjika kuomba msaada kituoni hapo.

Kijana huyo huonesha watumiaji wa kituo hicho kidonda chake ili wamuhurumie na kumpatia msaada wa fedha.

Hata hivyo, mwandishi alijaribu kuzungumza naye lakini hakuonyesha ushirikiano kwa madai kuwa ni kumchoresha.

“Oya tusizinguane, mbona unanichoresha mwanangu acha hizo wewe fanya yako, hapa mjini fanya yako…,”alisema.

 

Waiba mali za mwandishi

Jambo la kushangaza ni kwamba, wakati mwandishi wa makala haya akiwa anazungumza na Kileo, lilitokea kundi la ombaomba na kumwibia pochi ya kuhifadhia fedha, vitambulisho, kikiwamo cha New Habari (2006) Ltd, kadi ya benki CRDB, NIDA, kitambulisho cha kupigia kura, kadi nyingine za mawasiliano pamoja na fedha taslimu Sh 15,000.

Baada ya mazungumzo na Kileo ndipo aligundua kuwa amepotelewa na vitu hivyo.

Kutokana na hali hiyo, Kileo alilazimika kumtembeza katika maeneo mbalimbali ambayo watoto hao wa mitaani huficha vitu baada ya kuiba.

Baada ya mzunguko aliyochukua takriban saa mbili, alifika katika gofu moja lililopo mtaa wa Upanga na kufanikiwa kuona baadhi ya vitambulisho.

Miongoni mwa vitambulisho vilivyopatikana ni pamoja na kile cha kazi, NIDA, lakini fedha na kitambulisho cha kupigia kura havijaonekana.

Aidha, hatua hiyo ilimfanya mwandishi kwenda kutoa taarifa katika kituo kidogo cha Polisi Mnazi Mmoja ambako alitakiwa kwenda Tume ya Uchaguzi kupewa barua na benki husika kwa ajili ya kupata barua itakayosaidia kufunguliwa kwa taarifa za upotevu wa vitu hivyo.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles