27.5 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Ombaomba: Mjini kila mtu ana kazi yake

MAKONDASAFIASIFIWE GEORGE NA REHEMA ABDALLAH (A3), DAR ES SALAAM

OMBAOMBA katika jiji la Dar es Salaam  wamemjibu Mkuu wa Mkoa, Paul Makonda wakisema  hawawezi kuondoka kwa vile ‘mjini kila mtu ana kazi yake’.

Wamesisitiza  kuwa hawawezi kuondoka   Dar es Salaam kwa sababu wamekuja kutafuta kipato.

Baadhi ya ombaomba  walitoa kauli hiyo kwa nyakati tofauti jana, baada ya Gazeti hili kutaka maoni yao kuhusu tamko la    Makonda kwamba atafanya operesheni ya kuwakamata  Aprili 18 mwaka huu.

“Mimi siwezi kurudi Dodoma  kwa sababu nauli ni kubwa. Nilikuja jana kwa kulipa Sh 20,000 sasa mimi nitapata wapi fedha nyingine? Kama anataka tuondoke atupatie nauli.

“Kama hawezi kutupatia nauli atupeleke popote sisi tutaendelea  kuomba   tuweze kujipatia kipato kwa ajili ya kujikimu maisha.

“Kama unavyoniona mimi na familia yangu nimekimbia Dodoma kutokana na mafuriko… sasa wakiniambia nirudi nitaenda wap?.

Pamoja na kunipatia nauli wanifanyie mpango wa nyumba ya kuishi,” alisema mmoja wa ombaomba hao, Amina Ramadhani aliyekuwa eneo la Mnazi Mmoja.

Mwingine aliyekuwa amekaa na watoto wake wanne na ambaye hakutaka jina lake litajwe alisema: “Kila mmoja na kazi yake hapa mjini.

“Sisi tutaendelea kuomba kwa sababu ndiyo kazi yetu inayotupatia kipato cha kuendeshea familia zetu”.

Ombaomba mwingine ambaye naye alikuwa eneo la Mnazi Mmoja na pia hakutaka kutaja jina lake  alisema  viongozi wa Serikali nao ni wazazi kwa hiyo wanapaswa kuangalia namna ya kuwasaidia.

Akizungumza na waandishi wa habari   Dar es Salaam jana, Makonda alisema  muda wa ombaomba katika jiji  umekwisha hivyo amewataka kufungasha virago vyao na kurudi makwao.

Alisema amefanya utafiti na kugundua kuwa asilimia 80 ya ombaomba wanatoka nje ya Mkoa wa Dar es Salaam na asilimia 20 ni wakazi wa jiji.

Makonda alieleza masikitiko yake kuwa ombaomba hao  wamekuwa wakiwatumia watoto wao kuomba ili kujipatia kipato.

“Ombaomba wote wafahamu kwamba mji unapaswa kuwa safi na wale wanaokaa katika makutano ya barabara au nje ya maduka ya watu kwa ajili ya kuomba, watambue kwamba muda huo umekwisha, wanapaswa kurudi  katika mikoa yao.

“ Wafanyabiashara wengi wamekuwa wakiwalalamikia ombaomba wanaolala kwenye milango ya biashara zao kwamba hujisaidia hapo hapo hali inayochafua  mazingira na kusababisha usumbufu mkubwa.

“Sasa ninasema ombaomba hawa wamekuja kwa nauli zao hivyo wataondoka kwa nauli zao… nitakayemkamata katika operesheni yangu nitakayoifanya Jumatatu nitamchukulia hatua za  sheria ikiwa ni pamoja na kumfikisha mahakamani,” alisema Makonda.

Naye Kamanda wa Polisi Kanda ya Dar es Salaam,  Simon Sirro, alisema ombaomba ni wengi  katika jiji  na wanaopaswa kufuatilia watu hao ni viongozi wa Serikali za mitaa lakini wamekaa kimya.

“Wenyeviti wa Serikali za mitaa ni wajibu wao kuwashauri watu hawa hivyo tunawaomba wafanye hivyo kabla mkuu wa mkoa hajaanza kufanya operesheni hiyo,” alisema.

Wakati huo huo, Makonda amewataka   wote waliojenga maghorofa bila kutenga maeneo ya kuegesha magari, wayabomoe la sivyo watafute maeneo mengine kwa ajili ya maegesho.

“Majengo makubwa yanapaswa kuwa na maegesho. Ninashangaa kuona magari yameegeshwa ovyo ndani ya jiji hasa pembezoni mwa barabara hali inayosababisha watembea kwa miguu kukosa maeneo ya kupita kutokana na magari hayo.

“Hii ni hatari kwa sababu  mtu anaweza kugongwa kutokana na uzembe wa watu wasiozingatia sheria,” alisema Makonda.

Pia aliwataka wamiliki wa baa  kufuata sheria za leseni  zao na kufunga muda waliopangiwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles