26.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Oliver Semuguruka: Niliichukia siasa lakini nikajipa moyo nitashinda  

pg 12NA GUSTAPHU HAULE, DODOMA

UNAPOWATAJA wabunge wa Viti maalumu waliopo katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, huwezi kusahau kumtaja Oliver Semuguruka. Mbunge huyu alitwaa kiti hicho kupitia

Chama Cha Mapinduzi (CCM), akiwakilisha Mkoa wa Kagera huku chimbuko lake likiwa ni Wilaya ya Ngara.

Alibahatika kupata nafasi hiyo akiwa na umri wa miaka 30, ambapo alikuwa mdogo peke yake miongoni mwa wagombea aliopambana nao katika kinyang’anyiro kilichofanyika Julai 2015 mjini Bukoba.

Katika uchaguzi huo, ambao ulisimamiwa na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera, John Mongella, Oliver alipambana na watu maarufu akiwamo Elizabeth Batenga, aliyekuwa akitetea nafasi hiyo.

Mchuano wa Batenga na Oliver ulikuwa mkali lakini hata hivyo,  Oliver aliibuka kidedea baada ya kupata kura 314 wakati Batenga aliyekuwa kwenye nafasi hiyo kwa kipindi cha miaka 20 akipata kura 255.

Oliver alishika nafasi ya pili baada ya nafasi ya kwanza kuchukuliwa na Bernadetha  Mushashu, ambaye alipata kura  432 kati ya 626 huku kura 637 zikiharibika.

Mwishoni mwa wiki iliyopita MTANZANIA, lilifanya mahojiano na mwanasiasa huyo ambapo anaeleza furaha yake baada ya kutangazwa kuwa mbunge.

Anasema furaha hiyo ilitokana na kipindi cha kampeni ya uchaguzi wa mwaka 2015, alipitia changamoto nyingi ikiwamo kupata ajali na hata kugombana na wanasiasa wenzake.

“Kipindi cha kampeni za uchaguzi kilikuwa kigumu kwangu maana nilipitia misukosuko mingi kiasi ambacho kilinifanya nichukie siasa, lakini pamoja na  yote hayo sikukata  tamaa bali niliendelea kumuomba Mungu,” anasema.

Oliver anawashukuru wapiga kura wake ambao kwa namna moja au nyingine walijitoa kuhakikisha anashinda.

“Kweli, bila hawa akina mama wa UWT na wanaCCM wa Mkoa wa Kagera kuniunga mkono, leo hii nisingekuwa mbunge… nawaahidi kuwatumikia kadri ya uwezo wangu,” anaahidi.

Anasema kinachofanyika sasa ni kuvunja makundi na kuondoa tofauti zao za kisiasa ili kuwatumikiwa Watanzania ipasavyo, bila kuangalia itikadi za vyama, dini wala kabila.

Mbunge huyo anasema kiu ya wananchi wa Mkoa wa Kagera ni kuona kero zao zinapatiwa ufumbuzi hivyo, lazima ajitoe katika kuwatumikia.

“Dhamana niliyopewa na wanachama wa CCM ni kubwa lakini nasema nipo tayari kuwatumikia wananchi wote ili ifike mahali mkoa wetu upate maendeleo zaidi,” anasema.

Anabainisha kuwa mkoa huo bado unachangamoto nyingi hususani barabara, maji, elimu, afya na hata ajira kwa vijana, hivyo yupo tayari kushirikiana na wabunge wenzake na viongozi wengine wa serikali kuhakikisha wanatatua kero hizo.

“Kagera tunachangamoto nyingi, lakini ni imani yangu kuwa wabunge wa mkoa huu kwa kushirikiana na viongozi wengine wa serikali tunatapunguza changamoto hizo,” anaongeza.

Anasema atawakilisha kero hizo bungeni ili serikali iweze kuzitambua na baadae zipewe kipaumbele katika utekelezaji wake.

“Ni mara yangu ya kwanza kuingia bungeni lakini najua nimekuja kuwatumikia wananchi wa Kagera hivyo siwezi kuwaangusha kwani nipo mstari wa mbele kuwapigania, kikubwa ninachohitaji ni ushirikiano wao,” anasema.

Anasema kwa sasa tayari baadhi ya changamoto ameanza kuzisemea bungeni ikiwamo ya barabara ya Mizani, Murusagamba, Murugalama pamoja na Karagwe kupitia pori la Kimisi- Tubenako-Ngara.

Oliver anapigania barabara hizo ili zijengwe kwa kiwango cha lami na majibu ya serikali kupitia Wizara ya Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano yanaleta matumaini.

Anasema mbali na barabara hizo pia ataendelea kuzipigania barabara nyingine za Wilaya ya Ngara, ili ziweze kujengwa na kupitika kirahisi katika vipindi vyote.

“Barabara zikiwa katika hali nzuri nina imani uchumi wa mkoa nao utaimarika, kwa kuwa wananchi na wafanyabiashara wakubwa watazitumia katika kusafirisha mazao na bidhaa zao,” anasema.

Anasema serikali ya Rais dk. John Magufuli, imejipanga vizuri katika kuwatumikia wananchi wake hususani kwa kuondoa kero zinazowakabili.

Anasema kwamba anatambua wapo akina mama, wazee na vijana ambao wanakabiliwa na changamoto za kiuchumi lakini jambo kubwa ni kujiunga katika vikundi mbalimbali vya kijasiriamali.

Anabainisha kuwa serikali ina mikakati mingi ya kuwawezesha wananchi wake kiuchumi ndio maana Rais Dk. Magufuli aliahidi kutoa Sh milioni 50 kila kijiji.

Anashauri ili wananchi waweze kunufaika na fedha hizo, lazima wajiunge katika vikundi ili zinapokuja jamii yote ya Kagera iweze kunufaika.

“Naamini serikali ya awamu hii ina mikakati mizuri ya kuwawezesha wananchi wake kiuchumi, lakini cha msingi ni kuhakikisha fursa zinazotolewa zinatumika vizuri ili kila mwananchi aweze kunufaika nazo,” anasema.

Anasema kazi kubwa ya wabunge ni kuhakikisha wanasimamia kikamilifu mipango na mikakati ya serikali iliyowekwa kwa ajili ya kuwainua wananchi wake kiuchumi.

Oliver anatumia fursa hiyo kuwaasa wananchi na wanachama wa CCM kiujumla kuendelea kumuunga mkono Rais Magufuli ili aweze kutekeleza vyema mipango yake ya kuwaletea Watanzania maendeleo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles