Walter Mguluchuma -Katavi
OFISA mstaafu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania ambaye alistaafu hivi karibuni akiwa na cheo cha Meja, Inginus Isanga (54) amekikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Katavi kwa tuhuma za kuwabaka watoto watatu Wanafunzi wa darasa la tatu na la nne wa shule ya Msingi Muungano katika Manispaa ya Mpanda.
Watoto hao, wawili ni wa familia moja.
Mtuhumiwa huyo alifikishwa mahakamani jana kusomewa na mashitaka na Mwendesha Mashtaka Mfawidhi wa ofisi ya Taifa ya mashitaka Mkoa wa Katavi, Elisante Masaki mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Katavi, Emanuel Ngigwana.
Mwendesha mashitaka huyo alidai kuwa mtuhumiwa huyo ambae ni ofisa mstaafu wa JWTZ alitenda kosa hilo la kuwabaka watoto hao kwa nyakati tofauti kati ya Machi 1 na 2 mwaka huu.
Alidai mtuhumiwa aliwatongoza watoto hao wenye umri wa miaka 13 na 14 ambao ni wanafunzi wanaosoma katika shule ya Msingi Muungano katika Manispaa ya Mpanda darasa la tatu na la nne kwa kuwaahidi kuwapatia kiasi cha Sh 20,000 kila mmoja.
Mwendesha mashitaka huyo alidai kuwa mshitakiwa aliweza kuwabaka watoto hao katika nyakati tofauti katika nyumba ya kulala wageni iliyoko katika Mtaa wa Tambukaleli na kuwapatia kiasi cha Tshs 20,000 baada ya kuwa amewafanyia kitendo hicho cha kuwabaka .
Baada ya mshitakiwa kusomewa mashataka hayo, Hakimu Ngigwana alitaka ayajibu kama anayakubali au anayakataa ili mahakama iweze kuendelea na taratibu nyingine za kesi hiyo .