27.9 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

OBAMA ATUA NCHINI KIMYA KIMYA

Na MWANDISHI WETU – KILIMANJARO


RAIS Mstaafu wa Marekani, Barack Obama, amewasili nchini kimya kimya akiwa na familia yake.

Hii ni mara ya pili kwa Obama kuja nchini, ambapo mara ya kwanza ilikuwa Julai 2013, wakati kiongozi huyo akiwa bado madarakani.

Ziara yake hiyo ya kikazi ilikuwa ni sehemu ya kukamilisha ratiba yake ya mwisho ya ziara barani Afrika wakati akiwa Rais.

Tofauti na ziara yake ya awali ambapo alikuja na ndege ya Air Force One akiwa na msafara unaolindwa na kila aina ya teknolojia, safari hii alikuja na familia yake lengo likielezwa kuwa ni kwa ajili ya kupumzika.

Chanzo cha uhakika kililiambia MTANZANIA kuwa Obama alitua nchini  kimya kimya ambapo aliwasili Jumapili ya Julai 8, mwaka huu na kushukia katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro  (KIA) na kufanya mazungumzo na kiongozi mmoja mwandamizi wa Serikali katika eneo maalumu ambalo lilitengwa mjini Moshi.

Baada ya mazungumzo na kiongozi huyo wa Serikali yaliyodumu kwa takribani dakika 40, Obama alirejea KIA akiwa kwenye gari maalumu na kupanda ndege ndogo maalumu na kwenda kupumzika Mbuga ya Serengeti.

“Alipanda ndege ndogo akaenda Serengeti ambapo amefikia Singita Grumeti,” kilisema chanzo chetu.

Pamoja na hali hiyo inaelezwa kuwa Rais huyo Mstaafu wa Marekani, atakuwa hapa nchini kwa mapumziko ya wiki moja pamoja na familia yake.

Akiwa ndani ya Mbuga ya Serengeti atajionea utajiri mkubwa wa maliasili uliopo nchini pamoja na vivutio vyake ikiwamo wanyama.

Katika ziara yake ya mwaka 2013, Obama  aliisifu Tanzania na kusema ni kama nyumbani kwake, kutokana na historia yake.

Alisema uhusiano uliopo kati yake na Tanzania, umewafanya baadhi ya wanafamilia wake kuwa na uhusiano wa kuitembelea Tanzania kwa shughuli mbalimbali.

Katika mkutano wake na wanahabari uliofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam, ambapo alikuwa na mwenyeji wake wakati huo Rais Mstaafu Jakaya Kikwete, Obama alisema anajisikia fahari kuitembelea Tanzania, kwani ni moja ya nchi zinazounda Jumuiya ya Afrika Mashariki, ambayo anatoka baba yake.

Alisema Marekani na Tanzania, zimekuwa na uhusiano wa muda mrefu ambao uliwekwa na marais waliotangalia wa nchi hizo, akiwemo Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere na Rais wa 35 wa Marekani, John F. Kennedy.

 

Inaendelea…………………… Jipatie nakala yako ya gazeti la MTANZANIA.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles