Nyumbu wawaacha hoi watalii Serengeti

0
1028

Na JANETH MUSHI -SERENGETI

MAMIA ya watalii kutoka mataifa mbalimbali duniani, wako katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti eneo la Kanda ya Kaskazini, Mkoa wa Mara, kushuhudia tukio la kihistoria la nyumbu wakivuka Mto Mara wakitokea Mbuga ya Maasai Mara nchini Kenya na kuingia Serengeti Tanzania.

Aidha, tukio hilo ambalo hutokea mara moja kwa mwaka, licha ya kuvutia mamia ya watalii hao, pia linatajwa kuwa miongoni mwa vivutio vya pekee katika hifadhi hiyo.

Kutokana na umuhimu wa tukio hilo, baadhi ya watalii wamelazimika kuongeza siku za kukaa nchini ili kushuhudia makundi ya wanyama hao wakivuka mto huo.

Tukio hilo lilitokea juzi katika kivuko namba nne ambapo baada ya kusubiriwa kwa zaidi ya saa tano, makundi makubwa ya wanyama hao yalianza kuvuka mto huo na kushuhudiwa na mamia ya watalii hao.

Mhifadhi wa Hifadhi ya Serengeti, Kanda ya Kaskazini, Lameck Matungwa, alisema inakadiriwa kila mwaka nyumbu zaidi ya milioni moja na nusu huvuka kutoka upande wa pili wa mto huo kuanzia Julai kila mwaka.

“Tukio hili linafanyika mara moja kwa mwaka na katika eneo hili, nyumbu wanashuka kuanzia Julai kwa sababu wanafuata malisho.

“Wanavuka kwa makundi, watalii wengi huvutiwa na namna nyumbu hao wanavyovuka bila kujali mto una maji au hauna maji.

“Wanyama hawa ni wa ajabu na huvuka kwa makundi, wengine hupelekwa na maji, kingine kikubwa ni namna wanavyovuka na kukabiliana na wanyama wakiwamo mamba.

“Mbali na sababu za kiikolojia ikiwamo kuzaliana, wanavuka upande wa pili kufuata malisho na maji na makundi hayo huongozwa na kiongozi mmoja ambaye akishaanza kuvuka, haijalishi usalama wao uko kiasi gani,” alisema Matungwa.

Kwa upande wao, baadhi ya watalii na waongoza watalii walioshuhudia tukio hilo, walisema lina umuhimu mkubwa kwa sababu linachangia kukuza na kuongeza pato la Taifa.

“Tumeona nyumbu wakivuka maji kitu ambacho tumekuwa tukisimuliwa, tumeona leo kwa mara ya kwanza na kiukweli tunafurahia sana hili ni tukio muhimu sana kwetu,” alisema mtalii Joseph Schwachter kutoka Marekani.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here