27.1 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Nyuma ya Stars kuchemka Afcon kuna haya

NA MOHAMED KASSARA

TIMU ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ leo itashuka dimbani kucheza mchezo  wa mwisho wa kundi C wa fainali za mataifa ya Afrika(Afcon), zinazoendelea kushika kasi nchini Misri.

Stars ni miongoni mwa timu zilizotupwa nje katika michuano hiyo, baada ya kupoteza michezo miwili mfululizo ya hatua ya makundi.

Timu hiyo ilijikuta ikiaga michuano hiyo, baada ya kuchapwa mabao 3-2 na  majirani zao, Kenya katika mchezo wa pili, uliochezwa Alhamisi iliyopita   Uwanja wa June 30, Cairo.

Kipigo hicho kiliifanya Stars kuendelea kuburuza mkia katika msimamo wa kundi hilo, ikiwa imecheza michezo miwili na kuambulia patupu.

Stars ilianza vibaya michuano hiyo  kwa kupokea kichapo cha mabao 2-0, kutoka kwa Senegal,  katika mchezo wa kwanza uliochezwa Jumapili iliyopita kwenye Uwanja huo huo.

Kwa maana hiyo, Stars itaingia kwenye mchezo wa mwisho dhidi ya Algeria ambayo tayari imeshatinga 16 bora, utakaochezwa leo kukamilisha ratiba tu.

Stars  imebakiwa na mchezo mmoja dhidi ya Algeria, lakini kiuhalisia hata itapata ushindi hautaweza kuipeleka popote bila kujali matokeo ya mchezo Senegal na Kenya yatakuaje.

Sheria ya matokeo baina ya timu mbili ndio ‘head to head’ ndio huangaliwa katika michuano hiyo na tayari ilifungwa mabao 2-0 na Senegal kabla ya kupoteza kwa Kenya.

Kufanya huko vibaya kwa Stars kumeibua mjadala mzito kwa wadau wa soka wakitoa sababu tofauto tofauto zilizosababisha  iwe msindikizaji

Wapo walimnyoshea kidole kocha wa kikosi hicho, Emmanuel Amunike wakiamini ndiye chanzo cha matokeo mabovu  ya Stars, kutokana na kutowajumuisha baadhi ya nyota pamoja na kushindwa kukipanga vizuri kikosi chake.

Hoja hizo zilianza kuibuka baada ya Stars kupoteza mchezo wa kwanza dhidi ya Senegal, wengi walihoji namna kikosi kilivyocheza  kwa kiwango duni na uchaguzi wa wachezaji kwenye baadhi ya maeneo hasa eneo la katikati ya uwanja kwamba haukuwa sahihi.

Lakini ubora wa kikosi cha Senegal ulizima haraka mjadala na wadau kuona kweli hatukuwa na jambo jipya la kuifanya Stars ipate pointi tatu au moja mbele ya Simba hao wa Teranga.

Hata hivyo, ubora wa Senegal ikiwa namba moja kwa uimara katika soka Afrika na 22  duniani  unathibitisha  uhalali wa tofauti ya kiwngo katika ya vikosi hivhi viwili.

Kitu kingine ni uzoefu, Senegal inashiriki fainali za mwaka huu kwa mara ya 15, ingawa  haijawahi kutwaa ubingwa huku mafanikio yake kwa miaka ya karibuni ni kufika fainali mwaka 2002a na kuchapwa na Cameroon.

Kingine, wachezaji wao wengi wanacheza soka la kulipwa Ulaya, sehemu ambapo wanapata changamoto mpya kila mwisho wa wiki, tofauti na Mudhatir Yahya ambaye , wiki hii anacheza dhidi ya Biashara United, wiki inayofuata na Stand United.

Isingekuwa rahisi kwa Kelvin Yondani kumdhibiti mshambuliaji kama Keita Balde ambaye anapambana na mabeki kama Kalidou Koulibaly wa Napoli, Leonardo Bonucci wa Juventus kwenye Ligi Kuu Italia ‘Serie A’.

Hakuna maajabu ya Feisal Salum kumzima kiungo Idrissa Gana anayekipiga Everton na kupigana vikumbo na wakali , Paul Pogba, N’golo Kante, Fenandinho kwenye Ligi Kuu England kila wiki.

Hata hivyo, kitendo cha kufungwa na majirani zetu, Harambee Stars kimechafua zaidi hali ya hewa na kuibua mapya ambayo yalianza kufunikwa baada ya mchezo wa kwanza.

Kibaya zaidi, Stars ilianza vizuri mno kipindi cha kwanza na kuongoza kwa 2-1, lakini cha ajabu Kenya ilitoka nyuma na kuibuka na ushindi wa mabao 3-2, ambao umewaweka katika mazingira mazuri ya kutinga 16 bora.

Licha ya makosa yaliyosababisha kupoteza mchezo wa kwanza kujirudia, lakini ukweli ni kwamba tumeendelea kuvuna tulichopanda katika michuano hiyo.

Hawa Kenya ambao tunadhani tulistahili kupata pointi tatu mbele yao, wenzetu wanashiriki Afcon yao ya sita, mara ya mwisho ilikuwa mwaka 2004, zilipofanyika Tunisia.

Kitu pekee kinachotupa imani ya kuamini tuko sawa nao, labda ni ujarani tu na si kingine, wenzetu wana wachezaji wanaocheza ligi kubwa Ulaya na kwingineko duniani.

Wana Victor Wanyama ambaye ameisaidia Tottenham Spurs kufika fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu uliopita, Michael Olunga ambaye amepita ligi za Hispania, China na Japan.

Lakini kwa upande wa Stars, wachezaji wengi ukimwondoka Samatta na wenzake wachache wanashiriki Ligi Kuu Tanzania Bara isiyokuwa na ushindani  zaidi ya kushuhudia utawala wa Simba na Yanga.

Pia kuna upangwaji hovyo wa ratiba,  malamiko ya kupendelewa kwa timu kubwa za Simba na Yanga na wachezaji kutojitambua nini wanatakiwa kufanya wanapopata fursa adimu kama fainali za Afcon.

Serikali pia haijaweka kipeumbele kwenye sekta ya michezo, kwani bajaeti inayotengwa  katika Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo  ni ndogo kulingana  na mahitaji  halisi ya kuendeleza mchezo huo.

Sahau kuhusu serikali kutoweka bajeti ya posho na motisha kwa wachezaji kwa ajili ya michuano hiyo, lakini kitendo cha kupitisha bakuli la kuichangia timu hiyo ni moja kati ishara za kushindwa kujipanga mapema.

Wabunge walikwenda Misri kushudia baadhi ya mechi, lakini waliporudi walikuja na maneno makali kuhusu walichoakiona, lakini wanasahau kuwa wao nao ni sehemu ya tatizo hilo kwa kushindwa kutunga sera nzuri ya michezo na kusimamia upitishaji wa bajeti ya michezo.

Kama tunataka kufanikiwa hakuna njia ya mkato lazima tuwekeze kwenye soka, tubadili mfumo wa uendeshaji ligi zetu, lakini pia wachezaji kubadili mitazamo yao kuhusu Simba na Yanga.

Matokeo mabaya tuliyopata Afcon, yatuamshe kutoka usingizi kuelekea michuano inayokuja kama fainali za mataifa ya Afrika kwa wachezaji wanaocheza  ligi za ndani (CHAN), lazima nguvu zetu zielekezwe huko na si kulalamika.

Wasikie baadhi  ya wadau waliofunguka kuhusu kilichoikuta Stars;

Hussein Ngulungu

Kiungo huyo zamani wa Stars alisema hajashangazwa na matokeo hayo kutoka na kile alichodai kuwa tulifuzu kwenye michuano hiyo kwa bahati tu, hivyo timu haikuwa imejiandaa kikamilifu kupambana.

“Nilisema mapema hapa nikaoneka siyo mzalendo, tena baadhi ya watu wakachukua na maneno yangu kama kuikana nchi yangu, sijashangwa sana na matokeo hayo, simlaumu mwalimu, lakini tujitazame tulijikwaa wapi, hatuwezi kumtupia lawama mwalimu, amejitahidi kuwapa alichonacho wachezaji, lakini tumefeli kutokana na kutojiaanda vizuri mapema.

“Tulifuzu kwa bahati tu kwa Uganda, hilo lazima tulielewe, ukutaka kujua ukweli wa hilo waangalie Uganda, wamepata pointi nne mbele ya timu ngumu, hivi unadhani timu ile sisi tuliifunga mabao matatu, ni uongo, wachezaji wetu bado hawana uwezo kupambana kwenye michuano mikubwa kama hiyo, ni wakati wa kujitazama kuanzia kwenye ligi yetu ya ndani, tuanze kurekebisha hapo, lakini si kumtupia mtu lawama, alisema kiungo huyo wa zamani wa timu hiyo.

Msolla

Mwenyekiti wa Yanga, Mshindo wa Msolla alisema  matokeo hayo tuliyovuna ni matokeo ya tulichopanda, hivyo asitokee mtu kuangushiwa lawama kwa lolote lililotokea Misri.

Alisema timu ya Taifa imekuwa haina maandalizi mazuri kwa muda mrefu sasa, pia wachezaji kutokuwa na nidhamu ya mchezo ni sababu nyingine iliyosababisha kuambulia patupu kwenye michuano hiyo.

“Tumefanya vibaya kwa sababu kadhaa ambazo zinajulikana, timu yetu haina maandalizi mazuri, tumekuwa tukifanya maandalizi ya zima moto, wachezaji wetu pia hawana nidhamu ya mchezo, tuliongoza kwa mabao mawili, lakini wameshindwa kulinda ushindi huo.

“Kitu kingine kinachotukwamisha ni ligi yetu kutawaliwa na wageni, tuseme ukweli,japo tunasajili wachezaji hawa kutoka nje, lakini wanapoanza wengi kwenye kikosi kunasababisha vijana wetu kushindwa kupata nafasi mara kwa mara,”alisema Msolla ambaye aliwahi kuinoa timu hiyo kwa vipindi tofauti miaka ya 2000.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles