23.3 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

NYERERE ALIKUWA NA NIA YA KUTENGENEZA UCHUMI

Na DOTTO BULENDU


nyerereMWALIMU Julius Nyerere alikuwa na nia ya dhati kabisa kuhakikisha anatengeneza nchi ya ujamaa na kujitegemea. Mwalimu alilifanya suala la ujamaa na kujitegemea ni suala la kila Mtanzania na si la wachache.

Mwalimu alikutana na changamoto kubwa ya vita baridi, kwa maana ya mataifa yaliyokuwa yakiamini katika ujamaa na yale yaliyokuwa yakiamini katika ubepari.

Watanzania waliokwenda kusoma nchi za kibepari waliporudi nchini baadhi waliipinga falsafa ya Mwalimu na wengine walimpinga waziwazi. Julius Nyerere kwa sababu alidhamiria kujenga nchi ya ujamaa na kujitegemea alisimamia misimamo yake bila kuyumba, alikwaruzana mpaka na waziri wake wa fedha kipindi cha wananchi kujifunga mkanda miaka ya mwanzoni mwa 80, Edwin Mtei, mpaka Mtei akaandika barua ya kuachia ngazi.

Pamoja na kupishana kimtazamo, Mwalimu Nyerere na Mtei hawakuwahi kuwa maadui, nakumbuka nilipomtembelea mzee Mtei nyumbani kwake Tengeru Novemba, aliniambia ni Mwalimu ndiye aliyependekeza jina lake kuwa Mkurugenzi wa IMF barani Afrika kwa nchi zinazozungumza lugha ya Kiingereza.

Mwalimu aliipigania sana nchi yake, alijenga viwanda, aliunda mashirika ya umma na maduka ya Serikali pamoja na kujenga viwanda vingi kama nyuzi Tabora, nyama Shinyanga na Dar es Salaam, maziwa Utegi Mara, matairi Arusha, nguo Mwanza na Musoma, viberiti Kilimanjaro, magunia Iringa, za zana za kilimo Mbeya, makaratasi, sigara Morogoro n.k.

Mwalimu alihamasisha kilimo, mashamba makubwa yaliyoachwa na wakoloni kuanzia Karatu, Tanga, Morogoro n.k yaliendelezwa kwa ufasaha na Serikali.

Kosa alilofanya Mwalimu ambalo Serikali za sasa hazitakiwi kulirudia ni kutojenga sekta binafsi za ndani, kutotunga sera madhubuti itakayozalisha matajiri wa ndani.

Mwalimu Nyerere aliamini Serikali inaweza kufanya kila kitu bila kuzishirikisha sekta binafsi, alitaifisha kwa nia njema na kuikabidhi Serikali shule, hospitali ili iyaendeshe.

Hali ya utoaji huduma chini ya Serikali ilikuwa mbaya mpaka mwaka 1992 pale Serikali ilipoingia mkataba na madhehebu ya dini ili yasaidie kwenye utoaji wa huduma kama afya na elimu.

Mwanzoni taasisi za dini ziligoma kwa kuhofia Serikali kuja kutaifisha tena, madhehebu ya dini yalikubali pale Serikali ilipokubali kuwekeana mkataba wa kutotaifisha tena.

Mwalimu kwa nia njema aliamini Serikali inaweza kufanya kila kitu, madhara ya kudhani Serikali itafanya kila kitu na kutowekeza kwenye ujenzi wa sekta binafsi zenye nguvu na kutengeneza matajiri wako wa ndani wenye uwezo wa kusaidia kushika njia kuu za uchumi na hata kuingia nazo ubia katika kuendesha uchumi yalionekana pale nchi ilipolazimishwa kutekeleza masharti ya SAPs ya Benki ya Dunia na IMF.

Serikali iliambiwa ijiondoshe kwenye kufanya biashara, bahati mbaya hakukuwa na sera wala mpango wa kuwa na sekta binafsi zenye nguvu, hatukuwa na matajiri wa ndani, matokeo yake baada ya Serikali kushindwa kuendesha viwanda, mashirika na maduka yake, haikuwa na wa kumpa viwanda vyake, matokeo yake viwanda vikafa vyote, toka ndege karibu 14 mwishoni mwa miaka ya 70 mpaka ndege sifuri, leo ndiyo Serikali inanunua ndege!
Kama kweli tuna nia thabiti ya kuleta maendeleo endelevu nchini, Serikali yetu lazima iweke nguvu kubwa katika kutengeneza sekta binafsi zenye nguvu, kutengeneza matajiri wa ndani wenye uwezo wa kuingia ubia na Serikali katika kuendesha uchumi wa nchi.

Nimeona mpango wa bajeti ya mwaka 2017/2018, sioni nia ya Serikali kufanya kazi na sekta binafsi, tujifunze kutokana na makosa ya nyuma, sekta binafsi ni kiungo muhimu kwenye kusukuma mbele maendeleo ya nchi.
Tutengeneze matajiri wetu wa ndani, tutengeneze sekta binafsi yenye nguvu, tukumbuke hata hizi ndege za Bombardier hazitengenezwi ya kiwanda cha Serikali huko tunakonunua, ni sekta binafsi.

Tuimarishe sera ya ubia ya mwaka 2009 na sheria yake itakayosimamia mfumo wa uchumi wa PPP. Bila sekta binafsi imara, matajiri wa ndani, sera na sheria bora zitakazosimamia na kuwalinda walaji, hatutaweza kuwa na maendeleo endelevu. Ndiyo lilikuwa moja ya makosa ya Serikali ya Awamu ya Kwanza.

Mwandishi ni Mwanahabari na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino Jijini Mwanza. Aliandika uchambuzi wake huu kupitia ukurasa wa Facebook.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles