27.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

NYANZA KUWA ‘TAIFA’ JIPYA AFRIKA MASHARIKI?

NAIROBI, KENYA

MADAI yaliyopata kuzungumzwa kuhusu kujitenga kwa baadhi ya maeneo nchini Kenya yameanza kuibuliwa upya na baadhi ya viongozi wa taifa hilo.

Mambo hayo yalianza kujitokeza baada ya uchaguzi wa Oktoba 26, mwaka huu, ambao uligomewa na Kiongozi na Mgombea wa Muungano wa Upinzani NASA, Raila Odinga.

Hivi karibuni Mkuu wa Mkoa wa Mombasa, Hassan Joho, amesikika akiongea wakati akiongoza mkutano kuhusu namna ya kupiga kura ya kujitenga kwa Pwani ya Kenya, akielezea jinsi ambavyo eneo hilo limekuwa likitengwa kihistoria. Hata hivyo, ombi hilo lilikataliwa na chama tawala (Jubilee) pamoja na Jumuiya ya Kimataifa.

Joho alitoa hoja hiyo akiwa na Amason Kingi wa Kilifi na wawakilishi 15 waliochaguliwa kuhudhuria mkutano huo.

Viongozi hao wanashutumu visa vya kuchukuliwa ardhi ya eneo hilo na Wakenya kutoka mikoa mingine, ukosefu wa uwakilishi katika serikali ya kitaifa na kutengwa kiuchumi. Madai haya si mapya.

Pwani ya Kenya ina kundi linalodai uhuru wa eneo hilo, Mombasa Republican Council (MRC), tangu mwaka 1999, ambalo kulingana na madai yake eneo hilo, lilikuwa sehemu ya zamani ya Pwani iliyokuwa chini ya miliki ya uongozi wa Sultan wa Zanzibar.

Mkutano huo ulionekana kupambana na Serikali ya Rais Uhuru Kenyatta. Wakuu wa Mikoa ya Pwani kutoka upande wa chama tawala hawakushiriki mkutano huo.

Kwa upande wake, Waziri wa Utalii, Najib Balala, ambaye ni mwenyeji wa eneo hilo,  amelaani hotuba hatari zinazotolewa juu ya kujitenga kwa pwani ya Kenya.

Aidha, mjadala huo umewashtua mabalozi wengi wa Ulaya, ambao walikwenda Mombasa mwishoni mwa juma lililopita kwa madhumuni ya kuonyesha wazi kwamba, Ulaya inafanya kazi na Kenya yenye umoja, na kwamba mradi wako sawa kiuchumi.

Naye Katibu Mkuu wa MRC, Randu Nzai, aliwapongeza viongozi walioamua kufuata nyayo zao za kutaka Pwani ijitenge, akisema kuwa, MRC itawaunga mkono na kushirikiana nao.

Akinukuliwa na gazeti moja nchini humo, Nzai alikiri akisema kuwa, watashirikiana na viongozi hao, hasa Gavana wa Mombasa, Ali Hassan Joho na mwenzake wa Kilifi, Amason Jefa Kingi, kutimiza ndoto ya Wapwani.

“Tulipoanzisha safari ya kutaka kujitenga, wenzetu walitupinga, lakini kwa vile wao ni ndugu zetu na wamegundua kuwa mpwani anateseka, tunawakaribisha tuendeleze ajenda hii pamoja,” amesema Nzai.

Agosti 22, mwaka huu, mshauri wa kiuchumi wa NASA, David Ndii, aliibua mjadala mzito baada ya kusema katika mahojiano na Kituo cha Televisheni cha NTV katika kipindi chake cha “Decesion2017” kuwa wakati umewadia kwa sehemu nyingine za Kenya kujitenga.

Mwanasheria Mkuu wa Kenya, Githu Muigai, wakati huo, alikemea vikali maoni hayo, akisema yataligawa taifa hata zaidi ya misingi ya kikabila.

Ndii alitoa pendekezo hilo kwa kusema: “Korti haiwezi kutoa suluhu la kisiasa… michakato yote ya kisiasa iliyopatikana tangu uhuru imepatikana kupitia nguvu… wengi wetu hatuna haja na nafasi za kisiasa, lakini ni kwa ajili ya kuifanya Kenya mahala pazuri.”

Aliongeza: “Tumekuwa tukiitisha maandamano tangu mwaka 1990, na hatutakoma… Tutaitisha maandamano, ndiyo tutaitisha maandamano. Hatutaishi katika siasa za udikteta. Tuko katika Mahakama Kuu ili tu kuuonyesha ulimwengu kilichofanyika wakati wa uchaguzi,” alisema.

MGAWANYO WA KENYA MBILI

Kwa mujibu wa Ndii, ambaye alipendekeza kugawanywa nchi hiyo na kuunda mataifa mawili, amepata kusema kuwa, taifa jipya litakuwa na majimbo yake kamili.

Sehemu ya kwanza aliita kuwa ni Central Republic of Kenya na ya pili itaitwa People’s Republic of Kenya.

Ndii alisema mgawanyo wa maeneo hayo na mipaka ni kama ifuatavyo; Magharibi ya Kenya; ukanda huu utaundwa na maeneo ya Luo, Luhya, Teso, Kisii, na Kurial. Pwani ya Kenya; itakuwa na maeneo ya Swahili, Mijikenda, Pokomos, Giriamas, Taifa, na Taveta. North West Kenya itaundwa na maeneo ya Turkana na Pokot.

Kukamilisha hatua hiyo, wanatarajia kufungua shauri au madai katika Tume ya Haki za Binadamu ya Afrika (African Commission on Human and People’s Right) yenye makao yake mjini Banjul, nchini Gambia.

Sababu kubwa inayotajwa ni kutokana na maelezo kwamba, kulingana na Tume hiyo, wananchi wanao uhuru kulinda haki zao za kujitawala pamoja na kuanzisha taifa lao bila vikwazo vyovyote.

Wafuasi wanaotaka Kenya igawanywe wanaegemea katika Ibara ya 10 ya Mkataba wa Banjul (Banjul Charter), kwa tafsiri isiyo rasmi ya Kiswahili, inasema: “Watu wote watakuwa na haki ya kuishi na kutawala, watakuwa huru kuamua mwelekeo wao wa hadhi ya kisiasa na watakuwa huru kutekeleza sera zao za uchumi na maendeleo ya jamii kwa mujibu wa kanuni na taratibu walizozichagua kwa uhuru wao”.

‘JAMHURI YA NYANZA’

Katiba Mpya ya Kenya ya mwaka 2007 ililifanya Jimbo la Nyanza kujumuisha wilaya zifuatazo; Bondo, Borabu, Gucha, Homa Bay, Kisii, Kisumu Mashariki, Kisumu Magharibi, Kuria Magharibi, Kuria Mashariki, Manga, Masaba, Migori, Nyamira, Nyando, Rachuonyo, Rarieda, Rongo na Siaya.

Nyanza ni jiji la tatu kwa ukubwa nchini Kenya. Kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2009, lina jumla ya watu 5,442,711.

Jimbo hilo limewahi kutoa wasomi, wanasiasa na magwiji katika fani mbalimbali. Miongoni mwao ni Tom Mboya, Barack Obama Sr., Jaramogi Oginga Odinga, Raila Odinga, Betwell Allan Ogot, Achieng Oneko, Chrispine Otwal, Robert Ouko na James Joshua Nyamon. Umaarufu wa watu wanaotoka eneo hili umechangia safari ya Raila Odinga na wafuasi wake kueneza kampeni ya ‘kujitenga’. Je, jaribio hilo litafanikiwa au serikali mpya itajumuisha vyama vyote?

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles