NYALANDU ATOA SABABU SITA ZA KUONDOKA CCM

0
41

Na WAANDISHI WETU-DAR/ARUSHA

MBUNGE wa Singida Kaskazini, Lazaro Nyalandu, ametoa sababu sita za kuamua kujivua uanachama wa CCM na nafasi zote alizokuwa akizishikilia ndani ya chama.

Wakati Nyalandu akitoa sababu hizo, CCM Arusha wamesema kada huyo ameondoka kwa sababu ya kukosa uwaziri mkuu, waliodai kuwa alikuwa akiuota na kwamba ameenda Chadema ili awanie urais 2020.

Kwa upande wao, Chadema wamesema kuondoka kwa Nyalandu ndani ya CCM, ni mwanzo wa kung’oka kwa vigogo wasioridhishwa na siasa za chama tawala.

 Maelezo ya Nyalandu

Nyalandu ambaye amekuwa mbunge wa Singida Kaskazini tangu mwaka 2000, jana akiwa mkoani Arusha alitangaza kujitoa katuika chama hicho.

“Nimechukua uamuzi huu kutokana na kutoridhishwa kwangu na mwenendo wa hali ya kisiasa nchini, ikiwa ni pamoja na ukiukwaji wa haki za kibinadamu, ongezeko la vitendo vya dhuluma wanavyofanyiwa baadhi ya Watanzania wenzetu.

“Pia kutokuwepo kwa mipaka ya wazi kati ya mihimili ya dola (Serikali, Bunge na Mahakama), kunakofanya utendaji kazi wa kibunge wa kutunga sheria na wa kuisimamia Serikali kutokuwa na uhuru ulioainishwa na kuwekwa bayana kikatiba.”

Nyalandu, ambaye alikuwa Waziri wa Maliasili na Utalii katika Serikali ya Awamu ya Nne, alisema anaamini kwamba bila Tanzania kupata Katiba mpya sasa, hakuna namna yoyote ya kuifanya mihimili ya dola isiingiliane na kuwapo kwa ukomo wa wazi.

“Naamini kwamba bila Tanzania kupata Katiba mpya sasa, hakuna namna yoyote ya kuifanya mihimili ya dola isiingiliane na kuwepo kwa ukomo wa wazi na kujitegemea kwa dhahiri kwa mihimili ya Serikali, Bunge na mahakama ambayo ndio chimbuko la uongozi bora wa nchi, na kuonyesha kwa uwazi kuwa madaraka yote yatokana na wananchi wenyewe, na kwamba Serikali ni ya watu kwa ajili ya watu.

“Mimi naondoka na kukiacha CCM, nikiwa nimekitumikia kuanzia ngazi ya uenyekiti wa UVCCM mkoa, ujumbe wa kamati za siasa wilaya na mkoa, ujumbe wa kamati ya wabunge wote wa CCM na mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa.

“Nimejiridhisha kuwa kwa mwenendo wa hali ya kisiasa, kiuongozi na kiuchumi uliyopo Tanzania sasa, CCM imepoteza mwelekeo wake wa kuisimamia Serikali kama ilivyokuwa hapo awali.

“Naamini kuwa kama ilivyotokea kwa mihimili ya Bunge na Mahakama kutokuwa na uhuru kamili, bila kuingiliwa kiutendaji kwa namna moja au nyingine, CCM nayo imekuwa chini ya miguu ya dola badala ya chama kushika hatamu na kuikosoa Serikali inapobidi kama yalivyokuwa maono ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

“Hivyo basi, kwa dhamira yangu na kwa uamuzi wangu mwenyewe, nikiwa na haki ya kikatiba, natangaza kukihama CCM leo hii na nitaomba ikiwapendeza wanachama wa Chadema, basi waniruhusu kuingia mlangoni mwao, niwe mwanachama, ili kuungana na Chadema na Watanzania wote wanaopenda kuleta mabadiliko ya kisiasa na kiuchumi nchini kupitia mfumo wa kidemokrasia na uhuru wa mawazo.

“Vilevile, nimemua kujiuzulu kiti cha ubunge, Jimbo la Singida Kaskazini kuruhusu kufanyika kwa uchaguzi mwingine ili wananchi wapate fursa ya kuchagua itikadi wanayoona inawafaa kwa majira na nyakati hizi zenye changamoto lukuki nchini Tanzania.

“Ni imani yangu, kamwe hayatakuwa ya bure maneno haya, wala uamuzi huu niufanyao mbele ya Watanzania leo ili kwamba sote kama taifa tuingie kwenye mjadala wa kuijenga upya misingi ya nchi yetu.

“Ni maombi yangu kwa Mungu kuwa haki itamalaki Tanzania. Upendo, amani na mshikamano wa watu wa imani zote za dini, mitazamo yote ya kiitikadi za kisiasa na makabila yote nchini uimarike.

“Tushindane kisera na kuruhusu tofauti za mawazo, lakini tubaki kama ndugu na taifa lililo imara na nchi yenye maadili,” alisema Nyalandu.

Nyalandu pia alisema amemwandikia barua Spika wa Bunge, Job Ndugai, juu ya kujiuzulu nafasi yake ya ubunge wa Singida Kaskazini aliyoishika tangu mwaka 2000.

Hata hivyo, Katibu wa Bunge, Stephen Kagaigai, alisema hana taarifa za kujiuzulu kwa Nyalandu.

“Amejiuzulu kweli? Kwanini? Sina taarifa, Ofisi ya Bunge wala ya Spika haijapata barua yoyote kutoka kwake, kwa hiyo siwezi kulizungumzia zaidi maana taarifa sina,” alisema.

 Uamuzi wa Nyalandu wapokewa kwa hisia tofauti                          

Wakati Nyalandu akisema hayo, Katibu Mwenezi wa CCM Mkoa wa Arusha, Shabani Mdoe, alisema uamuzi aliochukua wa kujiuzulu nafasi zote ndani ya CCM, ni matokeo ya kisirani na kununa baada ya kukosa cheo cha uwaziri mkuu alichokuwa akiota kupewa.

“Hayo ni matokeo ya hasira na kununa baada ya kuukosa uwaziri mkuu na hata nafasi ya uwaziri, ni mtu mjanja mjanja anayefukuzia vyeo, sisi tunazo habari hata huko Chadema anakokwenda anataka nafasi ya kugombea urais mwaka 2020, ni sawa na fisi anayesubiri mkono kuanguka, hana chochote isipokuwa tamaa ya madaraka,” alisema Mdoe.

Kwa upande wake, aliyekuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Vijana wa CCM Mkoa wa Arusha na Diwani wa Kata ya Sambasha wilayani Arumeru, Lengai ole Sabaya, alisema hatua aliyochukua Nyalandu imechelewa na kwamba alitakiwa kufukuzwa.

“Uamuzi wake umechelewa mno, alipaswa kufukuzwa uanachama siku nyingi, anajua madhambi yake ndiyo kisa cha kujihami. Najua hatakuwa peke yake, wapo wengi ambao kwa sasa CCM chini ya Mwenyekiti wetu Rais Dk. John Magufuli si mahali salama kwao,” alisema.

Sabaya alikwenda mbali zaidi kwa kumhusisha Nyalandu na uozo mwingi ambao ulifanyika katika Wizara ya Maliasili na Utalii katika kipindi ambacho alikuwa waziri.

“Alikuwa na madhaifu yake kwenye Wizara ya Maliasili na Utalii, ni kati ya wapiga dili ambao baada ya kugundua uchafu wake utafukuliwa muda mfupi ujao, ameamua kukimbia, lakini kama wanasiasa tunamtakia kila la heri kule anakokwenda,” alisema Sabaya.

Naye Meya wa Jiji la Arusha, Kalisti Lazaro (Chadema), alisema kujiuzulu kwa mwanasiasa huyo ni mwanzo wa kujiuzulu kwa idadi kubwa ya viongozi wasioridhishwa na hali ya kisiasa inayoendelea nchini.

“Kwanza nampongeza kwa kujitambua na kuchukua uamuzi wa kuhama kutoka chama ambacho hivi sasa hakifanyi siasa tena. CCM ni chama dola, hakuna mtu hasa mwanasiasa makini anayependa siasa safi ataendelea kubakia CCM.

“Uamuzi wake ni wa hiari, ni utashi wake, hajalazimishwa na mtu yeyote, na sisi kama chama cha demokrasia, chama kinachoendesha siasa za kistaarabu na shirikishi tunamuunga mkono,” alisema.

Akizungumzia wito wa Nyalandu kutaka kujiunga na Chadema, Kalisti alisema suala la kumpokea litafanyika haraka na kazi hiyo itafanywa na viongozi wa juu wa chama.

“Itakuwa jambo la ajabu sana kutompokea mwanasiasa wa kariba na haiba ya Nyalandu, tutampokea kwa mikono miwili na ni matumaini yangu Mwenyekiti wetu wa taifa, Freeman Mbowe, amesikia wito wa kumfungulia milango,” alisema.

Aidha meya huyo ambaye pia ni kiongozi wa Chadema ngazi ya mkoa, alipiga kijembe washindani wao kisiasa kuwa baada ya wao kuwachukua madiwani toka Chadema, chama chake kimejibu mapigo kwa kumchukua mbunge.

“CCM wao wanahangaika na madiwani, sisi tunachukua viongozi wa hadhi ya Nyalandu na si yeye peke yake, wapo wengi wanaotaka kujiunga nasi, ni suala la muda tu, watakuja wengi,” alisema Lazaro.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here