27.5 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

NYALANDU AITAKA KATIBA YA WARIOBA

Na NORA DAMIAN-DAR ES SALAAM


MBUNGE wa Singida Kaskazini, Lazaro Nyalandu (CCM), amesema anakusudia kuwasilisha muswada binafsi bungeni utakaoweka sharti la kurejewa mjadala wa Katiba Mpya.

Akizungumza na MTANZANIA jana, alisema muswada huo atauwasilisha katika kikao cha tisa cha Bunge kinachotarajiwa kuanza Novemba 7  mwaka huu mjini Dodoma.

Alisema Katiba ya nchi ni mkataba wa wananchi ambao utadumu kwa miaka mingi hivyo hautakiwi kufanywa kama dharura au kuogopwa bali unahitaji umakini.

“Mchakato ulianza ukatumia fedha nyingi na kuhusisha watu wengi lakini haukukamilika, na hapa katikati ulighubikwa na sintofahamu nyingi.

“Na kwa namna yoyote ile ili tuweze kuwa na Katiba bora itakayohusisha wadau wote kwa maana ya wananchi, viongozi wa vyama vya siasa na upande wa serikali itakuwa ni muhimu mchakato uanze kwa kuzingatia rasimu ya katiba kama ilivyowasilishwa na Tume ya Jaji Warioba,” alisema Nyalandu.

Alisema anatarajia kuwa wabunge wa chama chake na wabunge wa upinzani watamuunga mkono   hoja hiyo iweze kurudi upya na wadau wote wapate fursa ya kujadili ipatikane Katiba Mpya.

“Wabunge tuna nafasi yetu ya kujadili na kupeleka maoni ya binafsi na yale ya pamoja.

“Katiba imempa nafasi mbunge mmoja mmoja bila kujali ametoka chama gani, hivyo mimi naona ni hoja ambayo ni lazima ipate nafasi kama hoja nyingine na kufanyiwa kazi.

MATOKEO YA TWAWEZA

Wakati huohuo, Taasisi ya Twaweza jana ilitangaza matokeo ya utafiti ambayo yanaonyesha Watanzania wawili kati ya watatu wanahitaji Katiba Mpya.

Utafiti huo uliopewa jina la ‘Zege Imelala’ ulilenga kupata maoni ya wananchi kuhusu kukwama kwa mchakato wa kuunda Katiba Mpya.

Akitangaza matokeo hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa Twaweza, Aidan Eyakuze, alisema ulifanyika kati ya Juni hadi Julai mwaka huu na kuhusisha watu 1,745 kutoka maeneo mbalimbali ya Tanzania Bara.

“Asilimia 67 ya Watanzania wanasema ni muhimu kwa Tanzania kupata katiba mpya na nusu ya wananchi wanasema mchakato wa katiba uanze upya na tume mpya,” alisema Eyakuze.

Kulingana na utafiti huo, asilimia 49 ya wananchi wanafahamu juu ya mchakato wa kukusanya maoni uliofanywa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyoongozwa na Jaji Warioba na asilimia 21 wanafahamu kuwa vipengele vya rasimu ya Warioba viliondolewa na Bunge Maalumu la Katiba kupitia Katiba Inayopendekezwa.

“Wananchi hawakubaliani na mabadiliko mengi yaliyofanywa na BMK chini ya Mwenyekiti wa Kamati ya Uandishi wa Katiba Mpya, Andrew Chenge,” alisema.

POLEPOLE

Akizungumza baada ya kutangazwa   matokeo hayo, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Humphrey Polepole, alikiri kuwa inahitajika Katiba Mpya lakini kwa sasa wameamua kushughulikia kwanza   shida za wananchi.

“CCM inaamini katika utafiti kama nyenzo ya kutuarifu juu ya yale tunayoyatenda. Hata mimi na serikali ya CCM inataka Katiba, lakini kwa sasa tumeamua kushughulika na shida za watu suala la katiba litakuja baadaye.

“Tuna miaka mitano kupanga ni kuchagua, mageuzi ya katiba yatafanyika pale ambapo tumefanikiwa kufanya mageuzi ya taasisi za siasa, jamii  na serikali…itaandikwa pale ambako nidhamu ya viongozi na watumishi itakuwa imenyooka,” alisema Polepole.

Alisema yeye alikuwa miongoni mwa wajumbe wa BMK lakini walikwama kwa sababu kulikuwa na masilahi binafsi ya viongozi wa vyama vyote ambao walishindwa kuwa na uelewa wa pamoja juu ya nini Watanzania wanataka na  muafaka na maridhiano pia havikuwapo.

ACT WAZALENDO

Katibu wa Itkiadi na Uenezi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Ado Shaibu, alisema katiba mpya bado ni kipaumbele cha Watanzania na kuinyoosha nchi bila katiba ni kazi bure.

ASASI ZA KIRAIA

Mwakilishi wa Asasi za Raia, Deogratias Bwire, alimtaka Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi kumshauri Rais Dk. John Magufuli aupe kipaumbele mchakato wa Katiba Mpya.

“Serikali inafanya mambo mengi mazuri kama vile ya kulinda rasilimali za nchi je, haya yote yanalindwa kwenye nyaraka gani.

“Tunapotaka kunyanyua maisha ya mtu mnyonge halafu mwisho wa siku hakuna sehemu anapoweza kwenda kuidai haki yake tunakuwa tunamdanganya,” alisema Bwire.

CHADEMA

Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Maendeleo na Demokrasia (Chadema), Profesa Mwesiga Baregu, aliishauri Serikali isikilize maoni ya wananchi.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles