NYALANDU AIBUA MKANGANYIKO

0
19

Na Mwandishi Wetu

Siku moja baada ya Mbunge wa Singida Kaskazini, Lazaro Nyalandu kutangaza kujiuzulu ubunge Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimemwandikia barua Spika wa Bunge, Job Ndugai kuwa mbunge huyo amepoteza sifa za uanachama wa chama hicho.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Spika wa Bunge, barua ambayo Nyalandu alisema amemwandikia Spika haijamfikia na badala yake siku hiyo Oktoba 30, alipokea barua kutoka kwa Katibu Mkuu wa CCM ikimjulisha kuwa Nyalandu amepoteza sifa za uanachama wa chama hicho na hivyo kupoteza nafasi zote za uongozi wa ndani wa chama hicho na ubunge kwa mujibu wa Ibara ya 13 ya chama hicho.

Barua hiyo imemnasibu Nyalandu kuwa kwa muda chama hicho kilishaanza kumchukulia hatua za kiudhibiti na kinidhamu dhidi ya vitendo na kauli zake zisizoridhisha kinyume na misingi, falsafa na itikadi ya CCM.

“Ofisi ya Spika ingependa kuwaarifu Watanzania wote kwamba mpaka sasa haijapokea barua toka kwa aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Singida Kaskazini, ambayo amekuwa akiarifu kwamba amemwandikia Mheshimiwa Spika kumtaarifu kujiuzulu kwake.

“Kutokana na barua hiyo ya CCM ambayo ni mamlaka halali ndani ya CCM, ambacho Nyalandu alipata ubunge kupitia chama hicho na kwa mujibu wa Ibara ya 71 (1)(f) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayotamka kwamba, Mbunge atakoma kuwa Mbunge na ataacha kiti chake cha ubunge iwapo litokeapo lolote kati ya mambo yafuatayo: (f) Iwapo mbunge ataacha kuwa mwanachama wa chama alichokuwamo wakati alipochaguliwa au alipoteuliwa kuwa mbunge.”

“Hivyo, Ndugu Lazaro Nyalandu si Mbunge tena na hatua stahiki za kuiarifu Tume ya Taifa ya Uchaguzi zinaendelea kuchukuliwa,” imesema taarifa hiyo.

Nyalandu alitangaza kujiuzulu nyadhifa zake zote ndani ya chama hicho pamija na ubunge kwa madai kuwa amechoshwa na mwenendo wa kisiasa nchi ambapo aliomba kujiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here