28.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 16, 2024

Contact us: [email protected]

Nyakati ngumu zinaweza kukufanya ufanikiwe

Na CHRISTINA BWAYA

MAISHA wakati mwingine hutupitisha kwenye nyakati ngumu. Tunapopita kwenye vipindi vigumu vinavyokatisha tamaa na kutuumiza, tunajiuliza maswali mengi yasiyo na majibu. Tunajiuliza imekuwaje Mungu mwenye upendo aruhusu tupatwe na magumu kiasi hiki? Kama hujawahi kufika mahali ukajiuliza maswali kama haya, pengine huwezi kuelewa.

Hufika kipindi kila kitu kinakuwa kama hakiendi. Unajikuta mahali unahisi giza nene linakuandama. Unaangalia pande zote ukitegemea msaada lakini huoni dalili. Kila uliyefikiri atakusaidia, ndiye kwanza anashangaa kwa nini unafikiri yeye ndiye anayeweza kukusaidia.

Inawezekana unajitahidi kusoma makala haya lakini unajua kabisa umekata tamaa. Pengine ndio kwanza umetoka kupokea barua ya kuachishwa kazi. Hukuwa na hili wala lile, ghafla, giza la kukosa kazi limekukabili. 

Pengine ndio kwanza umepokea habari mbaya. Labda ni kuachwa na mpenzi wako, kufeli mtihani au kuondokewa na mtu wa karibu uliyempenda na mambo kama hayo. Katika nyakati ngumu kama hizi maisha hubeba sura tofauti. Furaha na matumaini vyote huyeyuka.

Hata hivyo, pamoja na ukweli kuwa hatupendi kupatwa na magumu, ukweli ni kwamba hatuwezi kuzikwepa. Nyakati ngumu ni sehemu kamili ya maisha yetu binadamu. Fikiria misimu mbalimbali katika mwaka. Kuna msimu wa masika ambapo mvua hunyesha, lakini pia baada ya muda huja majira ya kiangazi wa jua kuwaka. Pamoja na ugumu wake, bado kiangazi nacho kina nafasi yake katika mwaka kama ambavyo magumu nayo yana nafasi yake katika maisha.

Kuna kisa kimoja katika Biblia ningependa ukitafakari. Tunasoma habari za Yusufu kijana wa mzee aliyeitwa Yakobo aliyekuwa na watoto wapatao 12. Yusufu tofauti na ndugu zake wengine alikuwa na ndoto nyingi za kimaisha. Mbali na ndoto zake hizo, alikuwa kipenzi cha baba yake. Upendo huo mkubwa wa baba ulimlinda na maisha ya suluba waliyoyaishi kaka zake. Hali hiyo ya upendeleo ilichochea uadui mkubwa kati yake na ndugu zake. Ingawa ndugu zake hawakumpenda, lakini baba yake alifanya kila linalowezekana kuhakikisha Yusufu anaishi maisha ya furaha. Yusufu alizoea maisha yenye furaha ya kupendwa na mzee wake. 

Ghafla, Yusufu aliyezoea furaha na mapenzi ya baba, anajikuta shimoni. Ndugu zake mwenyewe wanataka kumuua. Hata hivyo, kwa jitihada binafsi za kaka yake mkubwa, Rubeni, Yusufu anajikuta mikononi mwa wafanyabiashara wa Misri kama bidhaa. Ndugu zake mwenyewe wanaamua kumuuza ili kujilipa kisasi. Huenda aliomboleza njia nzima akipelekwa Misri asiamini imekuwaje maisha yageuke giza nene kiasi hicho.

Katika maisha wakati mwingine mambo hubadilika ghafla. Ulienda kazini ukitokea kwenye nyumba yako, mathalani, ghafla unarudi nyumbani unakutana na ‘tingatinga’ linafanya kazi yake. Huna tena mahali pa kuishi. Uliishi na wazazi wako waliokupenda, ghafla unaambiwa mzazi wako amefariki dunia. Hali kama hizi huyafanya maisha yetu yawe mithili ya giza nene kama ilivyokuwa kwa Yusufu.

Kitu ambacho mara nyingi huwa hatupati muda wa kukitafakari tunapokutwa na majanga kama haya ni namna gani mambo kama haya magumu yanavyoweza kutuandaa na kutufanya imara kwa ajili ya mafanikio yaliyo mbele yetu. Kama ilivyokwetu leo hii, Yusufu pengine alijihurumia kuona anatengwa na familia yake. Kwa hali ya kawaida, Yusufu angependa kuendelea kuishi maisha ya furaha akiwa na familia yake pale kijijini kwao. Kitu ambacho hakuwa amekijua ni kwamba ili afikie ndoto alizokuwa nazo, ilibidi kwanza apite kwenye tanuru.

Tanuru la kuchukiwa na ndugu zake wa karibu, kutupwa shimoni na baadae kuuzwa kama bidhaa. Tanuru la kutengwa na familia yake, kusingiziwa mabaya na kujikuta gerezani hali akijua hana hatia. Mambo haya magumu yalikuwa yakimwandaa kuwa mtu mkubwa mbeleni. Bila kuteseka gerezani, Yusufu asingekutana na wasaidizi wa mkuu wa nchi. Bila kusingiziwa uongo ulimfanya afungwe, uwezo wake wa kutafsiri ndoto za watu usingefahamika na hivyo asingekaa akutane na mkuu wa nchi.

Nyakati ngumu katika maisha hutuandaa kwa mambo mazuri mbeleni. Unaweza usielewe kwa nini unaandamwa na matatizo uliyonayo, lakini jifunze jambo kwa Yusufu. Magumu tunayokutana nayo ni mtaji wa mafanikio mbeleni.  Unaweza kusikitika kukosa kazi leo, kwa sababu huelewi kwamba ili upate kazi unayoipenda lazima uondoke mahali. Unaweza kusikitika kuachwa na mchumba umpendaye leo, lakini usichoelewa ni kwamba ili ukutane na mtu sahihi mtakayeishi kwa furaha, lazima kwanza uachwe na huyu asiye sahihi. Acha kujihurumia kwa sababu hali uliyonayo, pamoja na ugumu wake, ni ya muda tu. 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles