30.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

NMB yakabidhi milioni 900/- za madawati

Ofisa Mkuu wa Fedha wa Benki ya NMB, Waziri Barnabas (kushoto), akimkabidhi Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tamisemi, George Simbachawene, mfano wa hundi ya sh. milioni 900 kwa ajili ya kusaidia madawati  ya shule mjini Dodoma juzi.
Ofisa Mkuu wa Fedha wa Benki ya NMB, Waziri Barnabas (kushoto), akimkabidhi Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tamisemi, George Simbachawene, mfano wa hundi ya sh. milioni 900 kwa ajili ya kusaidia madawati ya shule mjini Dodoma juzi.

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

BENKI ya NMB imekabidhi hundi ya Sh milioni 900 kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Tamisemi), George Simbachawene, ili kuunga mkono hatua ya Rais Dk. John Magufuli, kuhakikisha madawati yanapatikana kwa wakati.

Hatua hiyo ni moja ya utekelezaji wa benki hiyo katika kusaidia miradi mbalimbali ya maendeleo ya jamii  kupitia kitengo cha huduma kwa jamii ambapo hutenga takribani asilimia moja ya faida yake baada ya kodi kwa miradi ya kijamii.

Akizungumza wakati wa kukabidhi hundi hiyo, Ofisa Mkuu wa Fedha wa Benki ya NMB, Waziri Barnabas, alisema sera ya NMB kuhusu uwajibikaji kwa jamii hulenga katika utoaji wa misaada hususani kwenye sekta ya elimu kwa shule za msingi na sekondari ili kuiongezea Serikali nguvu katika juhudi za kutatua changamoto ya upungufu wa madawati shuleni.

“Ili kupunguza uhaba wa madawati shuleni kama njia ya kuchangia kuimarisha miundombinu, NMB imekuwa mstari wa mbele katika kusaidia shule za Serikali kwa kuwapatia madawati.

“Kufikia  Juni mwaka huu, zaidi ya Sh milioni 600 zimetumika kununua madawati zaidi ya 6,000 kwa shule za msingi na sekondari nchi nzima. Hii ikiwa ni sehemu tu ya ahadi yetu ya Sh bilioni 1.5 ambayo ni asilimia moja ya faida tuliyopata mwaka 2015 ambayo ilikuwa shilingi bilioni 150.2,” alisema Barnabas.

Alisema mwaka 2015, nje ya asilimia moja tunayoitoa kusaidia jamii kama sera inavyosema, tuliweka ahadi ya kusaidia kutatua changamoto ya madawati shuleni na kuahidi kununua madawati 15,000 yenye thamani ya Sh bilioni 1.5 tuliyoweka kusaidia tatizo la madawati nchini kwa miaka mitano.

Pamoja na hali hiyo, alisema kuwa kutokana na sera ya elimu bure, kumekuwa na  ongezeko la wanafunzi shuleni na kusababisha uhitaji mkubwa wa madawati  ambapo benki imeamua kukabidhi  hundi ya Sh milioni 900 ikiwa ni katika kuendeleza ahadi ya kusaidia upungufu wa madawati katika  shule za msingi na sekondari nchi nzima.

Alisema benki hiyo inajivunia kwa kuwa na mtandao mkubwa nchini ambapo ina matawi zaidi ya 177 nchi nzima yanayohudumia wateja zaidi ya milioni mbili pamoja na mashine za ATM 600.

Barnabas alisema kuwa benki hiyo inaendelea kuboresha mahusiano mazuri yaliyopo baina ya benki na Serikali kwa ujumla.

“Ni kweli NMB imekuwa ikishirikiana na  Serikali katika utekelezaji wa mahitaji ya kisera. Kwa sasa NMB inatoa misaada kusaidia ujenzi wa maabara za kisayansi na utoaji wa vitabu kwa shule za msingi na sekondari. Pia NMB inaungana na Serikali katika  kuboresha maarifa ya Tehama kwa kutoa kompyuta kwenye shule zenye umeme,” alisema.

Kwa upande wake Waziri Simbachawene, alipongeza hatua ya benki hiyo kwa kuunga mkono juhudi za Serikali katika kukabiliana na changamoto ya upungufu wa madawati kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari nchini.

“Tunaipongeza Benki ya NMB kuwa moja katika ya taasisi za fedha zilizounga mkono mpango huu wa Serikali kwa vitendo na kwa hakika hata taasisi nyingine zitaiga mfano huu,” alisema Simbachawene.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles