24.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 16, 2024

Contact us: [email protected]

NKAMIA AMETUKUMBUSHA GHARAMA ZA DEMOKRASIA

NA MARKUS MPANGALA


MBUNGE wa Chemba, Juma Nkamia amekuja na jambo jipya katika ulimwengu wa kisiasa. Juma Nkamia ameleta hoja mezani kwa Spika wa Bunge, Job Ndugai ya kuomba kuwasilisha Muswada binafsi wa Mabadiliko ya Sheria ya ukomo wa nafasi ya ubunge kutoka miaka mitano kwenda miaka saba.

Nkamia anaona muda wa ubunge wa miaka mitano hautoshi, kwahiyo ingefaa kufanyiwa mabadiliko ya sheria na Bunge ili litamke kuwa muda wa ubunge utakuwa miaka saba.

Jambo hilo limekuwa likidodoswa mara kadhaa tangu miaka ya nyuma. Lakini kitu kimoja kilichokwamisha ni kutoyumba kwa misingi ya nchi juu ya ukomo wa nafasi ya urais au ubunge.

Nakumbuka Mwalimu Nyerere aliwahi kuonya juu ya hatua za aina hiyo hata kama tutajidanganya kuwa Nyerere sio msahafu. Kwenye kitabu chake cha “Uongozi Wetu na Hatima ya Nchi yetu,” Mwalimu Nyerere anaandika, “Rais alieleza kuwa walikuwa wamekubaliana kwamba vipindi vya kuwa Rais ni lazima vitamkwe, lakini walikuwa hawajaafiki uamuzi viwe vipindi vingapi. Awali baadhi ya viongozi wa chama walikuwa wameanza kampeni za kutaka Rais Mwinyi aongezewe vipindi vya muda wa kuwa Rais,”

“Nilipotambua hivyo nilikuwa nimekwenda mara moja kwa Rais na kumsihi azizime kampeni hizo; na viongozi wahusika nilitafuta nafasi nao nikawaomba wasilifufue jambo hili. Nikadhani tumeelewana hivyo. Kwa hiyo nilistuka niliposikia kuwa kumbe suala hilo la vipindi vya urais bado linazungumzwa, na ati bado uamuzi wa vipindi vingapi haujafikiwa!”(Uk.9).

Katika kitabu hicho hicho, Mwalimu Nyerere anaeleza  tena, “Suala hili lilikwishaamuliwa zamani, na sasa ni sehemu ya Katiba yetu. Uamuzi huo inafaa uheshimiwe. Rais Mwinyi ndiye Rais wa kwanza kuchaguliwa kwa mujibu wa Katiba hiyo. Yeye akisema kuwa vipindi viwili havitoshi, na akataka viwe vitatu; Rais wa pili atasema vipindi vitatu havitoshi, na atataka viwe vinne na kadhalika mpaka tufikie Ngwazi wa Tanzania,(uk.10).

Baada ya kusema hayo nije kwenye hoja yangu. Kuna jambo unaweza kutopendezwa nalo katika uongozi, maisha au kitu chochote, lakini wapo wanadamu wenzetu wanalivalia njuga na kulikumbatia wakiamini ni jambo bora. Hata kama ubora huo haufiki viwango na vigezo unavyotamani, lakini wenzako wanakumbatia.

Gharama za demokrasia ni pale anapojitokeza mtu kuwa kinyume cha wengi, kama alivyofanya Mbunge Juma Nkamia. Hili aliweza sana Samuel Sitta (Apumzike kwa aAmani). Sitta aliweza kusimama peke yake na kuhamisha fikra za watu katika masuala ambayo alikuwa akiyaamini.

Mfano wa karibuni ni mgongano uliowahi kujitokeza alipokuwa Mwenyekiti wa Bunge la Katiba na namna ilivyopatikana kamati ya kuandika Katiba Mpya iliyoongozwa na Andrew Chenge.

Wapo Watanzania wengine pia wamejaribu lakini wameshindwa, kwani wameishia kuwa wazungumzaji wenye moto lakini mantiki zao hupoa ndani ya saa 48 tu.

Nimeitazama barua iliyoandikwa na Juma Nkamia kwenda kwa Spika. Nikatafakari na kumfikiria mwenye ajenda husika. Nilikasirika kidogo, lakini nikajiuliza yafaa nini kutaka nilingane fikra na Juma Nkamia ambaye anapendekeza kuongezwa muda wa ubunge, ambao utachochea kubadilishwa muda wa madaraka ya urais hapa nchini.

Maoni yanaweza kuwasha washa, yakakupanikisha, ukachokozeka na kadhalika. Hata hivyo nakubaliana na Hillary Clinton kwamba mtu thabiti hawezi kukasirishwa na mguso wa unyoya.

Mimi siungi mkono ingawa sina mamlaka. Nihesabiwe hivyo, hata kama nina hisia kuwa hili ni “kubutua na kubadili mwelekeo uliopo sasa wa hali ya usalama wa raia hapa nchini,” bado hoja ya Nkamia inaudhi na kutafakarisha pia.

Inaudhi kwa kuwa ni sehemu ya demokrasia ambayo inatulazimu kumsikiliza. Inatafakarisha kwa kuwa inatulazimu kutafuta jawabu na hoja za kumpinga, kwamba muda unapoongezwa una uhusiano gani na maendeleo ndani ya nchi?

Kwamba kama muda wa Rais kubaki madarakani ukiongezwa, utachochea maendeleo nchini au utadhoofisha? Je, iwapo muda wa Mbunge kuwa madarakani utaongezwa ni jawabu la ufanisi na utekelezwaji wa ahadi zao kwa wananchi?

Kwamba kwa kuwa mbunge anakuwa na miaka mitano, ina maana haitoshi kukamilisha ahadi zake kiasi cha kuhitaji nyongeza ya miaka miwili tena, ikiwa na maana mihula miwili itakuwa miaka 14 na baadaye tutakuwa na wabunge haambiliki?

Hebu tazama mfano huu, imemchukua mwaka mmoja tu Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe na ofisi ya Mbunge jimboni humo kuwalipia karo wanafunzi wote wa kidato cha tano na sita katika shule za Serikali jimboni humo. Imemchukua muda huo huo kukabidhi magari ya wagonjwa kwa manufaa ya jimbo lake. Je, kuongeza muda wa mbunge kunaleta faida au hasara?

Pengine hayo ni maswali mepesi, lakini ninaanzia hivyo kuelekea kupata jawabu kamili juu ya nyongeza ya muda wa mbunge. Kwa mfano, Nkamia anaitumia Rwanda kama mfano wake.

Asichofahamu ni kwamba Rwanda walikuwa na sababu za msingi kutokana na historia ya nchi yao hivyo ikakubaliwa uongozi uwe wa miaka saba. Lakini Katiba sasa imebadilishwa, kwamba kuanzia mwaka 2024 Rwanda itakuwa na ukomo wa urais wa miaka mitano na si saba tena. Hii ina maana Rwanda wanatamani kuwa kama sisi halafu sisi tunataka kuwa kama wao wakati hatulingani historia zetu za kisiasa.

Nakiri kuwa sijashawishika na sioni sababu za msingi na hakuna ulazima wa kuongeza ukomo wa ubunge hapa nchini au hata ukomo wa urais kufika miaka saba bado sioni hoja za msingi hadi sasa maana akija mwingine tutasema tuongeze iwe miaka kumi na mwingine miaka 20. Aibu ilioje.

Tumekuwa tukiandaa visingizio vingi sana tunaposhindwa kutekeleza wajibu wetu kwa wananchi. Kuleta maendeleo kwa nchi si suala la miaka mitano au saba bali dhamira.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles