23.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 16, 2024

Contact us: [email protected]

NJELU KASAKA: HAKUNA ALIYE SALAMA

Na MWANDISHI WETU – ARUSHA

MWANASIASA mkongwe ambaye alipata kuwa mwenyekiti wa kundi la wabunge waliohitaji muundo wa Serikali tatu (G55) wakati wa utawala wa awamu ya pili, Njelu Kasaka, amesema hakuna mtu aliye salama ndani au nje ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Kauli hiyo aliitoa wakati wa mkutano mkuu wa kidemokrasia uliofanyika jana jijini Arusha ambako alikuwa mgeni mwalikwa.

Pasipo kutaja jina la mtu, Kasaka alitumia kauli hiyo kwa kugusia matukio ya kisiasa yaliyojiri katika siku za hivi karibuni.

Moja ya matuko hayo ni lile lililotokea katikati ya wiki hii kwa aliyekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye kukabiliana na changamoto ya kutishiwa bastola na mtu anayeaminika kuwa askari kanzu.

 “Ingekuwa wakati CCM ilipokuwa imeshika hatamu, suala hili la RC wa Dar es Salaam tayari CCM ingekuwa imeishakaa na kumuelekeza Rais cha kufanya juu ya mkuu huyo wa mkoa,” alisema Kasaka.

Alisema siku hizi hali haiko hivyo ndiyo maana hata Katibu Mkuu wa CCM mwaka 2015 kabla ya uchaguzi mkuu, alitaka kodi kero zifutwe, lakini ndio kwanza zikaongezwa.

“Ni kwa kuwa CCM ya sasa haina nguvu hizo tena, wapinzani wakiungana na kuondoa tofauti zao wanaweza kuiondoa CCM madarakani,” alisema.

Kasaka ambaye amepata kuwa mbunge, waziri na mkuu wa mkoa, alijitoa ndani ya CCM mwaka 2015 na kujiunga na Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Mbali na Kasaka, Kiongozi Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, alisema wamiliki wa vyombo vya habari na waandishi wa habari hapa nchini sio maadui wa Rais Dk. John Magufuli bali adui yake ni yeye mwenyewe.

Alimtaka Rais Magufuli badala ya kukasirikia vyombo vya habari ambavyo vinafanya kazi kubwa ya kuuhabarisha umma wa Watanzania, yeye binafsi ajitafakari na awe na akiba ya maneno pale anapozungumza.

“Sijui kilichomkasirisha Rais ni kitu gani, mimi binafsi nashangaa, anasema kalamu za waandishi ndizo zitasababisha mauaji ya halaiki kama ilivyotokea katika nchi za jirani, sio kweli, badala ya kurudia rudia kutamka mauaji ya kimbari ya Rwanda, sisi tunamwambia aache na aweke akiba ya maneno.

“Kama kiongozi wetu awe makini, awe mnyenyekevu na ajue hawezi kujua kila kitu, atuunganishe Watanzania, kwa sababu kile kilichotokea huko anakotolea kama somo ni matokeo ya utawala mbovu, ni itikadi ya jamii moja kujiona bora kuliko jamii zingine na ni matokeo ya wananchi kukosa matumaini,” alisema Zitto.

Pia alitumia fursa hiyo kuendelea kulaani kitendo kilichofanywa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam cha kuvamia Clouds Media huku akiwa na askari.

“Adui wa Rais Magufuli ni John Pombe Joseph Magufuli, ni kutokana na kuacha kutumia mifumo katika kutawala, matokeo yake viwanda havipanuki, ajira haziongezeki. Akirudi na kutumia mifumo atafanya vizuri.

“Serikali haitakiwi kuhangaika na watu wadogo wadogo waliowekeza mitaji yao na kuajiri wafanyakazi, wala haitakiwi kuwafilisi, bali inapaswa kuangalia, kujadili na kuziba mianya yote ya ukwepaji kodi unaofanyika katika nchi yetu,” alisema.

Akizungumzia dhana ya ujamaa, Zitto alisema tangu ujamaa ulipotupwa miaka 25 iliyopita pengo kati ya walionacho na wasio nacho limeongezeka na kiwango cha umasikini, hasa vijijini kinakua kwa kasi hali inayohatarisha umoja wa wananchi.

Kwa mujibu wa Zitto, hali hiyo imechangiwa kwa kiasi kikubwa na sera mbovu za CCM na Serikali yake na hakiwezi kukwepa lawama na shutuma kwani ndio chama kinachotawala hivi sasa.
Naye Mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini,  Godbless Lema (Chadema), alisema kuwa amepata maono mapya, kwamba ameona viongozi mbalimbali wa dini; masheikh na maaskofu wakichomwa moto kutokana na kutenda dhambi ya woga.
Lema alisema hayo wakati alipokuwa akitoa salamu za Chadema na kusisitiza umuhimu wa vyama vyote vya upinzani kuungana na kwenda kuwaelimisha wananchi madhara ya hofu na woga unaowakabili.

“Nimepata maono, nimeona viongozi wa dini, mashekhe na maaskofu wakichomwa moto wa jehanamu, nikamuuliza Mungu kwanini, mbona hawa wanachomwa moto, akanijibu kwa sababu ya dhambi ya woga,” alisema Lema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles