31.7 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Nimrod afyatuka

 Nimrod Mkono
Nimrod Mkono

NA AZIZA MASOUD,

MMILIKI wa kampuni ya uwakili ya Mkono & Co Advocates, Nimrod Mkono, jana aliishambulia kwa maneno makali Kampuni ya Yono Auction Mart & Co ambayo watumishi wake waliifunga ofisi yake mwishoni mwa wiki iliyopita.

Alisema waliofunga ofisi yake ni wahuni na vibaka ambao hajui sababu iliyowafanya waifunge na baadaye jana kuifungua ofisi yake.

Mkono ambaye pia ni Mbunge wa Butiama, alisema maneno hayo jana katika mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika ofisini kwake Dar es Salaam, siku moja baada ya kuondolewa kwa makufuli ya Yono yaliyokuwa yameifunga ofisi yake.

Alisema si kweli kwamba ofisi yake ilifungwa na Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) kama ilivyoelezwa awali, bali wahuni waliodai kuwa ameshindwa kulipa malimbikizo ya kodi inayofikia Sh bilioni moja.

“Si walifunga sijalipa kodi, waulizeni nimelipa? Watasema, hili si jukwaa la kura, nawaambia uwazi na ukweli. Duka limefungwa kwanini sijui wala sababu za kufunguliwa sijui, ningependa kusema duka lilifungwa kwa sababu zao na sasa limefunguliwa mimi nipo hapa.

“Ningekuwa nadaiwa wasingefungua duka wangelifunga mpaka kodi ipatikane, waliofunga si TRA, walikuwa ni vibaka na mimi sijui kwanini walilifunga na imekuwaje wamelifungua.

“Hao vibaka siwachukulii hatua watajijua wenyewe kwa sababu hawakuiba kitu. Kama ofisi wanaona haikulipa kodi labda hesabu zao hazikuwa vizuri. Nani hadaiwi kodi? Kila mtu anadaiwa kodi nyingine ndogo na kubwa hata pipi tu inadaiwa sembuse Mkono,” alisema Mkono.

Hata hivyo, alikataa kusema kiasi cha kodi anayodaiwa na badala yake alisema Serikali inafanya kazi nzuri na kodi lazima ilipwe kwa utaratibu uliowekwa.

Wakati Mkono akieleza hayo, taarifa zilizosambaa kwenye mitandao ya jamii zinadaia kuwa Mkono anaidai Serikali zaidi ya Sh bilioni 9 kwa kazi za kisheria ambazo amekuwa akizifanya. Hata hivyo, alivyoulizwa kuhusu ukweli wa taarifa hizo alikataa kuzizungumzia.

“Mwanasheria yeyote hawezi kusema anamdai kiasi gani mteja wake, haiwezekani duniani kote na haijawahi kutokea. Wakili huwezi kutoa siri ya mteja hata siku moja, kama nimeifanyia kazi Serikali ni siri yangu na Serikali, siwezi kutoka mbele ya kadamnasi kusema nawadai,” alisema Mkono.

Alisema ofisi yake inazungumza na TRA pamoja na Wizara ya Fedha ili kupata ufumbuzi wa jinsi ya kulipana fedha ambazo kila upande unadai upande mwingine.

Akizungumzia kauli hiyo ya Mkono, Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi wa TRA, Richard Kayombo, alikiri kufunguliwa kwa ofisi hiyo na kusisitiza kuwa waliofunga hawakuwa vibaka kama inavyoelezwa na Mkono bali ni mawakala wa TRA ambao waliagizwa kufanya kazi hiyo.

“Si vibaka na wala TRA haiwezi kufanya mambo  kienyeji, kampuni iliyofunga ni wakala wetu wa kudai madeni na wanatambulika na walipata baraka zote za TRA, deni lipo ndiyo sababu ya kufunga ofisi lakini tumefikia makubaliano ya jinsi atakavyolipa,” alisema Kayombo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles