30.2 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Ni mtihani Mbowe kung’oka, kubaki madarakani

NA MARKUS MPANGALA


MWANGWI umesikika tena hivi karibuni baada ya sauti ya Freeman Mbowe mwenyewe kuwaambia wale wote wanaotaka kuona anang’atuka basi watangoja kwa muda mrefu.

Kauli ya Mbowe imezua gumzo kubwa katika duru za kisiasa ambapo wapinzani wake wanahaha kila kukicha kuhakikisha anaondoka madarakani baada ya kushindwa chaguzi ndogo za udiwani na ubunge kwenye majimbo ya Ukonga mkoani Dar es salaam na Monduli mkoani Arusha, lakini mwenyewe amebainisha kuwa hana mpango wa kung’atuka.

Chaguzi ndogo zilizofanyika kwenye kata na majimbo hayo zimesababisha kamati kuu ya Chadema kutoa uamuzi kuwa chama hicho hakitashiriki uchaguzi mdogo wa ubunge katika Jimbo la Liwale mkoani Lindi.

Mbowe aondoke au abakie madarakani?  Hilo ndilo swali linalotawala kwenye duru za kisiasa nchini juu ya nafasi ya uenyekiti wa Mbowe anayeongoza Chama cha Demokrasia na Maendeleo-Chadema.

Mjadala huo unamzungumzia Mbowe ambaye alianza kuwa mwenyekiti wa Chama hicho tangu mwaka 2004.

Wakati mjadala huo unaendelea kufukuta chini kwa chini ni muhimu pia kuangazia mafanikio aliyoyafanya ndani ya Chadema.

Itakumbukwa kuwa katika Uchaguzi Mkuu wa ubunge, urais na udiwani wa mwaka 2005, Mbowe aligombea nafasi ya urais na kupata kura 668, 756 sawa na wastani wa asilimia 5.88, na kuambulia wabunge 19.

Mwaka 2010 Chadema kikiwa chini ya Mbowe katika Uchaguzi Mkuu wa rais, ubunge na madiwani wa Chadema kilipata wabunge wa kuchaguliwa 24 na viti maalumu 23.

Mbowe huyo huyo akiwa mwenyekiti wa chama katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 wa urais, ubunge na madiwani, Chadema kilivuna wabunge 34 majimboni na viti maalumu 36 na kuweka rekodi ya kuwa na wabunge 70 kabla ya Dk. Mollel(Siha), Julius Kalanga (Monduli) na Mwita Waitara (Ukonga) kujiuzulu na kuhamia CCM.

Chini ya uongozi wa Mbowe, Chadema kimekwepa mitego iliyoving’oa katika siasa za kuongoza Kambi ya Upinzani nchini, vyama vya NCCR-Mageuzi na Chama cha Wananchi -CUF.

NCCR-Mageuzi ndicho kilichokuwa kikiongoza upinzani baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 1995 chini ya mgombea urais wakati huo, Augustino Mrema na baadaye, nafasi hiyo kuchukuliwa na CUF, ambacho hata hivyo, baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005, kiliongoza Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kwa ushirikiano na vyama vingine, kiongozi wake alikuwa Hamad Rashid Mohammed na Naibu wake alikuwa Dk. Wilbrod Slaa.

Chadema kimejinusuru na mitego ya kuvurugwa pia kimejiongezea kura hata katika maeneo ambayo hakikuwa na nguvu za kisiasa kama Unguja na Pemba huko visiwani Zanzibar, ambako hata hivyo, kimetumia mgongo wa ushirikiano wa vyama vingine vitatu vya NCCR-Mageuzi, CUF na NLD, ingawa kwa Zanzibar, CUF ndicho kimekibeba zaidi Chama hicho.

Kwenye uchaguzi wa mwaka 2015 Chadema kilipata mafanikio zaidi baada ya kushirikiana na vyama vingine, huku mwanachama aliyeazimwa kutoka CUF- Juma Duni Haji, akikisaidia kupata kura kwa upande wa wapigakura wa Zanzibar.

Wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanasema Mbowe ni mmoja wa watu muhimu na katika siasa za upinzani na kwamba Chadema ndicho kilichokuwa kikiendesha kampeni za Umoja wa Katiba ya Wananchi- UKAWA dhidi ya chama tawala cha CCM.

Aidha, Mbowe amewahi kuwa Mbunge wa Hai mkoani Kilimanjaro mwaka 2000-2005.

Uchaguzi wa mwaka 2010 ulishuhudia Mbowe akiweka kando masilahi binafsi na kumkabidhi jahazi la kugombea urais aliyekuwa Mbunge wa Karatu, Dk. Wilbrod Slaa ambapo walifanikiwa kupata asilimia 27 ya kura za urais na wabunge 24 wa kuchaguliwa.

Tafsiri inayopatikana sasa ni kwamba Mbowe ni kiongozi muhimu aliyefanikisha mafanikio ya Chadema. Mbowe pia anasifika kuongeza idadi ya madiwani katika kata mbalimbali kutoka 39 hadi 376.

Vilevile wenyeviti wa mitaa na vijiji kutoka 116 hadi 3,960 kwa mwaka 2009 na mwaka 2014 walifikisha wenyeviti 6,780 (kabla ya kukumbwa na wimbi la hama hama ya madiwani wake).

Mara nyingi kwenye harakati za kugombea uenyekiti wa Chadema kumekuwa na misuguano mingi. Mbowe amekuwa kwenye hali hiyo dhidi ya Chacha Wangwe na Kabwe Zitto (kabla ya kufukuzwa uanachama wa Chadema).

Baadhi wamemtazama Mbowe kama kiongozi anayetakiwa kung’atuka  kwa kuwa amekiongoza chama hicho kwa kipindi cha miaka 14 mfululizo, lakini wengine wanaamini anastahili kuendelea. Hapo ndipo penye mjadala mkali mno.

Kiini cha shinikizo kutaka ang’oke:

Wapinzani wake ndani na nje ya Chadema wanaamini kuwa Mbowe amefanya makosa kadhaa ya kiufundi licha ya kukiongezea chama hicho umaarufu na idadi ya wawakilishi wa wananchi kwenye majimbo, kata, vijiji na mitaa.

Wanaamini kuwa Mbowe alichukua uamuzi mgumu uliokigawa chama kwa kumkaribisha Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa, kugombea urais kwa tiketi ya chama hicho pamoja na muungano wa vyama wa UKAWA.

Uamuzi huo unadaiwa kuwa chanzo cha kukimbiwa na aliyekuwa Katibu wake mkuu, Dk. Slaa pamoja na mwenyekiti Mwenza wa UKAWA, Profesa Ibrahim Lipumba.

Wakati wa harakati za kugombea uenyekiti wa Chadema uliofanyika mwaka jana, kulitokea msuguano kati ya pande mbili huku wengine wakisisitiza kwamba Mbowe asigombee.

Mnyukano wa makundi hayo mawili bado unaendelea huku Chadema kikiwa kinajitayarisha kwenye uchaguzi wake wa ndani mwaka huu na wa serikali za mitaa hapo mwakani.

Haiba ya Mbowe

Mazingira ya siasa nchini hayatoi nafasi kwa viongozi wa upinzani ambao hawana nguvu kiuchumi na kuwa na misimamo thabiti.

Tangu kurejeshwa mfumo wa vyama vingi vya siasa mwaka 1992 kumekuwa na kupanda na kushuka kwa baadhi ya vyama. Lakini Chadema kimekuwa juu kwa miaka 14 mfululizo kikiwa kinapanda na kuongeza uwezo wake.

NCCR-Mageuzi kilikuwa chini ya uenyekiti wa Augustine Mrema, lakini hakuhimili mawimbi yaliyotoka chama tawala pamoja na wapinzani wake.

Ikumbukwe kuwa Mrema alihamia TLP hakukuwa na cha mno mno. Tumeona uenyekiti wa Profesa Ibrahim Lipumba licha ya kupanda hadi chama chake kuongoza Kambi ya upinzani bungeni lakini kilishindwa kuhimili mitego kutoka chama tawala hadi pale mwaka 2015 kilipookolewa kwa ushirikiano na Umoja wa Katiba ya Wananchi-UKAWA.

UDP ni mfano mwingine ambao John Cheyo ameshindwa kukipaisha chama hicho na kimebaki kimefubaa zaidi.

Vyama vingine kama NLD, TADEA, Chauma havijafua dafu hadi sasa, kutokana na kukosa kiongozi mwenye nguvu ya kiuchumi na ushawishi ambaye anaweza kusikilizwa na maelfu ya wafuasi na wanachama wake.

Kwamba kiongozi mwenye nguvu ya kiuchumi anaweza kukipaisha chama na  hatakuwa na chanzo chochote cha kuyumbishwa na mitego ya chama dola.

Haiwezekani kiongozi mwenye uchumi mkubwa akalaghaiwa na vijisenti vichache na kukiuza chama kwa bei chee.

Haiba ya nguvu ya kiuchumi aliyonayo Mbowe ni sehemu nyingine muhimu inayoweza kutumiwa na Chadema kama nyenzo ya kuongeza nguvu na kukiimarisha chama chao.

Kwa muktadha huo Mbowe aking’oka madarakani Chadema itakuwa na kibarua kigumu cha kumpata mrithi mwenye misimamo thabiti asiyeyumbishwa na nguvu ya aina yoyote iwe ya kifedha au misuli ya Chama dola.

Mchambuzi wa masuala ya siasa nchini, Elisa Muhingo anasema ameunga mkono Mbowe kuendelea kuwa mwenyekiti wa Chadema. “Huu ni ushauri mzuri kuhusiana na nafasi ya mwenyekiti, hivi sasa Chadema kinaelekea kushindwa kwa mazingira ya sasa. Uongozi ukibadilika watasingiziwa viongozi wapya kuwa ndio wamesababisha. Hivyo Mbowe abaki kuwa mtu muhimu kwenye chama.”

Mtaalamu wa Sheria za Kimataifa ambaye pia ni kada wa Chama cha Mapinduzi (CCM) aishie mjini Geneva, nchini Uswisi, Lameck Kumbuka, amesema  nchi yetu inahitaji upinzani imara ambao utakisaidia CCM kutolala na kufanya kazi kwa bidii kila siku kutimiza Ilani yake.

“Nahofia kuegemea upande mmoja, kwa kuwa mimi ni Mwana-CCM, hata hivyo huwa ninajitahidi kuangalia mambo kwa uhalisia bila kumezwa na itikadi. Nchi yetu inahitahji upinzani imara, hata kama mimi ni kada wa CCM, naamini bila upinzania imara hatuwezi kwenda popote. Tunahitaji mawazo mbadala, tunahitaji kukosolewa na kuamshwa tukilala. Hayo yote yanawezekana kama kuna upinzania makini.

Kumbuka anaongeza kuwa; “Hiyo inanipa kibali cha kuongelea uenyekiti wa Mbowe. Ni wakati sasa kuondoka, kwa manufaa ya chama chake na kwa manufaa ya Taifa pia. Kuna damu changa, vijana wasomi wenye uzoefu katika chama, wapewe nafasi walete mabadiliko. Hakuna kitu kizuri na cha muhimu kama kuamini na kutambulisha mawazo mbadala  kwa kubadilishana madaraka. Mbowe ataheshimika sana akiwaachia vijana wengine na kubaki kama mshauri”.

Licha ya kukabiliana na upinzani ndani ya chama, Mbowe anaonekana kiongozi mwenye ushawishi miongoni mwa wafuasi wa Chadema. Makundi ya vijana ndiyo yenye nguvu kubwa kwa sasa na viongozi mbalimbali wa chama kote nchini.

“Nadhani ni muhimu sana kuleta mawazo na nguvu mpya. Sawa Mbowe ni kiongozi mzuri wa upinzani, lakini kuwa na mabadiliko ni muhimu zaidi,” anasema Kumbuka

Hii ina maana Mbowe anakubalika na kukataliwa ni suala lake mwenyewe kufanya tathimini kama inafaa aendelee au ang’atuke madarakani.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles