27.9 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Ni mateso

NA WAANDISHI WETU, DAR NA MIKOANI
NI mateso. Ndivyo unavyoweza kusema baada ya maelfu ya wananchi kukwama kusafiri, kutokana na madereva wa mabasi yaendayo mikoani kugoma jana.
Mbali ya mabasi yaendayo mikoani kugoma, jijini Dar es Salaam nako hali ilikuwa mbaya, baada ya madereva wa daladala nao kusitisha huduma ya usafirishaji.
Takwimu zinaonyesha karibu mabasi 300 hufanya safari kila siku kati ya Dar es Salaam, mikoani na na nchi jirani za Kenya, Uganda, Zambia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) Malawi, Burundi na Rwanda.
Hali hiyo ilianza kuonekana mapema asubuhi, baada ya abiria wengi kufika kituo cha mabasi Ubungo na vituo vya daladala na kukuta hakuna huduma yoyote.
Hali hiyo, ilisababisha mamia ya watu kukusanyika na kujikuta hawana la kufanya zaidi ya kusubiri magari ya watu binafsi ambako walitoa nauli kati ya Sh 5,000 hadi 7,000 kulingana na umbali ambao wanakwenda.
Kadri muda ulivyozidi kwenda, wakazi wa Dar es Salaam waliamua kuanza kutembea kwa miguu, kukodi pikipiki (bodaboda), bajaji na teksi na kutozwa kiwango kikubwa cha nauli.
Katika kituo cha Ubungo (UBT) ambacho kwa kawaida husheheni pilikapilika nyingi za usafiri, kwa siku ya jana hapakuwa na basi lililotoka wala kuingia, tofauti na siku zote.
Ndani na nje ya kituo hicho, kulikuwa na watu wengi wanaosafiri wakiwa nje ya mabasi waliokata tiketi, lakini wengi wao walionekana kukata tamaa.
Wakati abiria wakionekana kukata tamaa, baadhi ya madereva walionekana wamebeba mabango yenye ujumbe mbalimbali ambayo yalisomeka ‘JK madereva unatuachaje? kusoma, posho, mishahara, ajira, tunataka heshima kwa madereva.
Mengine yalisomeka ‘Tanzania bila madereva inawezekana? Mabomu ya machozi tumeyazoea, NIT (Chuo cha Taifa cha Usafirishaji) sio CCP (Chuo cha Mafunzo ya Polisi) na hati ya adhabu anazoandika Zuberi, Serikali inajua?
Hali hiyo, ilimlazimu Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani nchini, Mohamed Mpinga kutembelea eneo la Ubungo saa mbili asubuhi.
Alifika kituoni hapo, lakini hakufanya jambo lolote na baada ya muda mfupi kamanda huyo aliondoka.
SUMATRA
Ilipofika saa 3 asubuhi, Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA), ilitoa tangazo kwa abiria waliokuwa tayari kuahirisha safari ili warudishiwe nauli zao.
Meneja wa Mawasiliano wa mamlaka hiyo, David Mziray alitoa tangazo akiwa ndani ya gari la polisi.
“Ndugu abiria tunawatangazia yeyote ambaye anataka kuahirisha safari yake afike katika ofisi aliyokatia tiketi ili arudishiwe nauli yake,” alisema Mzirai.
Baada ya tangazo hilo, abiria mmoja alifika ofisi za Kampuni ya Majinja, ambapo wahusika waligoma kumrudishia nauli yake.
Mmoja wa mawakala wa basi hilo, Emiliana Kasebele alisema hawawezi kurejesha nauli hadi wapate idhini kutoka kwa wamiliki.
Mmoja wa abiria walikokuwa wakisaffiri kwenda mkoani Tabora, Issa Jafary alisema mgomo umeaathiri kwa kiasi kikubwa na kuitupia lawama Serikali kwa kushindwa kuutatua mapema.
Abiria huyo aliitupia lawama Serikali kwa kushindwa kutoa majibu ya haraka ili mgomo huo usijirudie.
Mgomo huo ulisababisha madereva kuhamasishana kutoka maeneo mbalimbali na kukutana Ubungo. Saa 5:05 wakiwa na gari aina ya Toyota DCM lenye namba za usajili T 748 DDA, haikujulikana mara mora walikuwa wanatoka wapi.
Ilipofika saa 5 asubuhi, taharuki kubwa ilitokea baada ya askari polisi kufyatua mabomu mawili ya machozi.
Hali hiyo, ilisababisha watu wengi kukimbia ovyo.
Kibaya zaidi, kijana mmoja ambaye jina lake halikufahamika mara moja, aligongwa na gari lenye namba za usajili T 977 DCF.
Baada ya kumgonga, dereva aliamua kujisalimisha kituo cha polisi Ubungo.
RC D’SALAAM
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadiq alionekana kuwa mwenye kigugumizi kuzungumzia mgomo huo.
Alipoulizwa alisema. “Subirini mtapewa taarifa lakini leo (jana) waziri mkuu atakutana na viongozi wa madereva” alisema.
UMOJA WA MADEREVA
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Umoja wa Madereva Tanzania, Rashidi Salehe aliliambia MTANZANIA kuwa wameitwa ofisini kwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kwa ajili ya majadiliano.
“Tumetaarifiwa na mkuu wa mkoa kwamba tukakutane na waziri mkuu…ndio tunaelekea huko,” alisema Salehe.

Kamati Maalumu
Hata hivyo taarifa zilizopatikana wakati gazeti linakwenda mtamboni zilieleza kuwa, kutoakana na mgomo huo Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ameunda kamati maalumu ya kudumu itakayoshughulikia matatizo mbalimbali ya usafiri nchini.
Akizungumza na waandishi wa haabri mjini Dar es salaam jana,Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta alisema kamati hiyo imehusisha wadau wote wa usafiri na imeanza kazi rasmi jana.
Alisema kamati hiyo, imeundwa na jopo la watu 13 akiwemo mwakilishi wa madereva ambapo lengo kuu ni kuhakikisha wakati wote bila kusubiri migomo kunakuwa na majadiliano shirikishi ya wadau na kuyapatia ufumbuzi.
“Mara kadhaa kumekuwa na migomo ya kushinikiza madai yatimizwe, hii si njia sahihi zipo njia za kudai haki,” alisema Sitta.
Alisema Serikali ina mwisho wa uvumilivu na haitapenda kuona wananchi wakiendelea kuteseka.
Alisema haitasita kuwachukulia hatua kali watakaoendelea na migomo hiyo.
Alisema wamebaini chanzo cha migomo hiyo ni kutokuwepo kamati ya kudumu ya usafiri.
“Suala la usafiri linahusu sekta nyingi, sisi wizara yetu inashughulikia sera lakini haisimamii sheria za usalama barabarani wala mikataba ya madereva na waajiri wao.

“Tatizo lilikuwa gumu kulishughulikia kwa sababu majibu yanatoka idara tofauti tofauti.
“Ninawaagiza Polisi kuwashughulikia watu hao kwani wanachangia migomo kuendelea,”alisema Sitta.
Alisema kuanzia sasa, Serikali imeunda utaratibu mpya ambao hauruhusu dereva kuendesha basi la abiria kwa zaidi ya kilomita 700.
HAKI ZA BINADAMU
Naye Mkurugenzi wa Taasisi ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (SAUTI), Fabian Haule amesema mgomo unaoendelea umechangiwa na Jeshi la Polisi kuwa madalali wa kukusanya kodi wakati si kazi yao.
“Kazi hii, inatakiwa kufanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kwa sababu ndiyo wanaohusika polisi tunawaomba wafanye kazi yao,”alisema.
Alisema kimsingi madai ya madereva yanatija na kudai haiwezekani wapewe fedha tofauti na waajiliwa wengine walioko serikalini, wakati taaluma ni moja.
“Utakuta dereva anatoka Dar es Salaam kwenda Kilimanjaro , akirudi anapewa Sh 50,000, huku familia na majukumu mengine yanamsubiri, eti alafu anaambiwa akasome,”alisema Haule.
Naye mmoja wa abiria waliokwama, Sharifa Hamadi alisema. “Tunataka turudishiwe pesa zetu au tuambiwe tutalala wapi na hatuwezi kuendelea kuwa hapa kwanza gharama zimekuwa juu hadi sasa chakula tu Sh 5000 na hapa sina hata fedha,” alisema.
KILIMANJARO
Huko mkoani Kilimanjario, mgomo huo uliathiri kwa kiasi kikubwa shuguuli za kila siku.
Mamia ya abiria walikwama kwenda sehemu mbalimbali za nchi katika stendi kuu ya mabasi mjini Moshi.
Hali pia imewakumba walimu wapya waliopangiwa vituo vya kazi kushindwa kuripoti katika maeneo yao ya kazi kwa wakati.
Mmoja wa abiria hao, Godbles Lema alisema mgomo unaoendelea umewaathiri na kusababisha biashara zao kuyumba.
Alisema mgomo huo, umeleta athari kubwa kwa wagonjwa baada ya kushindwa kwenda hospitali kutibiwa katika Hosptali ya Rufaa ya KCMC, kwani nauli ya Tax imepanda kutoka Sh 5,000 hadi 15,000.
MTWARA
Mkoani Mtwara, abiria walilazimika kukaa kituo kikuu cha mabasi kwa zaidi ya saa tano wakisubiri mgomo umalizike, bila mafanikio.
Akizungumza na MTANZANIA, mmoja wa abiria, Eric Msafiri alisema kitendo cha kugoma kimesababisha athari kubwa kwake kutokana na kutakiwa kuripoti kazini leo katika Halmashauri ya Wilaya ya Masasi.
Alisema Serikali inapaswa kusikiliza kilio cha madereva ili kupata suluhu ya matatizo waliyonayo.
DODOMA
Mkoani Dodoma, simazi ilitawala mji mzima kutokana na mgomo huo, ambapo mabasi yaendayo mikoani na daladala zinazotoa huduma katika maeneo mbalimbali ya mji huo yalisitisha huduma.
Hali hiyo ililazimu baadhi ya mabasi yaendayo mikoani kusafiri huku yakisindikizwa na gari za Polisi kwa hofu ya kushambuliwa na makundi ya watu njiani.
Baadhi ya mabasi ambayo MTANZANIA ilishuhudia yakiondoka kutoka katika kituo kikuu cha mabasi cha Dodoma, ni yale ya Kampuni ya Shabiby ambayo yalipewa ulinzi na polisi.
Akizungumzia mgomo huo, Meneja wa Kampuni hiyo, David Kenny alisema kampuni yao haina tatizo na Serikali hivyo hawana sababu ya kugoma kusafirisha abiria.
Kwa upande wa daladala, hali ilikuwa tete kutokana na magari mengi kugoma tangu alfajiri katika maeneo yote ya Manispaa ya Dodoma.
ARUSHA
Arusha nako hali ilikuwa mbaya tangu alfajiri, kitendo kilichomlazimu Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani hapa, Liberatus Sabas na Mkuu wa Usalama Arusha (RTO), Harison Mwakyoma kufika kituo cha mabasi kuamuru madereva waondoe magari.
Kamanda Sabas alifika stendi hiyo saa 3.51 asubuhi na kukuta mabasi yaendayo mikoani yakiwa yamepaki.
Aliwataka madereva kuondoa mabasi yote kwa vile eneo hilo si la kuegesha magari, kwani abiria waliolipa nauli wana haki ya kusafirishwa.
“Hapa si mahali pa kupaki magari, ondoa gari unafunga barabara, lazima usafirishe abiria vinginevyo utachukuliwa hatua za kisheria,”alisema.
Baada ya mvutano mrefu kati ya madereva na Polisi, ilipofika saa 4.43 asubuhi, mabasi yalianza kuondoka.
CUF walaani
Kwa upande wake Chama cha Wananchi (CUF), kimelaani mgomo huo na kueleza kuwa Serikali imeshindwa kushughulikia tatizo hilo tangu lilipoanza Aprili 10, mwaka huu.
Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari mjini Dar es Salaam jana na kusainiwa na Naibu Mkurugenzi wa Habari na Uenezi, Abdual Kambaya ilisema chama chake kinashangazwa na ukimya wa Serikali juu ya mgogoro huo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles