23.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

NI KUUMA, KUPULIZA AU KUZALIWA UPYA KWA SPIKA NDUGAI?

Na ELIZABETH HOMBO


WAKATI Bunge la 11 likiendelea na vikao vyake kujadili Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2018/2019 jijini Dodoma, Spika wa Bunge hilo, Job Ndugai ameanza kuzua gumzo baada ya kuonekana kubadilika.

Licha ya kulalamikiwa kwa muda mrefu na wabunge wa upinzani kuwa anakandamiza hoja zao, sasa wabunge hao wameanza kumsifia na kumwita mtu ‘strong’ (imara).

Malalamiko ya wabunge wa upinzani dhidi ya Ndugai yalianza kuibuka katika mikutano iliyopita hasa pale wabunge hao wanapotoa hoja ya kuikosoa Serikali.

Lakini wiki iliyopita mwelekeo mpya umeshuhudiwa na kuzua gumzo miongoni mwa wachambuzi wa mambo, iwapo ndiyo Ndugai amezaliwa kwa mara ya pili au ndio kule kuuma na kupuliza?

Hali hiyo iliibuka baada ya kuingilia kati mvutano ulioibuka bungeni kuhusu tofauti ya bei ya sukari kati ya Tanzania Bara na Zanzibar.

Kinyume na ilivyotarajiwa kuwa angekuwa upande wa Serikali, Ndugai alieleza wazi kuwa majibu yaliyotolewa na Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage hayatoshelezi.

Kutokana na hilo, Ndugai alisema swali lililoulizwa na Mbunge wa Mpendae, Salim Hassan Turkey (CCM) litaulizwa tena wiki hii ili Serikali itoe majibu ya kina, huku akisisitiza swali hilo ni la msingi na linapaswa kutolewa majibu mazuri na Serikali.

Mbali ya hiyo, Ndugai pia aliungana na Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe kuwa kuna umuhimu kwa Mwijage na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamis Kigwangalla kusafiri nje ya nchi ili kutafuta fursa za Biashara na Uwekezaji.

Itakumbukwa kuwa wakati Rais John Magufuli anaingia madarakani alisitisha safari za nje na zisizo na tija kwa watendaji wa Serikali na kueleza kuwa yeye, Makamu wake na Katibu Mkuu Kiongozi ndio watakaotoa vibali vya safari za nje.

Akiitikia mchango wa Zitto kwa Bajeti ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji ya mwaka 2018/2019, Ndugai aliwashauri mawaziri hao wawe wakisafiri nje ya nchi kutafuta masoko na kujenga uhusiano wa Kidiplomasia.

Akichangia bungeni, Zitto alisema Mwijage anaiendesha wizara hiyo kana kwamba ni Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) badala ya kuiongoza Kidiplomasia.

“Wizara ya Viwanda na Biashara tumepoteza Dola za Marekani bilioni moja (zaidi ya Sh.trilioni 2.4) katika kipindi cha miezi 24, ni sawasawa na kupoteza kila siku Sh. bilioni 3 kwa mwaka uliopita.

“Lakini bado upo hapa kwanini usijiuzulu? Umeshindwa kazi, huwezi kuendesha Wizara ya Viwanda na Biashara kama TAMISEMI, ni diplomasia kwenda nje kutafuta masoko.

“Malaysia, nenda huko ni rafiki wa Mwalimu (Julius) Nyerere, huwezi kujidanganya na viwanda vya cherehani, biashara ina nguvu na Wahindi waliopo hapa ni kutoka Bujarati zungumza nao waliopo hapa. Bidhaa zote zimeshuka bei unafanya nini,”alisema Zitto.

Baada ya Zitto kumaliza kuchangia, Ndugai alisema: “Ni kweli alichokisema Zitto, mawaziri lazima msafiri kweli, eeee, Waziri wa Biashara hawezi kukaa hapa na sisi, lazima asafiri, eeee, tumwombee popote pale kwenye mamlaka.

“Lazima asafiri sasa bidhaa zetu tutauza wapi? Kongwa, Kongwa kuna soko, Waziri wa Maliasili na Utalii aondoke wapige mawingu huko, ndio ukweli wenyewe. Sisi wabunge lazima tuwasemee,” Alisema Ndugai.

Hatua hiyo ya Ndugai kutoa misimamo ya aina hiyo, inatajwa kuwa anaonekana kubadilika ghafla tofauti na mwanzo alipokuwa akidaiwa kuwa ni chanzo cha mlolongo wa mizozo iliyokuwa ikiibuka ndani ya Bunge.

Pamoja na hilo, hata hivyo, baadhi ya wachambuzi wa mambo wanaonesha wasiwasi wao iwapo mabadiliko hayo yatakuwa ya kudumu kwa vile hii si mara ya kwanza kwa Ndugai kuonesha mwelekeo chanya kwa upinzani.

Wanatoa mfano katika Bunge la Bajeti la 2016/2017, alionekana kuwakosha wabunge wa upinzani na hivyo kumshangilia mara kwa mara, akiwa ndiyo amerudi kutoka India alikokuwa akipata matibabu.

Ikumbukwe wakati akipata matibabu nchini India, wabunge wa upinzani walikuwa na mvutano wa mara kwa mara na Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson ambayo ilikuwa ikisababisha wabunge wa upinzani kutoka nje ya ukumbi na wengine kupewa adhabu ya kuvikosa vikao vya Bunge.

Mvutano huo uliibuliwa hata katika Bunge hili la Bajeti ambapo wabunge wa Chadema, John Mnyika (Kibamba) na Esther Bulaya (Bunda) walitimuliwa ndani ya ukumbi wa Bunge na Dk. Tulia kwa madai ya kuendekeza usumbufu pindi Bunge lilipokaa kama kamati kupitisha Bajeti ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji.

Vivyo hivyo, kwa baadhi ya wenyeviti wa  Bunge, akiwamo Mussa Zungu ambaye naye alikumbwa na msukosuko kutoka kwa wapinzani ambao walisusa na kutoka nje ya ukumbi kwa madai kuwa analiendesha Bunge kibabe.

Wabunge hao waliongozwa na Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema na Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT Wazalendo).

Licha ya Naibu Spika na baadhi ya wenyeviti kuonekana kusuasua lakini safari hii hali imekuwa tofauti kwa Spika Ndugai.

Itakumbukwa kuwa baada ya kurudi kutoka India, Ndugai alihojiwa na kituo kimoja cha habari, ambapo pamoja na mambo mengine alieleza kusikitishwa kwake kwa hatua ya wabunge wa upinzani kutoka mara kwa mara nje ya ukumbi wa Bunge.

Kutokana na hilo, aliahidi yeye, Naibu Spika, wenyeviti wa Bunge watakaa pamoja na wabunge wa upinzani ili wamalize tofauti zilizopo kwa kuwa haipendezi spika kuongoza kikao halafu wengine wanatoka nje.

Pia alisema hali inayoendelea bungeni inachochea chuki na migogoro na hivyo bora wakae chini kama Taifa ili kumaliza hali hiyo.

Pamoja na ahadi hizo, haikuchukua muda matarajio waliyokuwa nayo wabunge wa upinzani kwa Ndugai yakatoweka.

Kama ilivyokuwa wakati wa Naibu wake, mivutano ya mara kwa mara baina ya kiongozi huyo wa Bunge na wabunge wa upinzani ikawa sehemu ya chombo hicho cha kutunga sheria.

Kwa kutaja mifano michache, miongoni mwa matukio ya kukumbukwa ni pale Spika Ndugai alipotoa kauli, ambayo iliibua mjadala mkubwa.

Ni baada ya kumwambia Zitto kuwa anaweza kumpiga marufuku kuongea awapo bungeni kwa miaka yote iliyosalia ya ubunge wake na kwamba hatomfanyia kitu.

Lingine ni pale alipokubali barua aliyoandikiwa na Mwenyekiti wa CUF anayetambuliwa na Msajili wa Vyama vya Siasa, Profesa Ibrahim Lipumba ya kuwavua uanachama wabunge wanane wa Viti Maalumu wa chama hicho.

Spika Ndugai alitoa uamuzi huo siku moja tu baada ya kueleza kupokea barua ya Profesa Lipumba na kusema anaitafakari kabla ya kutoa uamuzi wake.

Ndugai alichukua uamuzi huo huku akijua fika kuna mpasuko ndani ya chama hicho wa makundi mawili; moja ikiwa ni lile linalomuunga mkono Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad na lingine linalomuunga mkono Lipumba.

Pamoja na kwamba kanuni za Bunge zinamruhusu Ndugai kuchukua uamuzi huo lakini ingependeza angetumia busara kwa kuwa kuna mpasuko ndani ya chama hicho.

Lakini pamoja na yote hayo, tusubiri kuona kama anabadilika kulingana na upepo au pengine amezaliwa upya?

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles