26.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

Nguvu ya ziada inahitaji kwa maofisa ardhi

MOJA ya wizara ambazo zimekuwa na mafanikio makubwa tangu Serikali ya awamu ya tano ilipoingia madarakani, ni Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

Wizara hii inasifika kwa kutatua migogoro ya ardhi ambayo ilikuwa imeshamiri kila kona ya nchi yetu.

Migogoro hii, ilisababisha maafa makubwa yakiwamo ya wakulima na wafugaji kuuana kila kukicha katika mikoa ya Morogoro, Manyara, Arusha na Dodoma. 

Baada ya kuteuliwa kuongoza wizara hii, William Lukuvi  na naibu wake, Dk. Angeline Mabula wamefanya kazi kubwa ya kuwabadilisha watumishi wa wizara hii na kuwafukuza wengine.

Ndiyo wizara ambayo ilikuwa inatuhumiwa kwa rushwa  na kugawa kiwanja kimoja kwa zaidi ya watu wawili, jambo ambalo lilisababisha migogoro.

Tumeshuhudia mabadiliko makubwa yakiwamo ya kuwa na ofisi za kanda maalumu za kushughulikia migogoro hii ambayo imeanza kuzaa matunda.

Leo tumelazimika kuzungumzia wizara hii, kutokana na madudu ambayo yanaonekana bado yapo na yanahitaji nguvu kubwa kuyamaliza.

Inaonyesha wazi bado kuna wafanyakazi hawataki kubadilika au kwenda na kasi iliyopo ili kuwahudumia wananchi.

Jambo la kusikitisha, ni kitendo cha Idara ya Ardhi katika Halmashauri ya Wilaya ya Mtama mkoani Lindi kwa kuwa na viwanja 105 tu vilivyopimwa na kumilikishwa kwa wananchi ndani ya miaka 40 tangu kuanzishwa mwaka 1980.

Hali hii inasikitisha na kushangaza, miaka yote hiyo kupima  viwanja 105 tu. Tatizo ni nini hapa? Hakuna watendaji wa kutosha au watumishi wanafanya kazi kwa mazoea?

Madudu haya yameibuliwa wakati wa  ziara ya Dk. Mabula ya kuhamasisha ukusanyaji maduhuli ya Serikali kupitia kodi ya ardhi na kuangalia utendaji kazi wa sekta ya ardhi.

Dk. Mabula anasema pamoja na halmashauri kuwa ya siku nyingi, imeshindwa kupima maeneo na kuwamilikisha wananchi jambo lililosababisha hadi sasa kuwa na viwanja vichache.

Tunaamini kutomilikisha wananchi viwanja, pia kunaikosesha Serikali mapato yatokanayo na kodi ya pango la ardhi.

Lakini pia wananchi wengi wanakosa fursa ya kujiendeleza kiuchumi kupitia hati za ardhi ambazo zingeweza kutumika kuchukulia mikopo benki.

Hali hii inaonyesha wazi watumishi wa sekta ya ardhi hawafanyi kazi yao ipasavyo ama kuna uzembe ambao unapaswa kuchukuliwa hatua haraka iwezekanavyo.

Maajabu mengine yako Halmashauri ya Mtama ambako  mwaka mmoja wameanza hati mbili za ardhi. Hii inatia shaka kama kweli maofisa ardhi hawa wanatimiza wajibu wao ipasavyo.

Ni wazi Lukuvi na Mabula sasa wanapaswa kuchukua hatua za haraka kunusuru halmashauri hizi ambazo zinaonekana wazi utendaji wake  unatia shaka.

Tunasema haya  sababu mawaziri hawa wamekuwa wachapakazi usiku na mchana, ambao hawalali kuhakikisha wanamaliza uzembe uliopo kwenye wizara yao.

Sisi MTANZANIA, tunawasisitiza maofisa ardhi wa halmashauri zote kubadilika na kufanya kazi kulingana na kasi iliyopo ya Serikali.

Kutimiza majukumu yao kutasaidia kuingiza mapato ya Serikali na kuwapa wananchi hati ambazo zitawasaidia kukopa mikopo benki na kufanya biashara ambazo zitawasaidia katika masuala mbalimbali.

Lakini pia tunasisitiza waziri mwenye dhamana kuchukua hatua haraka Mkoa wa Lindi ambao unaonyesha wazi utendaji kazi hauridhishi. Kufanya hivyo kutasaidia kuleta mageuzi mapya ndani ya wizara hii. 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles