27.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

Ngeleja naye ajitosa, amwaga ahadi

SITTA TUMMA NA JOHN MADUHU, MWANZA

IDADI ya makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) waliotangaza nia ya kuwania urais kupitia chama hicho imefikia 11 baada ya Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja naye kujitosa rasmi.

Ngeleja alitangaza nia jana katika ukumbi wa Chuo cha Benki Kuu ya Tanzania (BoT) tawi la Mwanza.
Akionekana kubwana na maswali magumu kutoka kwa waandishi wa habari juu ya tuhuma mbalimbali za ufisadi, Ngeleja aliwaahidi Watanzania neema ya maendeleo yatakayotokana na uchumi wa kilimo, gesi, uvuvi, nishati ya umeme na kuapa kukomesha rushwa na mmomonyoko wa maadili.
Ngeleja mwenye umri wa miaka 48, aliyetumia saa 2:35 kunadi vipaumbele vya Serikali yake ya awamu ya tano iwapo atateuliwa na CCM kugombea kupeperusha bendera ya CCM katika uchaguzi mkuu Oktoba, mwaka huu.

UCHUMI
Alisema akifanikiwa kuwa Rais wa Tanzania, Serikali yake itasimamia vizuri ukusanyaji wa kodi na matumizi ya fedha za umma.
Ngeleja alisema uchumi wa Tanzania umekuwa ukikua kwa asilimia saba kwa miaka 10 mfululizo, huku tatizo la umasikini likipungua kwa kiwango cha asilimia mbili.
Alisema amekusudia kuwakomboa wananchi na lindi la umasikini ambalo limekuwapo muda mrefu.
“Naomba ridhaa ya kuwa Rais wa Tanzania ili ifikapo mwaka 2025, Tanzania iwe imefika kwenye uchumi mzuri…nitapunguza umasikini kwa kasi kubwa. Nitalinda tunu zote za taifa na ukiwamo Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
“Tangu nchi hii ipate uhuru mwaka 1961 mpaka sasa, asilimia 70 ya Watanzania bado wanaishi kwenye mazingira duni na nyumba zisizokuwa imara kwa sababu ya uchumi wao kuwa mdogo. Ndiyo maana nasimama kuomba ridhaa kuongoza ili wananchi waneemeke kimaendeleo,” alisema Ngeleja.
Alihoji sababu ya sekta ya kilimo kuchangia asilimia nne tu kwenye pato la taifa, wakati zaidi ya asilimia 75 ya Watanzania wanajishughulisha na kilimo.
Aliahidi kuwezesha Watanzania kwa kukopeshwa fedha kwa ajili ya shughuli za ujasiriamali na kutozwa riba nafuu.

GESI NA UMEME
Ngeleja alisema yeye ndiye mwasisi wa mradi wa bomba la gesi la kutoka Mtwara kwenda Dar es Salaam na iwapo Mungu akimbariki akakabidhiwa dola ataitumia gesi kukuza uchumi.
“Nitasimamia kuongezeka kwa mapato ya nchi na kutatua tatizo la mikopo kwa wanafunzi wa vyuo vikuu nchini. Gesi ikianza kuchimbwa nchini zaidi ya ujazo wa lita trilioni 70, nitahakikisha kila Mtanzania ameneemeka,” alisema.
Alisema ana ufahamu vizuri utajiri wa gesi, kwani mwaka 2009 akiwa Waziri wa Nishati na Madini, aliongoza ujumbe wa Serikali kwenda nchini China kwa ajili ya mazungumzo ya mradi huo.
Aliahidi kusimamia na kueneza huduma ya umeme vijijini na mijini, kama alivyousimamia Mpango wa Umeme wa Vijijini (REA) wakati akiwa waziri mwenye dhamana.

UFISADI
Katika hatua nyingine, Ngeleja aliyefuatana na mke wake, Blandina Ngeleja na mtoto wake wa kike, alipoulizwa maswali na waandishi wa habari kuhusu kashfa za ufisadi dhidi yake, ikiwamo ya kupokea rushwa ya Sh milioni 40 za sakata la uchotwaji fedha kwenye akaunti ya Escrow na kuondolewa kwenye Baraza la Mawaziri kwa shutuma hizo, alisema yeye si fisadi.

Alisema sababu ya kuondolewa kwake katika Baraza la Mawaziri na Rais Jakaya Kikwete mwaka 2012 haitokani na ufisadi, bali ni utaratibu wa kawaida unaoweza kufanywa na mkuu wa nchi kutokana na mamlaka aliyopewa kisheria.
Kama vile haitoshi, Ngeleja alijaribu kujisafisha kwa kusema hawezi kuzungumzia zaidi tuhuma za Escrow kwa sababu Desemba 22, 2014 Rais Kikwete alimaliza mambo yote kwa kusema hizo fedha hazikuwa za umma.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles