25.7 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

NGELEJA AHAHA SAKATA LA ESCROW

Na FERDNANDA MBAMILA- DAR ES SALAAM



HATUA ya Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja, kudai kupeleka Sh milioni 40.4 Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), akisema anarudisha mgawo wa fedha za Akaunti ya Tegeta Escrow, alizopewa na Mkurugenzi wa Kampuni ya VIP Engineering, James Rugemalira, imeacha maswali mengi kuliko majibu.

Baadhi ya maswali yaliyoibuka ni pamoja na endapo hatua yake hiyo itafanya asichukuliwe hatua nyingine za kisheria, kwa nini arudishe fedha hizo TRA na si kwa Rugemalira ama Benki ya Mkombozi ambayo ndiyo iliyopitisha fedha hizo kwenda kwenye akaunti yake.

Je, wenzake waliopata mgawo huo kutoka kwa Rugemalira nao watazirejesha fedha hizo? Kwa nini amerudisha Sh milioni 40.4 wakati alishalipa Sh milioni 13 kama kodi ya fedha alizopewa? Je, hatua yake ya kurudisha fedha hizo TRA haitatafsiriwa kama ni kuingilia kesi iliyoko mahakamani?

Baadhi ya maswali yalipata majibu jana, ikiwa ni pamoja na TRA kupitia Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi, Richard Kayombo, aliyesema taarifa za mbunge huyo kurejesha fedha walizipata kutoka kwenye vyombo vya habari.

“Tumesikia kama wewe ulivyosikia. Hatujui kama zimelipwa kweli na zimefuata utaratibu upi. Kwa sasa I have no comment,” alisema Kayombo.

Nao Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), imesema licha ya Ngeleja kurudisha fedha hizo, itaendelea na uchunguzi wake ili kujua kama alipozipokea alikuwa na nia ovu ama la.

Msemaji wa Takukuru, Mussa Misalaba, alisema: “Katika makosa ya jinai huwa inaangaliwa nia ovu na kitu anachofanya mtu, lakini matokeo ya jambo hilo, kinachoangaliwa ni nia ovu.

“Kwa hiyo katika uchunguzi kwenye ushahidi inaangaliwa je, nia ovu ilikuwepo halafu ndiyo mhusika anafikishwa mahakamani,” alisema.

Alipoulizwa endapo tayari Ngeleja amehojiwa, alisema: “Tangu kina James Rugemalira wafikishwe mahakamani, tulikuwa tunaendelea na uchunguzi wetu, hivyo siwezi kusema kama Ngeleja kahojiwa au vipi kwa sababu ni usalama wa kuchunguza.”

Hata hivyo, gazeti hili limedokezwa na moja ya chanzo cha habari kuwa juma lililopita Ngeleja alihojiwa na mamlaka hiyo.

Hatua hiyo ya Ngeleja inakuja wakati ambao vinara wa sakata hilo, akiwamo Rugemalira ambaye pia alikuwa mwanahisa wa Kampuni ya Independent Power Tanzania Ltd (IPTL), na Habinder Sethi Singh, Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni ya Pan African Power (PAP), wakiwa wameshafikishwa mahakamani.

Kwa mara ya kwanza walipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam Juni 19 na kusomewa mashtaka sita, yakiwamo ya uhujumu uchumi.

Julai 3, vigogo hao walifikishwa tena kwenye mahakama hiyo na kuongezewa mashtaka mengine sita, yakiwamo ya utakatishaji fedha.

Kwa jumla wake, mashtaka 12 waliyosomewa Rugemalira na Sethi Julai 3, ni pamoja na kutakatisha fedha na kusababisha hasara ya Dola za Marekani 22,198,544.60 na Sh 309,461,300,158.27 kwa Serikali.

KAFULILA

David Kafulila ambaye wakati akiwa mbunge alishikia kidete hoja hiyo ya Escrow, jana alisema uamuzi wa kulipa kodi wahusika waliufanya baada ya presha ya Bunge kwani hawakulipa walipochukua.
“Uamuzi wa kuzilipia kodi ilikuwa agizo la Serikali ambalo tangu mwaka 2014 nilisisitiza kuwa ilikuwa sawa na Serikali kuzitakatisha fedha ambayo ni jinai.

“Uamuzi wa Ngeleja ni hatua ya kwanza kwamba amekubali jinai na amerudisha na hivyo wenzake pia warudishe (asset recovery) ili wabaki na jinai ya kwamba walijipatia fedha hizo isivyo halali. Kifupi kurudisha fedha hizo haimwondolei jinai yoyote aliyehusika,” alisema Kafulila.

 

ALICHOSEMA NGELEJA

Akizungumza na waandishi wa habari jana Dar es Salaam, Ngeleja alisema ameamua kurudisha fedha hizo ili kulinda heshima yake na masilahi mapana ya nchi yake, chama chake, Serikali yake na familia yake.

Alisema alipokea fedha hizo kwa nia njema kama msaada wanavyopewa wabunge wengine, hivyo hakushtushwa na mchango kutoka kwa Rugemalira ili zimsaidie katika kutimiza majukumu yake ya kibunge, hususan kwa wananchi wa jimbo lake la Sengerema na taifa kwa ujumla.

Ngeleja alisema hata hivyo alizipokea fedha hizo kwa lengo la kutekeleza shughuli za kijamii kama vile ujenzi wa makanisa, misikiti na kusaidia kulipa karo za shule kwa wanafunzi wasiojiweza.

“Nilipokea fedha hizo kutoka kwa Rugemalira bila ya kujua kwamba fedha hizo zilikuwa zinahusishwa na kashfa ya akaunti ya fedha za Escrow kama ilivyo sasa, nimeamua kurudisha fedha zake za msaada hata kama aliyenipa bado ni mtuhumiwa, kwa vile hajathibitika kupatikana na hatia, kwa sababu sihitaji kuwa sehemu ya kashfa na tuhuma hizo,” alisema Ngeleja.

Alisema fedha hizo atazirejesha serikalini kupitia TRA, licha kuwa tayari alishazilipia kodi kiasi cha Sh 13,138,125 ambayo ni sawa na asilimia 30 ya msaada aliopewa kama alivyoelekezwa na TRA.

“Nimepima na kutafakari na hatimaye kuamua kwa hiari yangu mwenyewe kurejesha serikalini fedha zote nilizopewa kama msaada bila ya kujali kwamba nilishazilipia kodi ya mapato na risiti ya ushahidi wa kurejesha fedha hii hapa,” alisema Ngeleja.

Alisema kuwa kupokea msaada ni jambo la kawaida ila ikibainika una harufu ya uchafu hata kama haujathibitishwa na vyombo husika, ni vema kujiepusha nao.

Ngeleja aliongeza kuwa alipokea msaada huo kama wapokeavyo wabunge wengine kwa nia njema bila ya kujua kwamba Rugemalira baadaye angekuja kuhusishwa na kashfa ya fedha za akaunti ya Escrow kama ilivyo sasa.
Hata hivyo, Ngeleja alimpongeza kwa dhati Rais Dk. John Magufuli kwa utendaji wake wa kazi kubwa anayoendelea kuifanya katika kulinda na kutetea masilahi ya taifa letu.

Alisema anaungana na Watanzania wote wazalendo kumwombea Rais Magufuli kwa Mungu ili aendelee kufanya kazi kwa moyo.

Awali taarifa ya kupewa fedha iliripotiwa katika vyombo vya habari ya kuwa Februari 12 mwaka 2014, Ngeleja alipokea kiasi hicho cha fedha kutoka kwa Rugemalira kupitia akaunti yake yenye namba 00110102353601 ya Benki ya Mkombozi.

 

WENGINE WALIOLAMBA HELA ZA RUGEMALIRA

Mbali na Ngeleja, wengine waliopata mgawo wa fedha za Escrow kutoka kwa Rugemalira na kiasi wanachodaiwa kupewa kwenye mabano ni Mbunge wa Bariadi, Andrew Chenge (Sh bilioni 1.6) na Mbunge wa Muleba ambaye wakati huo alikuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka (Sh bilioni 1.6).

Wengine ni aliyewahi kuwa Waziri wa Nishati na Madini, Daniel Yona (Sh milioni 40.4), Mbunge mstaafu wa Sumbawanga, Paul Kimiti (Sh milioni 40.4) na aliyekuwa mjumbe wa Bodi ya Tanesco, Dk. Enos Bukuku (Sh milioni 161.7).

Wengine ni Jaji Profesa John Ruhangisa (Sh milioni 404.25), Jaji Aloysis Mujulizi (Sh milioni 40.4), aliyekuwa Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usajili wa Vizazi na Vifo – Rita, Philip Saliboko (Sh milioni 40.4), aliyekuwa Mkurugenzi wa Kituo cha Uwekezaji – TIC, Emmanuel Daniel ole Naiko (Sh milioni 40.4) na ofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania – TRA, Lucy Appollo (Sh milioni 80.8).

Kwa upande wa viongozi wa dini ambao waliingiziwa fedha hizo na Benki ya Mkombozi, ni Askofu Methodius Kilaini (Sh milioni 80.9), Askofu Eusebius Nzigirwa (Sh milioni 40.4) na Padri Alphonce Twimannye Simon (Sh milioni 40.4).

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles