27.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 16, 2024

Contact us: [email protected]

NEC yatoa sababu kusitisha ajira za uandikishaji wapigakura

Na ASHA BANI

-DAR ES SALAAM

SIKU moja baada ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kutangaza kusitisha ajira za muda za waandikishaji na wahakiki wa Daftari la Kudumu la Wapigakura, Mkurugenzi wa tume hiyo, Dk. Athumani Kihamia, ameeleza sababu za kufanya hivyo.

Ajira hizo zilitangazwa Mei 30, mwaka huu, kwa wenye elimu kuanzia kidato cha nne na umri wa miaka 18 hadi 45 kuomba nafasi kupitia tovuti ya NEC.

Pamoja na hali hiyo, juzi NEC ilisitisha ajira hizo huku ikiomba radhi kwa wale waliopeleka maombi na kuwapa pole kwa usumbufu uliojitokeza.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Dk. Kihamia alisema NEC ni taasisi yenye mambo mengi na mipango mingi hivyo pamoja na kusitishwa kwa ajira hizo, watatangaza tena na si kuzifuta moja kwa moja kama wengi walivyoelezwa.

“Taasisi hii ina mpango kazi na vitu vingi, hivyo kama tukiamua kutangaza tena mtaona kama ambavyo tangazo la awali lilionekana,” alisema Dk. Kihamia.

CHADEMA WAIBUKA

Kutokana na uamuzi huo wa NEC, Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema, alisema hawakubali uamuzi huo wa NEC na kudai kuwa imevunja Katiba ya ya nchi.

Alisema kwa mujibu wa kifungu cha katiba namba 343 ya mwaka 1985, ibara ya 15 (5) na 21 (5), NEC inatakiwa iwe imeboresha dafrari la kudumu mara mbili, lakini hawajafanya hivyo.

Mrema alisema kuwa NEC inatakiwa kusema uhakiki utafanyika lini tena badala ya kutoa tangazo la kusitisha pekee.

“Kwa mujibu wa kifungu cha 76 (15) (E), wakurugenzi hawatakiwi kusimamia uchaguzi tena kwa mujibu wa hukumu ya mahakama.

“Wasiwasi mkubwa hatujui kama tume imetengewa fedha na Serikali ya kufanya kazi hiyo au la, na ndiyo maana tunataka tume huru itakayoweza kujitegemea na kuwa na mfuko wake wa fedha na sio kutegemea serikalini tena ili kuepuka haya,” alisema Mrema.

Aliongeza kuwa taifa kwa sasa lina vijana milioni 5.6 ambao wanatakiwa kupiga kura, hivyo kutowaandikisha ni kuwanyima haki na kusababisha vurugu.

“Tunaitaka tume iandikishe vijana ili wapige kura na kuepuka machafuko hapo baadaye, ambayo hayatapendeza.

“Na tunataka taasisi za haki za binadamu na mashirika ya kimataifa watusaidie katika kupaza sauti juu ya hili,” alisema Mrema.

TAKWIMU 2015

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na NEC mwaka 2015 zilionesha kuwa waliotarajiwa kushiriki Uchaguzi Mkuu Oktoba 25, kati ya waliojiandikisha kupiga kura vijana ndio wengi.

Wapigakura vijana walio na umri wa kati ya miaka 18 na 35 walikuwa ni asilimia 57 ya wapigakura wote.

Wapigakura walio na umri wa zaidi ya miaka 50 ni asilimia 18 pekee, hao wengine asilimia 25 wakiwa na umri wa kati ya miaka 36 na 50.

Kwa jumla, wapigakura wote wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania walikuwa ni 23,253,982.

Takwimu hizo zinaonesha wapigakura wanaume ni asilimia 47 na wanawake asilimia 53, ikiwa na maana kwamba wanawake ni wengi kushinda wanaume.

NEC ilieleza kuwa baada ya uhakiki wa Daftari la Kudumu vituo vilipungua kutoka 72,000 vilivyotangazwa awali hadi 65,105 baada ya kubainika kuwapo kwa zaidi ya majina milioni moja yaliyoandikwa kimakosa.

Mara baada ya kukamilika kwa kazi hiyo, NEC ilitangaza idadi ya walioandikishwa kuwa ni 23,782, 558.

Ikiwa imebaki wiki moja kabla ya daftari hilo kupelekwa vituoni kwa ajili ya uhakiki na utambuzi wa vituo vya kupigia kura kwa kila mwananchi, tume ikiwa kwenye mkutano na viongozi wa vyama vya siasa ilitangaza marekebisho mapya yaliyopunguza idadi ya wapigakura na vituo.

Mwenyekiti mstaafu wa NEC wa wakati huo, Jaji mstaafu Damian Lubuva, alisema kila chama kilipaswa kutoa elimu kwa wafuasi wake ili wakatambue vituo vyao vya kupigia kura siku nane kabla ya Uchaguzi Mkuu.

Katika uchaguzi alisema upande wa Bara watapiga kura kwenye vituo 63,525 na wapigakura 503,193 wa Visiwani watafanya hivyo kwenye vituo 1,580.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles