23.3 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

NEC yaagizwa ikutane na vyama vya siasa

mussa zunguNa Maregesi Paul, Dodoma

BUNGE limeitaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ikutane na Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD), kuangalia namna ya kufanikisha uandikishaji wa wananchi katika Daftari la Kudumu la wapiga Kura.

Kauli hiyo ilitolewa bungeni juzi na Mwenyekiti wa Bunge, Mussa Zungu alipokuwa akijibu mwongozo wa Mbunge wa Kuteuliwa, James Mbatia.

“Waheshimiwa wabunge kama mtakumbuka leo asubuhi (juzi asubuhi), mheshimiwa Mbatia aliomba mwongozo kuhusu uandikishaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.

“Katika kushughulikia jambo hilo, tulikaa na Kamati ya Uongozi, Serikali, Wizara ya Fedha, Mbatia mwenyewe na wajumbe aliowapendekeza pamoja na wawakilishi wa TCD
“Kamati ya Uongozi imekubaliana TCD ikutane na NEC wiki ijayo ili kuangalia namna ya kufanikisha jambo hili na Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala ifuatilie utekelezaji wa suala hili na ilete taarifa Ijumaa,” alisema Zungu.

Wakati akiomba mwongozo wake juzi asubuhi Mbatia alitumia kanuni ya 47 inayomruhusu mbunge kusimama na kuliomba Bunge liahirishe shughuli za siku hiyo ili lijadili jambo la dharura kwa masilahi ya taifa.

“Mheshimiwa mwenyekiti, nchi yetu kwa sasa haina Daftari la Kudumu la Wapiga kura kwani Julai 9 mwaka jana, Tume ya Uchaguzi (NEC), ilitwambia daftari lililokuwapo ni chafu, limechafuliwa na hivyo linahitajika jipya litakaloandaliwa kwa mfumo mpya wa kielektroniki wa BVR.

“Katika hili, NEC walituhakikishia kwamba, daftari la kudumu litaanza Septemba mwaka jana, lakini wakashindwa kufanya hivyo na kusema wataanza Oktoba, lakini pia wakashindwa.

“Baadaye tuliambiwa wataanza Novemba mwaka hana huo huo, lakini wakashindwa na kuanza majaribio katika wilaya tatu nchini ilipofika Desemba mwaka jana.

“Januari mwaka huu, Mwenyekiti wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD), John Cheyo, aliwaalika NEC katika kikao chetu na walipokuja, walitwambia kuna changamoto nyingi katika utekelezaji wa zoezi hilo, lakini wakasema Februari 15 mwaka huu, zoezi litaanza baada ya wao kukutana na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC).

“Jambo la kushangaza ni kwamba, jana (juzi), NEC wametangaza kuanza kwa zoezi hilo katika Mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma bila hata sisi wadau kushirikishwa wakati walitwambia watakuwa wakitushirikisha kila hatua” alisema Mbatia.

Katika hatua nyingine Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, amesema Serikali imeiagiza Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), kuangalia utaratibu utakaowawezesha Watanzania wanaoishi nje ya nchi kupiga kura katika uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu.

Pinda alitoa kauli hiyo bungeni jana wakati akijibu swali la Mbunge wa Mkanyageni, Mohamed Habibu Mnyaa (CUF) wakati wa kipindi cha maswali ya papo kwa hapo kwa waziri mkuu.

Katika swali lake, Mnyaa alitaka kujua Serikali imefanya maandalizi gani katika uchaguzi mkuu ujao utakaowawezesha Watanzania wanaoishi nje ya nchi kutimiza haki ya kupiga kura kama ilivyofanyika katika Bunge Maalumu la Katiba, ambapo wajumbe wa Bunge hilo waliokuwa nje ya nchi waliruhusiwa kupiga kura kupitisha Katiba inayopendekezwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles